Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema watu hao walikamatwa katika msako maalum unaoendeshwa na jeshi hilo katika hali ya kukabiliana na hatua zozote zenye lengo la kuleta chuki na ubaguzi wa kidini nchini.
“Mtuhumiwa wa kwanza ambaye ni Kombo Hassan, tulimkamata akiwa na nyaraka nyingi za aina mbalimbali alizokuwa akisambaza na wenzake jijini Dar es Salaam pamoja na mikoani kwa makusudi ya kuleta mfarakano wa kidini nchini.
“Baadhi ya nyaraka hizo ni pamoja na nyaraka zinazochochea chuki na vurugu dhidi ya Serikali na taasisi nyingine, kundi hili pamoja na watu wengine ambao bado wanatafutwa limebaini kuwa na mtandao wa
mawakala sehemu mbalimbali nchini,” alisema.
Kamanda Kova alisema jeshi la Polisi litaendelea na msako mkali nchi nzima, ili kuwabaini wote wanaojihusisha na uchochezi kwa lengo la kuleta vurugu na uvunjifu wa amani.
Alisema upelelezi wa shauri hilo unaendelea sanjari na jalada la kesi kupelekwa kwa Wakili wa Serikali, ambaye atathibitisha kiwango cha tuhuma hizo na watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa makosa yatakayobainika.
Kamanda Kova alisema, Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaoleta uchochezi kupitia shughuli za kidini au kisiasa pia amewataka wananchi wote wapenda amani bila kujali dini au itikadi yoyote kuungana kwa pamoja, ili kuhakikisha kwamba watu wachache wenye nia mbaya wasifanikiwe kuharibu amani ya nchi yetu ambayo imezoeleka.
Katika hatua nyingine, alisema jeshi la Polisi linashirikiana na benki mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Benki Kuu ili kudhibiti mianya ya wizi katika mashine maalum za kuchukulia fedha (ATM).
Alisema hivi karibuni kuna wahalifu kutoka ndani na nje ya nchi ambao wametengeneza mtandao wa wizi katika ATM.
“Baadhi ya watu hao tumeshawakamata na kuwafikisha mahakamani na mashauri yao yanaendelea,” alisema Kamanda Kova.
No comments:
Post a Comment