DKT. JAKAYA KIKWETE. |
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu ninalopenda kuzungumza nanyi leo ni uhusiano wa Waislamu na Wakristo nchini. Jambo hili nimeshalizungumzia mara kadhaa siku za nyuma, lakini nalazimika kulisemea tena kutokana na hali ilivyo sasa. Tumefikia mahali ambapo kama viongozi na waumini wa dini hizi kubwa mbili hawatakubali kubadili muelekeo wa sasa, tunakoelekea ni kubaya. Nchi yetu nzuri tutaivuruga na sifa yake ya miaka mingi ya Waislamu na Wakristo kuishi pamoja kidugu, kwa upendo, ushirikiano na kuvumiliana itatoweka. Tanzania itaacha kuwa kisiwa cha amani na kuingia katika orodha ya nchi zenye migogoro na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Ndugu Wananchi;
Nyaraka na kauli kali kali zinazotolewa na viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu zinanishawishi kuamini haya niyasemayo. Nyaraka na kauli hizo zina mambo mawili makuu. Kwanza, kwamba kila upande unatuhumu, kushutumu na kulaumu upande mwingine kwa kufanya vitendo viovu dhidi ya dini yake. Kauli na mihadhara ya kudhalilisha dini za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu, kuchoma moto nyumba za ibada, mzozo kuhusu nani achinje na kuuawa kwa viongozi wa dini ni baadhi ya mambo yanayotolewa mifano.
Na, pili kwamba kila upande unailamu Serikali kwa kupendelea upande mwingine. Wakristo wanalaumu kwamba mihadhara ya kudhalilisha Ukristo inaendeshwa na Serikali haichukui hatua. Aidha, Wakristo wanateswa na viongozi wao kuuawa na Waislamu, lakini Serikali haichukui hatua. Kwa ajili hiyo wanadai kuwa Serikali imeshindwa kulinda uhai wa raia wake. Wanasema pia kwamba Serikali inapendelea upande wa Waislamu.
Ndugu Wananchi;
Waislamu nao wanadai kuwa kitabu chao kitakatifu, yaani Quran Tukufu, kinadhalilishwa kwa kuchanwa, kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na Serikali haichukui hatua yo yote ya maana. Waislamu wananyanyaswa katika nchi yao, wanakamatwa ovyo, hawapewi fursa sawa na kwamba Serikali inawapendelea Wakristo. Wanasema nchi inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo. Mimi binafsi wananishutumu kuwa napendelea kushiriki zaidi kwenye shughuli za Wakristo kuliko za Waislamu kama vile harambee za kujenga Makanisa na shule za Makanisa. Naambiwa kuwa mwepesi kushiriki maziko ya Maaskofu kuliko Masheikh wanapofariki. Ipo Misikiti mitatu hapa Dar es Salaam wamenisomea itikafu nife. Katika itikafu hiyo wamewajumuisha Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ndugu Suleiman Kova.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza, hatupendelei upande wo wote. Hatufurahishwi na kitendo cha mtu kudhalilisha dini ya mwenzake ndiyo maana wapo wahadhiri wa dini ya Kiislamu na wahubiri wa dini ya Kikristo wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa nyakati mbalimbali. Vyombo vya usalama vinatambua wajibu wake huo na kama haifanyiki ni ulegevu wa mtu tu katika kutimiza wajibu wao na siyo kwamba ni sera na maelekezo yangu au ya Serikali. Mtakumbuka kuwa mara kadhaa nimewakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya na wakuu wa vyombo vya usalama kuacha ajizi katika kutimiza wajibu wao kwenye suala hili.
Ndugu Wananchi;
Mimi binafsi sibagui, hushiriki shughuli za Waislamu na Wakristo kila ninapoalikwa labda nikose nafasi kwa sababu nyinginezo. Nimeshafanya shughuli nyingi za Waislamu kama vile Maulid ya Mtume Muhamad S.A.W., safari za Hija, ujenzi wa misikiti na madrasa na mengineyo mengi. Nimeshashiriki mazishi ya Masheikh kama nifanyavyo kwa Maaskofu na watu mbalimbali Waislamu na Wakristo. Pale ambapo sikushiriki mazishi ya Sheikh au Askofu itakuwa ni kwa sababu ya kubanwa na shughuli nyingine ambazo lazima nifanye mimi, au taarifa ilikuwa ya muda mfupi. Kwa upande wa Waislamu desturi yetu ya kuzika mara mtu anapofariki huwa kikwazo kwangu kushiriki hasa ikiwa ni nje ya Dar es Salaam kwa sababu ya taratibu za kumsafirisha Rais kutoka mahali pamoja kwenda pengine siyo nyepesi. Wakristo hawana utaratibu huo, huwa wanaweza kusubiri hivyo huniwia rahisi kushiriki.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali yetu haijashindwa kulinda usalama wa raia wake au viongozi wa dini na nyumba za ibada. Kama ingekuwa hivyo, tungeshuhudia mauaji ya raia, viongozi wa dini na matukio ya kuchomwa nyumba za ibada yakiwa mengi hapa nchini. Lakini hivyo sivyo. Nawasihi sana ndugu zangu Wakristo na Waislamu kuwa tusiyachakulie matukio ya kuuawa kwa Mchungaji Mathayo Kachila kule Buseresere, Geita, na Padri Evaristus Mushi kule Zanzibar, au kumwagiwa tindikali Sheikh Fadhili Soroga, Naibu Mufti wa Zanizbar, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda na kuchomwa moto kwa Makanisa Zanzibar na Mbagala, Dar es Salaam kuwa ni kielelezo na ushahidi wa Serikali kushindwa kutimiza wajibu wake.
Kila tukio lina mazingira yake, hakuna ushahidi wa vyombo vya Serikali kuzembea. Hakuna ushahidi wa matukio hayo kuunganika. Mpaka sasa hatujapata ushahidi wa kuwepo kikundi cha Waislamu wanaopanga kuua viongozi wa Kikristo na kuchoma moto Makanisa hapa nchini.
Ndugu Wananchi;
Kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila wa Buseresere ni matokeo ya vurugu zilizosababishwa na mzozo kati ya Wakristo na Waislamu kuhusu kama nyama iliyochinjwa na Wakristo Kanisani nayo iuzwe kwenye bucha iliyopo pale kijijini ambayo kwa mazoea huuzwa nyama iliyochinjwa na Waislamu. Katika ugomvi na vurumai hizo ndipo watu kadhaa wa pande zote walijeruhiwa na Mchungaji kupoteza maisha. Si tukio unaloweza kulihusisha na mengineyo nchini. Ni la pale pale Buseresere na limeanzishwa na kuhusisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere kwa sababu zao.
Hivi kama kusingekuwepo na mzozo wa nyama ile kuuzwa katika bucha ile kuumizana kule na mauaji yale yangetokea? Kabla ya mzozo ule Wakristo na Waislamu wa Buseresere hawakuwa na ugomvi baina yao. Walikuwa wanaishi kidugu na kushirikiana katika shughuli zao za kujitafutia riziki huku kila mmoja akimuabudu Mungu kwa misingi ya dini yake. Hivyo kutumia tukio hilo kutoa wito kwa Wakristo wote kuwa kuuawa kwa Mchungaji Kachila ni sawa na kuuawa kwa Wakristo wote nchini kulikofanywa na Waislamu ni kulikuza tatizo isivyostahili. Busara ituongoze kutafuta njia ya kuwapatanisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere wazungumze, waelewane na waendelee kuishi pamoja kama ilivyokuwa awali. Hata mzozo wa kuchinja wanaweza kuumaliza. Mbona bucha za kitimoto zipo na watu hawajapigana. Kutumia mzozo wa Buseresere kueneza chuki kati ya Wakristo na Waislamu nchi nzima si sawa. Hatuwatendei haki Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Kuuawa kwa Padri Evaristus Mushi wa Zanzibar ni tukio linalojitegemea halina uhusiano kabisa na lile la Buseresere, Geita. Hapakuwa na mzozo kuhusu nani achinje. Bado uchunguzi wake unaendelea na tumehusisha vyombo vya upelelezi vya nje vishirikiane na vyetu kufanya uchunguzi. Tumefanya hivyo kwa sababu ya ugumu uliopatikana katika uchunguzi wa matukio ya kabla yake. Yaani ile la kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa Padri Ambrose Mkenda na kumwagiwa tindikali kwa Naibu Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhili Soroga. Bado hakuna mafanikio ya kutia moyo. Na bado tunajiuliza kama matukio hayo matatu yanahusiana. Je, Makanisa kuchomwa moto kule Zanzibar nako kuna uhusiano wowote na matukio yale matatu? Uchunguzi unaoendelea unaweza kufumbua fumbo hilo.
Kuna watu wanadhani yanahusiana na kwa sababu nzuri. Lakini inabaki kuwa ni dhana ya kibinadamu mpaka ukweli halisi utakapobainika. Bado kazi ya uchunguzi inaendelea kufanywa na vyombo vya usalama vya nchi yetu wakishirikiana na wenzao wa nje. Katika mazingira hayo, ni mapema mno kumnyooshea kidole mtu ye yote na kuilaumu Serikali ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Serikali siyo mshirika katika mauaji hayo, na haina sababu ya kufanya hivyo. Ndiyo maana tunahangaika usiku na mchana kupata jawabu.
Ndugu Wananchi;
Hali kadhalika tukio la Makanisa ya Mbagala, Dar Es Salaam kuvamiwa, kubomolewa, mali kuibiwa na kuchomwa moto tarehe 12 Oktoba, 2012 nalo lina mazingira yake maalum. Chanzo chake ni mzozo uliotokana na tukio la kusikitisha la kijana mmoja Mkristo kukojolea Kitabu Kitakatifu cha Waislamu, yaani Quran Tukufu. Pamoja na maelezo kuwa walikuwa na ubishi wa kitoto na kijana mwenzake, lakini kitendo hicho kiliwakasirisha Waislamu. Kijana huyo alifikishwa kituo cha Polisi. Baadhi ya Waislamu wenye msimamo mkali walifika kituoni hapo wakidai wapewe huyo kijana wamuadhibu wao. Jeshi la Polisi lilikataa. Kukatokea mzozo kati ya waumini hao na Polisi na baada ya kushindwa walichokitaka baadhi yao walipotoka pale, wakaenda kufanya uhalifu wa kuvunja, kuiba na kuchoma moto Makanisa.
Ndugu Wananchi;
Baada ya tukio la Mbagala hapajakuwepo na tukio la kuchomwa Kanisa mahali popote kwa upande wa Bara. Aidha, hapajawahi kuwepo tishio lililothibitika la watu kutaka kuchoma Kanisa popote. Lakini maneno ya vitisho vya kuchoma Makanisa yako mengi hasa kupitia mitandao ya simu za mkononi. Kila ujumbe wa namna hiyo ulipofikishwa kwenye vyombo vya usalama uchunguzi umefanywa na hata hatua za tahadhari kuchukuliwa lakini hakuna hata taarifa moja iliyothibitika kuwa na chembe ya ukweli. Hata dalili hazijakuwepo.
Tulichojifunza ni kuwa ujumbe na vitisho vya aina mbalimbali hupelekwa kote, kwa Wakristo na Waislamu. Upo unaowalenga Wakristo ukiwaambia wenzao Waislamu wanapanga kuwadhuru. Na upo wanaopelekewa Waislamu wakiambiwa Wakristo wanao mipango mibaya dhidi yao. Watanzania wenzangu nawaomba mtanabahi na mjue kuwa wapo watu wanacheza mchezo mchafu wa kuwagonganisha na kutaka kuwagombanisha Wakristo na Waislamu kwa sababu wanazozijua wao na kwa faida yao. Wanapandikiza chuki kwa lengo la kutaka Wakristo na Waislamu wagombane. Wanapandikiza chuki baina ya Serikali na waumini wa dini zetu kuu mbili ili ionekane Serikali imewatelekeza raia wake. Ni mchezo mbaya, tusikubali kucheza ngoma tusiyoijua. Hivi ndugu zangu mmekaa chini na kujiuliza kumetokea nini kipya hata leo kuwa na mhemko kama huu kati ya Wakristo na Waislamu na kutishia kuleta vita baina nchini kote?
Ndugu Wananchi;
Serikali haijapuuzia kila palipotokea matukio ya uhalifu. Watu 76 wanaotuhumiwa kuharibu na kuchoma moto Makanisa kule Mbagala na kufanya fujo kituo cha Polisi wamekamatwa na kesi zao zinaendelea Mahakamani. Kwa upande wa tukio la Buseresere lililosababisha kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila, watu 17, wakiwemo waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu walikamatwa na kesi zao zinaendelea. Wapo walioshitakiwa kwa mauaji na wapo walioshitakiwa kwa kufanya vurugu. Jeshi la Polisi bado linawatafuta watu wengine waliohusika na uhalifu huo ili na wao wakamatwe. Kwa upande wa Zanzibar, watu 10 wanaotuhumiwa kuchoma Makanisa wamekamatwa na kesi zao zinaendelea. Bado hajakamatwa mtu kwa tukio la mwisho la kuchoma Kanisa baada ya kuuawa Padri Evaristus Mushi. Uchunguzi unaendelea.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kujeruhiwa kwa Padre Mkenda, bado uchunguzi haujakamilika pamoja na kuwapo taarifa kadhaa zinazoendelea kufanyiwa kazi. Kuhusu uchunguzi wa mauaji ya Padre Mushi, baada ya jitihada kubwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kushirikisha nchi zilizobobea katika uchunguzi wa makosa ya aina hii, hatua ya kutia moyo imefikiwa. Mtu mmoja amekamatwa na wengine wanaendelea kutafutwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kanda na vituo vya redio nako pia Serikali imechukua hatua. Watu kadhaa wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kurekodi na kusambaza kanda zinazochochea chuki na vurugu za kidini. Wapo Waislamu na Wakristo. Wapo watu wengine ambao wanaendelea kutafutwa. Zipo taarifa kuwa baadhi yao wamekimbilia nchi za nje. Jeshi la Polisi limeomba msaada wa Polisi wa Kimataifa, yaani Interpol, kusaidia kuwatafuta na kuwarejesha nchini. Vituo viwili vya radio yaani Kwa Neema FM cha Sengereme na Radio Imani cha Morogoro vimefungiwa kwa muda wa miezi sita. Baada ya muda huo kupita, Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano itaamua ipasavyo.
Ndugu Wananchi;
Nimeyaeleza haya kwa kirefu kuwahakikishia kuwa Serikali inajali usalama wa raia wake wa mali zao na amani na utulivu wa nchi yetu. Kamwe hatujashindwa kulinda raia wa nchi wa yetu na yapo mambo mengi yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika kuhakikisha kuwa Watanzania wa dini zote, makabila yote, rangi zote na mahali po pote walipo wako salama. Tunataka kuona watu wanaendelea kuishi kwa amani, upendo, ushirikiano na mshikamano kama tulivyokuwa tunaishi siku zote. Tunapenda kuona Watanzania wanaepuka mambo yanayowabagua na kusisitiza yale yanayowaunganisha. Tujiepushe kuyapa kipaumbele yale yanayotugawa.
Ndugu Wananchi;
Athari za mzozo kuhusu kuchinja kule Geita iwe fundisho kwetu sote. Tuazimie sote kuwa yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Hebu tufikirie maisha yetu Watanzania yatakuwaje kwenye shughuli za kijamii kama vile sherehe, harusi, ngoma na misiba iwapo tutaanza kuwa na chakula tofauti kwa Waislamu na Wakristo. Fikiria itakuwaje kwenye hospitali, shule na vyuo pawe na majiko mawili au labda hata mabwalo mawili ya chakula kwa Waislamu na Wakristo. Jeshini nako kuwe na majiko na mabwalo ya Waislamu na Wakristo. Hali iwe hivyo hivyo kwenye migahawa na maeneo mengine yenye huduma ya chakula.
Ndugu zangu, tunataka kuipeleka wapi nchi yetu? Tunataka kujenga nchi ya namna gani? Mimi naamini tukifanya hivyo huo utakuwa ndiyo mwanzo wa kubaguana kwa kila kitu na kila jambo na kuligawa taifa kwa namna ambayo hatutakuwa wamoja tena. Huko tunakoelekea siko, ni kubaya. Tubadilike, na wakati ni huu. Viongozi wa dini waongoze njia wawaepushe waumini wao na taifa letu na janga hili.
Ndugu Wananchi;
Bado narudia kusisitiza umuhimu wa viongozi wa dini zetu kubwa mbili kukutana na kuizungumzia hali hii na kuipatia ufumbuzi. Ni wao kuliko mtu mwingine ye yote wenye majawabu ya matatizo haya. Ni masuala yanayohusu imani za dini na yanafanywa na viongozi wa dini na wafuasi wao kwa jina la dini zao. Serikali ina wajibu wa kulinda amani. Kazi yetu itakuwa rahisi kama waumini hawatafanya vitendo vitakavyosababisha uvunjifu wa amani. Wa kuongoza waumini lipi jema na lipi baya ni viongozi wa dini.
Ndugu Wananchi;
Nimeshakutana na viongozi kadhaa wa madhehebu na taasisi za dini za Kikristo na Kiislamu kuzungumza nao kuhusu jambo hilo. Nimepata faraja kuona kuwa wote wanasikitishwa na mambo yanayotokea hivi sasa na wameona busara ya viongozi wa dini kuzungumza ili kuondoa tofauti zilizojitokeza. Wanakiri kuwa hali ilivyo sasa siyo ya kawaida kwa Tanzania na Watanzania. Kuna upepo mbaya wa shetani unapita ambao viongozi wa dini wana wajibu wa kuhakikisha kuwa hali ya hewa inasafishwa na kurejesha nchi yetu na watu wake katika maisha tuliyoyazoea. Maisha ambayo waumini wa dini tofauti wanaishi pamoja kwa udugu, upendo, ushirikiano na mshikamano kwa misingi ya ubinadamu wao na Utanzania wao.
Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, ameshaeleza dhamira ya Serikali ya kuitisha mkutano wa viongozi wa dini mapema mwezi ujao. Ni matumaini yangu kuwa wote watashiriki wenyewe bila ya kutuma wawakilishi. Lazima tupate jawabu kwa maslahi ya taifa letu na watu wake.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda kutumia nafasi hii kuwaomba na kuwasihi waandishi wa habari wasaidie kuliepusha taifa letu kuingia katika vita vya kidini. Waache kushabikia taarifa zinazochochea na kujenga uhasama baina ya waumini wa dini zetu. Nawaomba wapime athari za taarifa zao kabla ya kuziandika au kuzitangaza. Wawe makini na maneno wanayotumia. Katika hali tuliyonayo sasa lazima sote tuazimie kuondoa tofauti za kidini na kujenga umoja miongoni mwa Watanzania wa dini zote. Wasipofanya hivyo, wataliingiza taifa katika mgogoro mkubwa ambao hauna msingi kama ilivyotokea katika nchi jirani. Nawaomba wamiliki wa vyombo vya habari kutambua kuwa wanao wajibu wa kuhakikisha vyombo vyao havitumiki kuleta mifarakano kwa kuchochea uhasama baina ya Wakristo na Waislamu.
No comments:
Post a Comment