Tuesday, September 17, 2013

Wapinzani sasa kukutana na taasisi kuhusu katiba mpya

SIKU moja baada ya vyama vya upinzani kumtahadharisha Rais Jakaya Kikwete asisaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, leo vinatarajia kuanza kukutana na taasisi na makundi mbalimbali. Katibu wa Muungano wa Vyama hivyo, John Mrema alisema jana kuwa lengo ni kuwaomba kuunganisha nguvu bila kujali itikadi zao kunusuru mchakato wa katiba mpya.



Vyama vilivyoungana ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR Mageuzi.

Mrema ambaye pia ni Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa Chadema alisema vikao na taasisi hizo utakuwa wa wazi kwa waandishi na watu wengine kusikiliza na kutoa machango wao kadri watakavyoona.

“Suala la katiba mpya hatutaki kulifanyia mzaha kama Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinavyotaka kuwadanganya wananchi, kesho (leo) tunaanza ratiba ya kukutana na wadau mbalimbali kuangalia mustakabali mzima wa mchakato wa katiba mpya unavyoendeshwa.

“Kwa leo hatujaandaa ratiba rasmi lakini kuanzia kesho (leo) itawekwa wazi kila mtu ajue tunakutana na watu gani, hatutaki kufanya jambo hili kwa kujificha kwa sababu katiba ni ya Watanzania wote,”alisema.

Mrema alisema wanatarajia kukutana kwa nyakati tofauti na asasi za raia, taasisi za dini, vyama vingine vya siasa, taasisi za elimu ya juu, vyama vya wafanyakazi, jumuiya za wakulima, wafugaji na wavuvi.

Nyingine ni taasisi za sekta binafsi, jumuiya za watu wenye ulemavu, asasi za wataalamu wa masuala mbalimbali, jumuiya za wanawake, vijana, vyama vya wastaafu na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana lengo likiwa ni kupinga mchakato wa katiba kuhodhiwa CCM na Serikali yake.

Vyama hivyo juzi vilimtaka Rais Kikwete kutodhubutu kusaini muswada huo vikidai anaweza kusababisha machafuko.

Msimamo huo ulitolewa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia.

No comments:

Post a Comment