Friday, November 23, 2012

MAUWAJI YA WAPALESTINA YAMUIBUA MUFTI SIMBA, ALAANI VIKALI UDHALIMU WA israel

MUFTI wa Tanzania, Sheikh Issa Bin Shaaban Simba, amelaani matukio ya hivi karibuni yaliyotokea huko Palestina ya kuuwawa wanawake, watoto, wazee na vijana wasio na hatia.
Mufti, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bazara la Waislamu Tanzania (BAKWATA), alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa ameshtushwa na kusikitishwa na fujo zinazoendelea katika kipindi hiki ambapo mamia ya watu wasio na hatia wamepoteza maisha, hali ambayo inatishia usalama wa eneo lote la Palestina na nchi nyingine.
"Nalaani mauaji hayo ya kinyama yanayofanywa na Waisraeli dhidi ya wapalestina.
Hivyo, napenda kutoa wito kwa viongozi wetu wa kitaifa na wale wa kimataifa, likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) kutafuta haraka suluhisho la kudumu la mgogoro huu," alisema," alisema Mufti Simba katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Aliongeza kuwa Bakwata siku zote imekuwa na itaendelea kuwa mstari wa mbele kuunga mkono harakati za Wapalestina, ambao ni waislamu na wakristo katika kupigania haki yao ya msingi ya kuwa na taifa lao la Palestina.
"Nitumie fursa hii kuwapongeza wale wote ambao kwa njia moja ama nyingine wameweza kufanikisha kusimamisha harakati za umwagaji wa damu katika eneo hilo. Kipekee napongeza juhudi za Serikali ya Misri, kupitia kwa Rais wao na Waziri Mkuu kwa jitihada kubwa walizofanya kuhakikisha hali ya utulivu inarejea," alisema.
Sambamba na hilo, aliwaomba waislamu nchini kuwa watulivu na kutumia kipindi hiki kuwaombea dua wale wote waliopoteza maisha yao katika matukio hayo

No comments:

Post a Comment