Wednesday, October 9, 2013

WAMILIKI WA MALORI WAMEITAKA SERIKALI KUCHUKUA HATUA ZA HARAKA

Ikiwa ni siku ya tatu sasa tangu Wamiliki wa Malori wasitishe kutoa huduma kwa madai ya kulinda barabara zisiharibike hii leo wameitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kulipatia ufumbuzi suala la punguzo la uzito kwa asilimia tano kwenye mizani ya barabarani ili kunusuru uchumi wa nchi
.
Wamiliki hao wa malori wamesema iwapo wataendelea kutoa huduma upo uwezekano wa kuwepo kwa foleni kubwa za magari kutokana na sheria hiyo mpya iliyotangazwa na Waziri wa Ujenzi Dk. JOHN MAGUFULI kuanza kutumika kwani mizigo mingi iliyopo Bandarini imekuja kwa uzito wa awali na hakuna uwezekano wa kuifungua na kuipunguza.
Wamiliki hao akiwemo FAITHAR EDHA, IBRAHIM MASANGU na DEVIS MOSHA wakizungumza kwa niaba ya wenzao wamesema wameandika barua nyingi Serikalini hususan kwa Waziri wa Ujenzi lakini hakuna majibu waliyopewa wala Waziri hajaonyesha dalili za kufanya mazungumzo nao tangu aingie madarakani.
Aidha wamiliki hao wamesema kwa sasa hawajaamua kwenda mahakamani wanachokisubiri ni majibu kutoka serikalini kabla ya kuchukua hatua zozote ambapo kwa muda wote wanaosubiri hawatatoa huduma yoyote inayohusisha magari yao ikiwemo kusafirisha mafuta na kusafirisha mizigo iliyopo Bandarini.
Kupumzishwa kwa maroli hayo jana kulisababisha mabasi ya mikoani kugoma kwa muda huku wamiliki wake wakilalamikia kupunguzwa kwa asilimia tano ya uzito kwenye mizani na kusababisha usumbufu kwa abiria hali iliyomlazimu mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam SAID MECK SADICK kuruhusu mabasi ya abiria kupita kwenye mizani bila kupima kwa muda

No comments:

Post a Comment