Friday, May 31, 2013

TUNAFICHAFICHA YA KIFO CHA NGWEA, ILI TUWAUE WENGINE…

MSIBA umetokea, hakuna kinachoweza kuepukika kwa maana ya kwamba Albert Mangwea ametutoka na
unga 
kinachotakiwa kwa sasa ni kuungana, kuwa watulivu, kusahau tofauti za kawaida za kibinadamu zilizopo na kumsindikiza kwa amani.
Albert au Mangwea amepita njia sahihi, njia ambayo kila mmoja wetu aliye hai atapita kwa maana ya kuwa kila nafsi itaonja mauti, hilo halina mjadala.
Mkubwa zaidi yetu wote ni Mwenyezi Mungu, lakini haiwezekani tumuachie kila kitu kwa zile kauli tulizozizoea kwamba “ni mapenzi ya Mungu” au “tulimpenda lakini Mungu amempenda zaidi.”
Tukikubali hilo, sawa lakini mbele kutakuwa na tatizo kwa maana ya kuamini Mangwea angeweza kuishi zaidi na inawezekana imekuwa mapema zaidi kwa kuwa kuna mambo kadhaa hatukuweza kuyafanyia kazi mapema.
Gumzo kubwa linalohusiana na kifo chake ni dawa za kulevya, lakini inawezekana familia yake ikaona kujulikana kwa suala hilo ni kama aibu kwao na ikapigana kutaka kuwazuia watu wasizungumze au kutaja suala hilo.
Bado tutaendelea kusubiri ripoti ya daktari, achana na ile feki iliyosambazwa na magazeti mengine yakaingia mkenge na kuitumia yakiamini ilikuwa sahihi. Lakini familia yake itakuwa na uungwana kama itaeleza hadharani kuhusiana na ripoti sahihi itakapotoka.
Kuna tofauti kubwa ya Mangwea na Mtanzania wa kawaida kama Saleh Ally, tayari Mangwea ni maarufu, mtu wa watu wengi sana. Hivyo familia yake si ile ya Mzee Mangweha pekee, badala yake watu wote waliokuwa wanamuunga mkono wakati wa uhai wake alipokuwa akifanya kazi za usanii.
Hakika watataka kujua hasa, mimi ni mmoja wapo, lakini kama itaonekana kweli Mangwea kifo chake kilisababishwa na madawa ya kulevya, basi ukweli uwekwe hadharani na tutumie hasara ya kumpoteza kijana kama yeye kuwakumbusha au kuwalilia vijana wengine wa Kitanzania ambao ni nguvu kazi ya taifa, waache mara moja.
pombe kali !
Tunajua wako wasanii lukuki wanaovuta unga, nyie mna hofu kuwataja. Banza Stone, Msafiri Diouf wamekuwa wakipigana kuepuka kuondoka huko, lakini suala “siri” limekuwa msaada mkubwa kwao ili waendelee kufanya upuuzi huo.
Siri inataka kutumika tena katika msiba wa Mangwea, wako wanaoona kusema alikuwa anatumia madawa ya kulevya ni sawa na kumdhalilisha marehemu. Hivyo wanashika ‘mtutu’ kutaka kupambana na kila anayejaribu kusema hilo.
Niliwahi kuzungumza na Mangwea takribani miezi tisa iliyopita, nilimhoji kuhusiana na taarifa za matumizi ya ‘unga’, kwa kuwa nilikuwa namchukulia kama mdogo wangu, alikubali lakini akanisisitizia kwamba alishaacha, japokuwa mpenzi wake aliyekuwa naye pale, akatikisa kichwa kunionyesha kwamba alikuwa bado anaendelea na alichokuwa akinieleza hakikuwa sahihi.
Mara ya mwisho nikakutana naye Mlimani City, ilikuwa mwanzoni mwa mwaka huu nikiwa nimeongozana na John Joseph, Mhariri wa Championi Ijumaa. Nilizungumza na Mangwea maneno kadhaa, lakini mwisho nilimuuliza, “Yale mambo bado?” Nikimaanisha kama anaendelea kutumia.
Alinijibu hivi, “Nimetupa kule mtu mzima, angalia hata muonekano wangu kwa sasa”. Alikuwa anamaanisha kwamba amependeza, hiyo ilikuwa ni mara yangu ya mwisho kumuona, nasikia uchungu kutokana na ‘aina’ ya Mangwea, hakika alikuwa muungwana, anayejiheshimu na kuheshimu wengine, lakini kipaji chake kilikuwa cha aina yake.
Leo sijisikii nina makosa, kama madawa ya kulevya yatakuwa chanzo au sehemu ya chanzo, bado naona nimekuwa mkweli, angalau niliwahi kumueleza.
Jiulize wewe rafiki yake wa karibu ambaye hukuwahi kuinua mdomo na kusema lolote kumshawishi aachane na upuuzi huo, unajisikiaje leo? Lakini wewe ambaye unataka kuendelea kuficha hadi leo kwa kisingizio cha heshima, bado unaona unachofanya ni sahihi?
Taarifa za kifo chake nilizipata kutoka Afrika Kusini, rafiki zangu wengi wa huko walinieleza kwamba Mangwea alikufa kutokana na kuzidisha utumiaji wa madawa hayo. Ingawa walikuwa hawaelewi ilikuwaje lakini wako walisisitiza hilo la madawa ya kulevya.
Hata juzi mchana nilipoziona picha za mwili wake kwa mara kwanza zikiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti, nilisikia uchungu kwa kuwa povu la damu lililotoka mdomoni na puani na baadhi ya Watanzania wanaoishi Afrika Kusini wakasisitiza yote hiyo ni kutokana na kuzidisha matumizi ya madawa hayo ya kulevya.
Tunajua Mangwea alikuwa ni mtumiaji wa ‘unga’, sasa ni vizuri tukawaokoa wengine ambao wanaendelea kutumia. Hasara ya kumpoteza Mangwea si ya familia yake tu, hasara tena kubwa kwa taifa letu la Tanzania.
Kama tutaendelea kuficha eti kwa ajili ya kulinda heshima ya marehemu, basi tutajiangusha wenyewe, tutajiweka katika hali ngumu zaidi na huenda tukaendelea kuwapoteza watu wengi zaidi kila kukicha na hasa vijana.
“Mficha uchu hazai”, najua shida yetu si kuzaa, ila ni kuwabakisha vijana waendelee kulitumikia taifa kwa maana ya wao wenyewe, familia zao na taifa kwa ujumla. Tukiendelea kuficha matatizo, basi tutayakuza zaidi na kuendelea kuruhusu wengi wapotee ‘kizembe’ kama inavyoendelea kutokea.
Ukitaka kujua kama Mangwea alikuwa ni zawadi kutoka kwa Mungu, basi nakupa miezi sita, tafuta mwingine mwenye uwezo kama wake katika kurap hapa nchini, mwenye sauti ya aina yake kama yake, najua shida utakayoipata na jibu lako litakuwa “sijampata.”
Ndiyo maana nasisitiza, lazima tuwalinde waliopo na kama watakuwa wamepotea, basi tuwe wakweli ili kuwasaidia kurudi katika mstari kabla ya kufikia hapa tulipompoteza Mangwea.

No comments:

Post a Comment