ALIYEKUWA Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Nicholus Kuhanga, amesema upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wanaoanza vyuo vikuu nchini ni tatizo na kuishauri serikali kuingia kwenye mpango wa kuwakopesha kupitia benki.
Kuhanga alitoa kauli hiyo alipozungumza nasi kuhusu suluhu kwa wanafunzi wanaohitaji mikopo ambao wamekidhi vigezo lakini hawakupata.
Alisema ili kuondoa tatizo hilo serikali inatakiwa kuingia kwenye mpango huo ambao unatumiwa na nchi nyingine, ili kuondoa mgongano uliojitokeza kati yake na wanafunzi.
“Kwa kutumia mfumo wa benki nafikiri kila mmoja ataweza kunufaika na mkopo, watakapomaliza watatumia vitambulisho vyao ili kuanza kuzirejesha,” alisema na kuongeza kuwa wale ambao watakuwa hawana vigezo vya kupata mkopo benki, ndio wasaidiwe na Bodi ya Mikopo Tanzania (HELBS).
Alisema serikali haina fedha ya kutosheleza kumlipa kila mhitaji, japo wazo la kuanzisha bodi hiyo lilikuwa kwa serikali isaidie kuongeza idadi ya wanaokwenda vyuo vikuu kutoka katika familia za wasiojiweza.
Naibu Makamu Mkuu wa UDSM, alisema bodi ina bajeti kwa idadi fulani, hivyo wale ambao hawakupata sasa ni jukumu la wazazi, ndugu na jamii kuwasaidia.
No comments:
Post a Comment