Friday, March 15, 2013
POLISI:makanisa na mapdri sasa watapewa ulinzi mzito
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limeanza kutoa ulinzi kwa viongozi wa dini ya Kikristo na kwenye nyumba za ibada baada ya kuwapo vitisho dhidi ya viongozi hao. Hatua ya polisi imekuja siku chache baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentine Mokiwa.
Dk. Mokiwa alivamiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake, Mbezi Mashirikiano, usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita, ambapo watu hao walimjeruhi kwa mapanga mlinzi wake aliyefahamika kwa jina moja la Fred.
Watu hao walimjeruhi mlinzi huyo baada ya kukaidi amri yao wakitaka awaeleze alipo Askofu Mokiwa na mkewe. Habari tulizozipata ni kwamba bado hali ya kiafya ya mlinzi huyo ni mbaya.
Hatua ya polisi kuanza kutoa ulinzi kwa viongozi hao wa dini inakuja baada ya kuwapo malalamiko mengi dhidi ya jeshi hilo kupuuzia taarifa wanazopelekewa juu ya kuwapo vitisho kwa viongozi wa Kikristo.
Akizungumza , Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, DCP Suleiman Kova, alisema Jeshi la Polisi limeamua kutoa ulinzi kwa viongozi wote wa dini ya Kikristo waliotishiwa maisha yao na hata ambao hawajapata ujumbe wa vitisho.
Kamanda Kova pia alisema polisi kwa sasa imeanza kuweka ulinzi kwenye makanisa kwa lengo la kudhibiti vitisho vya kuyachoma moto.
“Ni kweli tumemwekea ulinzi Askofu Mokiwa pamoja na viongozi wote waliotishiwa maisha na hata wale ambao hawakutishiwa.
“Lakini pia hata kwenye makanisa nako tumeweka ulinzi kwani siku za karibuni kumekuwapo ujumbe wa kuyachoma moto,” alisema Kamanda Kova.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment