Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Lipumba alisema maelezo yaliyotolewa na polisi ya kumhusisha Sheikh Ponda na vurugu hizo hayana ushahidi wowote bali yanaongeza mfarakano katika jamii.
"Unaweza usikubaliane na Sheikh Ponda katika maelezo na msimamo wake kuhusu dhuluma dhidi ya Waislamu, lakini ni makosa kumsingizia mambo ambayo hakuyatenda,"alisema.
Profesa Lipumba alisema hata kesi aliyoshtakiwa Sheikh Ponda ni ya kuvamia kiwanja kisichokuwa chake kilichokuwa kinamilikiwa na East African Muslim Welfare Society kwa madhumuni ya kujenga Chuo Kikuu cha Kiislamu na kwamba kesi hiyo ni ya Mahakama ya Ardhi.
Alisema anachodai Sheikh Ponda ni kuwa kiwanja hicho cha Waislamu kimeuzwa kinyume na utaratibu na sheria zinazolinda mali ya Waqfu.
Lipumba alisema mwenye kiwanja alistahili kwenda Mahakama ya Ardhi na kueleza kuwa kiwanja chake kimevamiwa, hivyo kutumia polisi kumkamata Sheikh Ponda kumechochea vurugu hizo.
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, matamshi ya Kamanda Kova ya kumuhusisha Sheikh Ponda na uchomaji wa makanisa jambo ambalo hakuhusika nalo na kutoa wito kwa wafuasi wa Sheikh huyo kujisalimisha polisi ndiko kulikochochea maandamano ya Ijumaa iliyopita.
Alisema kitendo cha kuwaingiza barabarani askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kupambana na raia ni kitendo cha aibu na cha kusikitisha kwani kazi ya wanajeshi ni kulinda mipaka na siyo kwenda kupiga raia wanaoandamana.
Lipumba aliitaka Serikali iepuke kujenga uhasama kati ya Jeshi la Wananchi na raia.
CUF pia imemtaka Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua za kuleta maelewano ya kujenga utamaduni wa kuvumiliana baina ya Watanzania wenye imani tofauti.
By Abdulswamadu M Ally
No comments:
Post a Comment