IMEELEZWA kwamba, baadhi ya shule za msingi na sekondari jijini Dar es Salaam zinazozungukwa na makazi ya watu, maeneo ya biashara na zisizokuwa na uzio, zimekithiri kwa vitendo vya utovu wa nidhamu, ambapo wanafunzi wanalawitiana na wengine huvuta bangi.

Vitendo vya kulawitiana vilianza kuripotiwa na gazeti hili, Desemba, 2012 baada ya watoto zaidi ya sita wa Shule ya Msingi Mbuyuni iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam, kubainika kufanya vitendo hivyo.
Wakati wa uchunguzi huo, ilielezwa vitendo vya kulawitiana, ngono zembe na uvutaji bangi katika maeneo ya shule za msingi na sekondari, vinafanywa kati ya mwanafunzi na mwanafunzi na kati ya vijana wa mitaani na wanafunzi.
Wakati wa wanafunzi kujihusisha na vitendo hivyo, ilielezwa kwamba, wakati mwingine hutumia nyumba za wakazi wa jirani na shule wanazosoma.
Wakati hofu hiyo ikitanda ndani ya jamii, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillipo Mulugo, zaidi ya watoto 160,000 wenye umri chini ya miaka 15, wamekuwa wakilawitiana na hivyo kuambukizana maradhi mbalimbali ukiwamo Ukimwi.
Mulugo alitoa takwimu hizo Oktoba 12, 2012 wakati akifungua mkutano wa wadau wa elimu ya Ukimwi chini ya mradi wa kukuza uelewa juu ya virusi vya ugonjwa huo, katika shule za msingi ambao umefadhiliwa na Serikali ya Ubelgiji.
Mulugo alisema watoto hao wamepata ugonjwa huo kutokana na vitendo vya kulawitiana pindi wawapo shuleni, wengine kuupata kwa kuzaliwa nao na kwamba katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imeandaa walimu wawili kila shule, ili kusaidia kutoa elimu juu ya matatizo hayo kwa watoto walioko shuleni.
Pamoja na mambo mengine, alitoa wito kwa wazazi kuwaeleza mara kwa mara watoto wao madhara ya kulawitiana pindi wawapo shuleni, kwa kuwa vitendo hivyo vinawaadhiri kisaikolojia.
No comments:
Post a Comment