KAMUA NDIMU !

Wabunge hawana uhalali wa kuingia Bunge Maalumu la Katiba

Wabunge wetu wamesahau na kuweka pembeni kabisa mamlaka na madaraka yetu umma wa Watanzania kama yalivyoainishwa katika utangulizi wa Katiba ya sasa ya 1977 kuhusu misingi ya Katiba, na katika ibara ya 8 ya Katiba hiyo ya 1977 toleo la 2005.

Kwa ujumla kilichotokea katika kikao cha Bunge la 10 mkutano wa 5 mwaka 2011 na kikao cha Bunge la 10 mkutano wa 12 mwaka 2013 ni viashiria tosha kutuamsha sisi umma wa Watanzania kuchukua nafasi yetu ya mamlaka na madaraka ya kusimamia utungaji wa Katiba mpya ya nchi yetu.Katiba ambayo itaweka misingi mipya ya upatikanaji, uendeshaji na usimamiaji wa utawala wa nchi yetu kwa miaka mingi ijayo. Ni mamlaka na madaraka yaliyoainishwa kikatiba katika utangulizi wa Katiba ya sasa na katika ibara ya 8 ya Katiba hiyo hiyo toleo la 2005 tunavyotakiwa sasa kuvidai na kuvitumia katika kutunga Katiba mpya.Kwa mantiki hii, umma wa Watanzania tunao wajibu sasa wa kusimamia kwa pamoja masilahi ya taifa letu na watu wake wote kwa kutoa kauli za wazi kuhusu nini kifanyike kuokoa mwenendo wa mchakato wa kutungwa kwa  Katiba yetu mpya.Kauli ya kwanza ni kuwa ‘Tanzania ni nchi yetu sote Watanzania na kamwe si ya mamlaka za watawala zilizopo leo wala ya vyama vya siasa vilivyopo leo’.Pamoja na vyombo hivi kuwa na nafasi katika mchakato wa kutungwa kwa Katiba mpya, kama sehemu ya taasisi zetu lakini vyombo hivi havina mamlaka na madaraka wala uhalali wa kisheria, kijamii na kisiasa ‘kupoka’ mamlaka na madaraka yetu ya kujitungia Katiba mpya tunayoitaka.Vyombo hivi vyote ni uzao wa Katiba ya sasa ya 1977 na Katiba hiyo haijavipa mamlaka ya kupoka mamlaka na madaraka ya Watanzania. Mamlaka na madaraka vilivyo nayo vyombo hivyo ni ya kutekeleza wajibu wa majukumu yale kwa mujibu wa Katiba ilivyoviunda na wote waliomo katika vyombo hivyo vya utawala wameapa kuzingatia na kuilinda Katiba ya sasa.  Hivyo basi:Kwa kuwa jukumu na mamlaka na madaraka ya kutunga Katiba mpya ya nchi yetu ni letu sote Watanzania kupitia asasi na taasisi zetu za kisiasa, kijamii, kidini, kitaaluma, kiutawala, kiutamaduni n.k. ambazo ndizo zinatuunganisha kwa malengo mbalimbali yanayotuhusu kama Watanzania.Hivyo basi vyombo vyote vinavyohusika na mchakato wa Katiba mpya vinatakiwa vitokane na ushiriki wetu wa moja kwa moja. Hii ni kwa sababu vyombo hivyo ni vyetu, vinapaswa kuwajibika kwetu na kwa hiyo wajumbe wake wanapaswa kuteuliwa moja kwa moja na sisi kupitia asasi na taasisi, zetu za kiraia na kijamii katika ujumla wake na si kupitia wajumbe wa mamlaka za kiutawala ambazo ni uzao wa Katiba ya sasa ambayo waliapa na wanatakiwa kuilinda mpaka umma utakavyoamua kuwa na Katiba Mpya kuchukua nafasi ya hii iliyopo sasa.Jukumu la mamlaka za utawala na vyama vya siasa vilivyopo ni:-Kutuwezesha kwa kutushirikisha, kuweka mazingira ya kisheria, kiutawala na za utaratibu wa kuunda vyombo vya kusimamia mchakato mzima wa kutunga Katiba mpya.Kutuwezesha kwa kutushirikisha, kuweka mazingira ya kisiasa mshikamano na amani ili tuweze kufikia lengo letu la kuwa na Katiba mpya kwa maridhiano ya amani na mshikamano wa kitaifa.Kutenga rasilimali za kuwezesha vyombo husika na mchakato mzima wa kutunga Katiba mpya kutekeleza wajibu na majukumu yake kwa uhakika na ufanisi mkubwa.Kauli ya pili ni kuwa ‘Bunge Maalumu la Katiba ni chombo chetu maalumu Watanzania’.  Wakati wa mchakato mzima wa utungaji wa Katiba mpya vyombo vya sasa vya kiutawala na kisiasa vinatakiwa kuendelea na wajibu na majukumu yake ya kiutawala na kisiasa kwa mujibu wa Katiba ya sasa.Wajibu wa majukumu ya vyombo hivi katika mchakato wa Katiba mpya ni kuwezesha tu na si kupoka mamlaka na madaraka ya Watanzania kuongoza mchakato huu kupitia vyombo mahususi vilivyoundwa maalumu kwa jukumu hilo tu.Kwa hiyo dhana ya wabunge wote wa Bunge la Muungano na wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuingia katika Bunge maalumu la Katiba katika hatua husika ya mchakato wa Katiba Mpya haina mantiki wala uhalali wa kisiasa, kijamii na wala wa kisheria.Wabunge na wawakilishi hawa hawakuchaguliwa 2010 kwa kazi ya kutunga Katiba Mpya. Kwa kufanya hivyo ni sawa na kusimamisha shughuli zote za kawaida za vyombo hivi ambavyo vimeundwa kuzitekeleza kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar.Kufanya hivyo ni sawa na kuwafanya askari wa wanyamapori na viongozi wao ambao wapo kwa kazi ya kulinda/ kuhifadhi wanyama hao na papo hapo kuwapa leseni za kuwinda wanyama hao kwa masilahi yao binafsi. Uhifadhi na uwindaji ni vitu kinzani kabisa katika nyanja ya hifadhi ya wanyamapori.Askari na maofisa hao wameajiriwa na wanalipwa kulinda na kuhifadhi na si vyote viwili. Vivyo hivyo kuwaruhusu wabunge wote wa Bunge la Muungano pamoja na wawakilishi wa Zanzibar kushiriki katika Bunge maalumu la Katiba mpya kwa nyadhifa tu za ubunge wao walioupata mwaka 2010 ni sawa na kuwataka wavunje kiapo chao cha kuilinda Katiba ya sasa.Pamoja na ukweli kuwa mazoea huweza kuchukuliwa kama kanuni ama desturi lakini utamaduni wa chama kimoja wa kugeuza wabunge wote wa Bunge la kawaida kuunda Bunge Maalumu la Katiba kama ilivyokuwa 1977, hauwezi kukubalika kuwa utamaduni wa jamii ya Watanzania wa leo inayozingatia mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.Hivi ndivyo chama tawala na wabunge wake walivyojionesha kwa umma wa Watanzania katika vikao vya kujadili miswada ya mchakato wa Katiba mpya na mjadala wa rasimu ya Katiba Mpya iliyotolewa na tume.“Sisi tunalitambua Bunge la Jamhuri ya  Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuwa ni kati ya vyombo vyetu kitaasisi katika mfumo wa utawala wa sasa wa nchi yetu”.Lakini hatukubaliani kabisa na vyombo hivi kuingia moja kwa moja katika Bunge Maalumu la Katiba mpya. Tunachokubali ni  mabunge haya mawili yaingizwe katika orodha ya asasi na taasisi zetu na kupewa idadi ya washiriki wake ambao watateuliwa na mabunge yenyewe kwa kuzingatia uwiano wa uwakilishi wa kivyama katika mabunge hayo na uwiano wa sawa kwa sawa katika pande mbili za Muungano, sababu kuu za msimamo huu ni pamoja na; wabunge katika mijadala yao kuhusu mchakato wa Katiba mpya wameshindwa kuonesha uzalendo na utaifa, hivyo kujikita zaidi kiitikadi za kivyama na masilahi binafsi ya kibunge na kuegemea siasa za enzi ya chama kimoja.Bunge Maalumu la Katiba Mpya ni la jukumu maalumu na la muda maalumu. Sheria inatoa muda wa siku 70. Je, kwa wabunge wote kushiriki na hii ikiwa ni pamoja na mawaziri wote na baadhi ya wakuu wa mikoa:Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar vitakuwa likizo kwa kipindi hicho? Uwezo huo wanaupata wapi kisheria? Serikali kwa maana ya Baraza la Mawaziri litakuwa likizo kipindi hicho cha siku 70? Uwezo huo wanaupata wapi kisheria?  Je, rais ataendeshaje serikali bila Baraza la Mawaziri kwa kipindi hicho? Maamuzi ya kisiasa katika kipindi hicho atayatoa kwa ushauri wa chombo kipi?Je, wabunge na mawaziri kuchukua likizo ili kutunga Katiba mpya badala ya kusimamia iliyopo sasa kunaendana na kiapo chao cha utii na kulinda Katiba iliyopo na kutenda kazi zao kwa mujibu wa Katiba hiyo  mpaka umma wa Watanzania kuifuta kwa Katiba mpya?Je, nchi  ina upungufu wa watu wa kuteuliwa kuunda Bunge Maalumu la Katiba mpya bila kuathiri uendeshaji wa utawala wa nchi kwa mujibu wa Katiba iliyopo mpaka itakapofutwa na Katiba mpya? Sisi hatuamini hivyo.Je, kuna sababu ya kutumia fedha za umma kuwabeba wabunge wote wa kawaida katika Bunge Maalumu la Katiba badala ya mabunge hayo kuwakilishwa tu kitaasisi?Kauli ya tatu ni kuwa, pamoja na mapungufu yaliyojitokeza katika kuundwa kwake na utungaji wa kanuni za mabaraza ya wilaya, umma wa Watanzania sasa tunaamini kuwa ‘Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya inaendelea vizuri na kazi yake, kwa hiyo inatakiwa kuendelea na kazi hiyo hadi kupatikana kwa Katiba mpya’ bila kuingiliwa na vyombo vya kiutawala wala kisiasa  hususani Serikali na  Bunge na pia vyama vya siasa.Tume imeonesha usikivu kwa matakwa ya wananchi na kuwa na msimamo thabiti wa kulinda masilahi ya taifa letu. Hivyo kuifuta kabla haijakamilisha kazi yake ni usaliti wa wabunge wetu kwa Watanzania.Hivyo ‘tofauti na uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya’ uteuzi wa ‘Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba mpya’ lazima ufanywe na sisi umma wenyewe wa Watanzania kupitia asasi na taasisi zetu kama ilivyoainishwa katika taratibu za kuongoza mchakato wa Katiba mpya.Orodha hii ifanyiwe mapitio ili kuingiza asasi na taasisi ambazo hazimo katika orodha ya sasa yakiwamo mabunge mawili yaliyopo. Sheria itamke idadi ya wajumbe wa Bunge maalumu la Katiba na kisha idadi hiyo igawanywe kwa asasi na taasisi zitakazoainishwa kushiriki kutoa wawakilishi wa umma katika kuunda Bunge hilo.Aidha, sheria iainishe sifa za mtu kuteuliwa kuwa mjumbe katika Bunge hilo na asasi na taasisi zizingatie sifa hizo katika uteuzi wa washiriki wake. Wateule wote wa asasi na taasisi za kiraia na kijamii kuingia katika Bunge hilo waapishwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ishara maalumu ya uteuzi wao kisheria na mamlaka ya nchi, yaani mamlaka ya urais.Asasi na taasisi zipendekeze majina na kumwachia Rais kuamua nani ateuliwe ni kutupoka mamlaka na madaraka yetu umma wa Watanzania kuteua wawakilishi wetu wa Bunge Maalumu la Katiba, ili kulifanya Bunge hilo kuwajibika kwetu.Kauli ya nne na ya mwisho kwa leo ni kuwa tunavitaka vyombo vyetu vya ‘Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya’ na ‘Bunge Maalumu la Katiba mpya’ kubainisha wazi wazi mamlaka ya umma katika marekebisho yoyote ya Katiba yetu mpya kadiri itakavyolazimu baada ya kuanza kutumika kwake kama ifuatavyo:- Vifungu gani vya Katiba mpya vitaweza kubadilishwa tu kwa njia ya kura ya maamuzi (Referendum) ya umma.Vifungu gani vya Katiba mpya vitaweza kubadilishwa na Bunge kwa kushirikisha maoni ya umma kupitia asasi na taasisi zao za kijamii na kiraia.Vifungu gani vya Katiba mpya vitaweza kubadilishwa na Bunge kwa kuzingatia  mamlaka na madaraka yake ya kikatiba.Hii ndiyo njia ya pekee kuhakikisha kuwa watawala na vyama vyao vya siasa hawachezei Katiba Mpya kwa masilahi yao ya kisiasa.Pamoja na kuwa kauli hii imekuja baada ya vikao vya maridhiano kati ya vyama vya siasa ni vizuri utawala na vyama kutambua kuwa kauli ya umma wa Watanzania ndiyo msingi mkuu wa upatikanaji wa Katiba inayolenga masilahi ya nchi na watu wake.Serikali na wabunge watambue katika mabadiliko yoyote katika sheria ya mchakato wa Katiba, kauli hii inapewa uzito unaostahili na ndiyo maana kauli hii imepitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili kuimarisha mawasiliano ya madai ya umma kwa watawala na vyama vya siasa.

x

No comments:

Post a Comment