WINGI wa vyuo vidogo vinavyotoa mafunzo ya utalii na teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) nchini unaisababishia serikali kutokuwa na uhakika wa ubora wa wahitimu wanaomaliza katika vyuo hivyo.
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, wakati akizindua Tume ya Tehama iliyowashirikisha wadau wa mawasiliano kutoka taasisi binafsi na za kiserikali.
Makamba alisema kuna vyuo vingi vinasema vinafundisha masomo ya Tehama lakini hakuna uhakika, takwimu na ubora wa wahitimu katika sekta hiyo nchini.
Alisema jambo hilo ni kubwa zaidi ya Tehama kwa sababu wapo makanjanja wengi wa Tehama, hivyo kuwepo kwa tume hiyo kutasaidia kudhibiti changamoto hizo na kuwatambua wahitimu wenye vigezo.
“Tume hii itakuwa inaratibu masuala mbalimbali yanayoendeleza Tehama, ningependa kuona wadau wengi binafsi wanashiriki ili kuibua miradi mikubwa ya mawasiliano yenye sura ya kitaifa.
“Lakini ndani ya serikali kuna watu wana shaka na tume hii kwamba watanyang’anywa baadhi ya majukumu…nawahakikishia kwamba hakuna taasisi inayoweza kuwa na kiburi, kwa sababu serikali ndiyo baba; itachukua hatua kama taratibu zikikiukwa,” alisema Makamba.
Akizungumzia Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom, Salum Mwalimu, alisema tume hiyo itasaidia kukuza sekta ya mawasiliano kwa sababu wadau watakuwa wanafanya kazi pamoja, huku akitolea mfano Vodacom kwa kusema sasa inaishirikisha wizara katika mpango wake wa kusaidia wanafunzi masuala ya Tehama katika shule mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment