Rais Kikwete alisema wajumbe 640 wa Bunge hilo wengi ni wafuasi wa
vyama vya siasa, hivyo wanatakiwa kukubaliana kwa hoja badala ya kila
upande kuvutia kwake.
Aliwaonya pia wanasiasa kutokazania suala la muundo wa Muungano peke
yake, bali waangalie na masuala mengine yaliyomo kwenye rasimu hiyo
ambayo ni muhimu kwa Taifa.
Bunge la Katiba linafanyika baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
kukamilisha kazi yake ya miezi 20 kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa
Rasimu ya pili Katiba ambayo ilitolewa Desemba 30, mwaka jana.
Akizungumza na viongozi mbalimbali wa vyama hivyo jana katika mkutano
wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, Rais Kikwete alisema kama
wanasiasa wakikubaliana, hakuna mwananchi yeyote atakayepinga uamuzi
utakaopitishwa na Bunge hilo.
“Nimeshauriana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein kuwa Bunge
Maalumu la Katiba lianze vikao Februari 18, mwaka huu. Bunge hili
litafanyika kwa siku 70 na kama mambo yatakuwa hayajamalizika zinaweza
kuongezwa siku 20,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza: “Nyinyi ndiyo wenye jukumu la kuipatia nchi yetu katiba
nzuri inayojali masilahi ya watu wake ndani ya pande zote za Muungano,
kuanzia watu wanapoishi, wanapotoka na asili yao. Msije mkafanya uamuzi
utakaowaingiza katika uadui na chuki.”
Katika hotuba yake ya dakika 70, Rais Kikwete alisema yapo mambo
mengi ya kujadili katika Bunge hilo, siyo muundo wa Muungano pekee.
“Mnakwenda kuijadili Katiba kuhusu masuala mbalimbali yenye masilahi
ya nchi yetu, siyo mambo ya Muungano tu. Wekeni utaratibu ili muweze
kukubaliana hata katika masuala ambayo kila mmoja ana msimamo wake,” na
kuongeza:
“Kuna suala la ukomo wa kugombea ubunge kuwa vipindi vitatu. Hii
maana yake ni kuwa kama umeshakuwa mbunge kwa vipindi vitatu huwezi
kugombea hata urais,” alisema na kuongeza;
Kwa mujibu wa Rasimu ya Kwanza ya Katiba, Ibara ya 75 (e) mgombea
urais alitakiwa kuwa na sifa za kugombea ubunge, ikiwamo ya kutowahi
kuwa mbunge kwa vipindi vitatu. Hata hivyo kwenye Rasimu ya Pili
itakayojadiliwa na Bunge hilo, ibara ya 79 inayozungumzia sifa za
kuwania urais, hailazimishi mgombea urais kuwa na sifa za kuwania
ubunge.
Rais Kikwete alisema wanasiasa wana dhamana ya kuwapatia Watanzania
Katiba itakayodumu kwa miaka 50 ijayo na kuimarisha Muungano, umoja,
amani na utulivu, siasa safi na kuongeza kasi ya maendeleo na ustawi wa
wananchi.
“Mnatakiwa kuisoma vizuri Rasimu ya Katiba na kujua yaliyopendekezwa
na wananchi. Chambueni kinachofaa na kisichofaa lakini kwa kuzingatia
masilahi ya Taifa na siyo na vyama vyenu,” alisisitiza Rais Kikwete.
Alisema mafaniko ya mchakato wote wa Katiba yanategemea kauli, mwenendo na matendo mema ya vyama vya siasa.
“Vyama vya siasa vinatakiwa kujenga na siyo kubomoa. Mkiamua Katiba
Mpya ipatikane tutaipata, mkiamua isipatikane hatutaipata. Katiba Mpya
ni kwa masilahi ya watu wote,” alisema na kuongeza;
“Siyo lazima wazo la chama fulani lipitishwe, vyama vinatakiwa
kutambua kuwa wapo wenzao wenye mawazo mazuri kuliko wao. Siyo kila
unachokitaka wewe na wenzako wanataka hicho hicho. Muongozwe na nguvu ya
hoja siyo hoja za nguvu zilizotolewa na mjumbe wa chama chako.”
Alisema kuwa lengo lake siyo kuwazuia wajumbe kutoka vyama vya siasa
kutoa maoni katika Bunge hilo. Lengo ni kuwakumbusha kuwa msimamo wa
chama fulani kuhusu jambo lolote, usigeuzwe kuwa amri ndani ya Bunge
hilo.
“Itakuwa aibu kwa chama kwenda katika Bunge bila kuwa na msimamo wake
lakini pamoja na hali hiyo, mtakuwa tayari kusikiliza mawazo ya
wenzenu?” alihoji Rais Kikwete.
Uteuzi wa wajumbe
Rais Kikwete alisema leo atatangaza majina 201 ya wajumbe wa Bunge hilo kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.
Akizungumzia uteuzi huo alisema, “Majina yaliyowasilishwa na makundi
hayo yalikuwa 3,774. Kazi ya uteuzi imeshakamilika na kilichobaki sasa
ni kuhakiki tu majina, kuangalia uwiano wa wajumbe kimkoa na jinsia.”
Alisema taasisi zisizo za kiserikali zilizoomba zilikuwa 1,647 na
wameteuliwa watu 20, taasisi za dini waliomba 329 na kuteuliwa 20, vyama
vya siasa waliomba 198 na kuteuliwa 42, taasisi za elimu waliomba 130
na kuteuliwa 20, makundi ya walemavu waliomba 140 na kuteuliwa 20.
Wengine ni vyama vya wafanyakazi waliomba 102 na kuteuliwa 19, vyama
vya wafugaji wameomba 47 na kuteuliwa 10, vyama vya wavuvi waliomba 57
kuteuliwa 10, vyama vya wakulima waliomba 157 kuteuliwa 20 na makundi
yenye mrengo unaofanana walioomba 727 na kuteuliwa 20.
Ofisi ya Msajili wa Vyama
Alisema jambo jingine muhimu ambalo Serikali inaendelea kulifanya
kazi ni kuboresha muundo wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini
ili iweze kutekeleza ipasavyo majukumu yake.
“Tutaangalia jinsi ya kuongeza bajeti ya ofisi hii ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake,” alisema.
Sheria ya vyama vya siasa
Akizungumzia sheria ya vyama vya siasa alisema kuwa ina adhabu moja
tu ambayo ni kukifuta chama kinachofanya makosa, kusisitiza kuwa sheria
hiyo haitoi nafasi ya kutosha kulea vyama, hivyo inatakiwa kutazamwa
upya.
“Mchakato wa kupitia sheria hiyo na ile ya gharama za uchaguzi
umeanza. Naamini marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa itasaidia
kuboresha matatizo ya shughuli za kisiasa nchini,”
“Bila kuingilia uhuru wa vyama vya siasa na ile ya uchaguzi kusaidia wananchi kuchagua watu kwa ubora wao na vyama vyao.”
Kutenganisha biashara na siasa
Alisema jambo ambalo mpaka sasa halijaanza kushughulikiwa ni
kutenganisha biashara na siasa, “Jambo hili limeonekana kuwa gumu kweli
kushughulikiwa ndani ya mfumo wa Serikali, sijui limekwama wapi.”
Alisema lazima kuwepo na misingi ya maadili ya uongozi na kwamba
mfanyabiashara anayejitosa katika siasa lazima afuate utaratibu fulani
kama inavyofanyika nchi mbalimbali duniani, ikiwamo Marekani huku
akimtaka msajili wa vyama vya siasa kulishughulikia suala hilo ili
liweze kumalizika.
Wanasiasa wanena
Wakizungumzia hotuba ya Rais Kikwete, Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alisema, “Rais
anatakiwa kudhibiti kauli zinazotolewa na viongozi wa chama chake, ambao
wanapinga masuala mbalimbali yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba ikiwamo
serikali tatu.”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa
alisema, “Hakugusia kabisa wabunge wa Bunge hilo kuzingatia maoni ya
wananchi yaliyomo katika rasimu hiyo.”
Naye Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema, “Nadhani
mmesikia alichokisema Rais. Tutazingatia yote aliyoyasema kwa sababu
Katiba hii ni kwa ajili ya masilahi ya Taifa.”
Wakati huo huo, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Issa
Salum alizua kioja wakati akijitambulisha baada ya kujipambanua kuwa ni
muumini wa Muundo wa serikali mbili, kauli ambayo iliwafanya baadhi ya
wajumbe wa mkutano huo kumwangalia kwa mshangao.
No comments:
Post a Comment