Wednesday, October 9, 2013

MAHAKAMA YAKUBALI KAMPUNI 5 KUIPINGA #SIMCARD_TAX 2013-14

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam imekubali maombi ya Kampuni tano za Simu nchini kutaka kuingia katika kesi ya kupinga tozo ya kodi ya Shilingi 1000 kwa kila laini ya simu kwa mwezi, inayotakiwa kulipwa na watumiaji wa simu.

Hatua hiyo ya Mahakama imekuja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwasilisha pingamizi la awali la kupinga maombi ya Kampuni za Simu za MIC Tanzania Limited, Vodacom, Airtel, Zantel pamoja na TTCL ambazo ziliomba kuingia katika maombi hayo yaliyofunguliwa hivi karibuni na Chama cha Kutetea Haki za Walaji nchini.
Akiongoza Jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu wanaosikiliza kesi hiyo, Jaji ALOYSIUS MUJULUZI amesema Mahakama mbali na kukubali maombi hayo imeagiza Chama cha Walaji kuifanyia marekebisho hati ya Kiapo ili kuyaambatanisha maombi ya Kampuni hizo na kuiwasilisha mahakamani ifikapo Oktoba 15 mwaka huu.
Jaji MUJULUZI amesema baada ya hati hiyo kuwasilishwa itakabidhiwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili aipitie kabla ya kusikilizwa kwa maombi ya zuio la muda la utekelezaji wa Sheria ya utozaji wa Kodi kwa laini za simu ifikapo Octoba, 21 mwaka huu.
Katika kesi hiyo upande wa Serikali uliwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali ALESIA MBUYA huku wakili wa Kampuni za Simu akiwa ni FATUMA KARUME na Chama cha Kutetea Haki za Walaji nchini kikiwakilishwa na DK ALEX NGURUMA .

No comments:

Post a Comment