Akizungumza nasi, mmoja wa watu wa karibu na askofu Mokiwa alisema watu hao walifika kwa lengo la kutaka kuingia ndani ili waweze kumuona, hali iliyomfanya mlinzi kuwazuia.
“Wale watu walipofika kwa mlinzi walimuuliza kuwa askofu yupo.. mlinzi akawajibu kuwa hayupo,
wakamuuliza tena mama je (mke wa askofu), akawajibu kuwa wote hawapo, baada ya kujibiwa hivyo walianza kumpiga mlinzi kwa madai kuwa hataki kuonyesha ushirikiano, walimpiga na kumjeruhi vibaya kwa mapanga na hadi sasa amelazwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha,”,kilisema chanzo hicho.
Alisema mlinzi huyo aliyetambulika kwa jina la Fred, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 45, alipigwa hadi kuzimia kabla ya watu hao kutokomea kusikojulikana.
Habari zilizothibitishwa na mtu mmoja wa karibu na Askofu huyo zinaeleza kuwa, mlinzi huyo aligoma kuwaambia ukweli watu hao kwa sababu alikwishaonywa kuwa makini na wageni wa aina yoyote wanaofika nyumbani hapo kumuulizia Mokiwa.
Mtoa habari wetu huyo alitumbia kuwa wakati mlinzi huyo akivamiwa na kucharangwa mapanga, Askofu Mokiwa pamoja na mke wake walikuwemo ndani ya nyumba lakini hawakuweza kusikia lolote, kutokana na lango la kuingia nyumbani kwake kuwa mbali na nyumba.
“Askofu alishamtahadharisha mlinzi kwa sababu wiki mbili zilizopita alishatoa taarifa polisi kuhusiana na vitisho alivyokuwa akipewa na watu wasiojulikana, kikubwa kilichosaidia ni kwamba nyumba ya askofu iko umbali kidogo, lakini wangemdhuru,” alisema mtoa taarifa wetu huyo.
Katibu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Dickson Chilongani, alisema wamepokea taarifa hizo kwa masikikito na kwamba wanasubiri taarifa rasmi kutoka kwa askofu ili wazifanyie kazi.
“Tayari tumepata taarifa, lakini nimejaribu kumtafuta askofu Mokiwa nimeambiwa kwamba anahojiwa na vyombo vya usalama, tunasubiri amalize tuzungumze naye ili tulifuatilie kwa ukaribu suala hili, kwani ni tukio la kushtusha,” alisema Chilongani.
kaa chojo ilimtafuta Askofu Mokiwa kwa njia ya simu ambapo alithibitisha juu ya habari za kuvamiwa nyumbani kwake na akamtaka mwandishi amtafute baada ya dakika 40.
Mwandishi alimtafuta tena Mokiwa baada ya dakika 40 kupita simu yake, iliita bila mafanikio na alipotumiwa ujumbe mfupi wa kumkumbusha alilituambia kwa njia ya simu kuwa ana ugeni wa serikali na kulitaka tumpigie baada ya dakika 45.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyella, alisema amesikia taarifa hizo, lakini hajazipokea rasmi ofisini kwake.
“Ni kweli hata mimi nimesikia, lakini hazifafika ofisini kwangu rasmi, nitafute baadaye naweza kuwa na taarifa sahihi, kwa sababu wao wako Mbezi, inawezekana hizo taarifa zipo huko Mbezi katika kituo cha polisi cha Mbezi kwa Yusuph,” alisema Kamanda Kenyella
No comments:
Post a Comment