Monday, April 15, 2013

ndugu spika, naomba nianze kuropoka hovyohovyo ?


NDUGU Spika, awali ya yote ninaomba nikushukuru wewe mwenyewe kwa jinsi unavyoliongoza Bunge
kwa staili ambayo sijawahi kuiona, kuisoma wala kuisikia tangu nizaliwe; staili ya kuwaruhusu wabunge kusema hovyo hovyo bungeni na wakati mwingine kutukana.

Huu ni uhuru mkubwa sana kwa wabunge katika kutoa mawazo yao, hasa wakati huu wanapoelekea ukingoni mwa kipindi chao cha maulaji. Ni uhuru ambao umepita mipaka ya kujadiliana kwa lugha ya kistaarabu, ni uhuru unaofanana na ule wa kijiweni au katika vikao vya moja baridi moja moto. Nakupongeza sana ndugu Spika.



Ndugu Spika, naomba utambue kuwa kadIri siku zinavyozidi kusonga mbele, ndivyo mwenendo wa mambo bungeni unavyozidi kuwa wa hovyo hovyo kuliko wakati wowote katika historia ya Bunge letu tangu lilipoanzishwa.

Hivi ndivyo ninavyoona, kwa sababu katika siku zangu za kuishi hapa duniani, sikuwahi kuwasikia walionitangulia wakisimulia kuwapo kwa vituko kama vinavyojitokeza sasa bungeni.

Bunge la sasa limekuwa la kihistoria kwa kupita katika vipindi vya maudhi na vichekesho katika muda wa miaka mitatu na kidogo tu ya uhai wake. Kutoka Bunge la wanasiasa waroho, wanaotaka kulipwa vizuri kuliko hata wabunge waliopo duniani, mapema tu mwaka 2006.

Baadaye, hapo katikati likageuka kuwa Bunge la vicheko na vilio, hadi hivi sasa linapoelekea ukingoni ambapo limegeuka kuwa la kukashifiana na kutoleana matusi ya hovyo hovyo.

Ndugu Spika, hili ni jambo la kujivunia kwa sababu ninaamini kuwa kwa mara ya kwanza, Bunge letu linaweza kuingia katika kitabu cha kumbukumbu muhimu kwa kuwa la kwanza duniani kuwa na vituko vya aina hii; la wabunge mabingwa wa kusema hovyo dhidi ya mawaziri wao kwa sababu hawafanyi watakavyo. Hongera sana Spika kwa kusaidia kuandikwa upya kwa historia ya Bunge letu.

Kilichobaki sasa ni kumuomba Mungu aharakishe kutokea kwa ngumi bungeni. Yaani wabunge na mawaziri wapigane, halafu Spika awe mwamuzi. Hii ndiyo hatua iliyobaki kwa sababu kama tuna wabunge wanaoweza kuwaombea mawaziri wao laana na wengine kuwaita au kuwafananisha na mbwa ama nyoka wa mdimu, nadhani wanaweza hata kuwapiga. Na iwe hivyo mapema ili Bunge livunjike kama ambavyo nimekuwa nikiota siku nyingi kwa manufaa ya Watanzania.

Kabla sijajielekeza kwa kina katika mjadala wa leo, nitangulie kukuomba radhi ndugu Spika kwa kuchelewa kuwasili bungeni. Hii ni kwa sababu nilikuwa na matatizo mengi ya kifamilia, lakini kikubwa zaidi nilikuwa naogopa kushiriki kupitisha bajeti ya hovyo hovyo ambayo ilikuwa ikitaka kuwakamua hata wachunga kondoo wa Mungu kwa kosa lao la kuwadanganya wanakondoo wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Ndiyo maana nikaamua kubaki Dar es Salaam, kwa muda mpaka ilipopitishwa.

Ndugu Spika, naomba kuungana na ndugu Lucas Selelii, kuwatukana wajumbe wote walioshabikia kupitishwa kwa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2009/2010 huku wakijua kuwa kamwe haiendani na kaulimbiu ya “Kilimo Kwanza”. Namuomba Mwenyezi Mungu ailaani midomo yao ipinde kuelekea kushoto ili ishindwe kusema uongo wa wazi na wa kitoto kwa wapiga kura wao mwakani wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Ndugu Spika, ninamuomba Mungu, kwa hasira ya ajabu, awalaani wabunge wote waliokuwa na kiherehere cha kueleza kuwa wataipinga bajeti ya mwaka huu wa fedha kwa sababu ina upungufu kadha wa kadha, lakini baada ya kutishwa kitoto kabisa na wewe rafiki yangu, ndugu Spika, kuwa iwapo wataigomea bajeti hiyo basi Bunge linaweza kuvunjwa na wao wakakosa ulaji, wakaufyata.

Hawa ni wabunge wa hovyo ambao ninaamini kuwa wanajali sana matumbo yao kiasi kwamba ulipowatishia tu kuwa rais anaweza kulivunja Bunge iwapo wataendelea na msimamo wa kutetea marekebisho ya bajeti ili iwe na manufaa kwa Watanzania, wakanywea.

Naomba nikupongeze sana katika hili kwa sababu jamaa hawa hawajui kuwa wewe ni kiongozi mahiri unayejua kupima hali ya upepo kama unaweza kuvuma kwa kasi kuelekea upande wako na kuleta madhara au la. Una akili sana rafiki yangu Spika.

Ndugu Spika, ingawa si ustaarabu kutumia lugha za kuudhi kwa wengine, naomba nitumie maneno kama yale ya ndugu Mudhihir Mudhihir, kumwita nyoka wa mdimu na mtu mwenye roho mbaya yule jamaa aliyeomba mwongozo wa Spika baada ya Zitto kutoa maneno makali kwa mmoja wa watu wakubwa sana katika ofisi inayotunza fedha zetu hapa nchini.

Huyu anakitakia mabaya chama chetu kwa sababu anataka iwapo utathubutu kuchukua uamuzi wa kumsimamisha Zitto kama ilivyokuwa awali, basi uzito wake utakua mkubwa kwa Watanzania na kukugeukia wewe kuwa unatumia bunge kuwapatia umaarufu wapinzani.

Kwa sababu wewe ni rafiki yangu, nakushauri tumia busara sana katika hili ikibidi hata kupindisha kanuni ili usifanye kosa kama ulilofanya mwanzo kwa Zitto. Inatosha sana katika maamuzi yako kuwataka wabunge kumuombea Zitto na kumpa ushauri nasaha ili asiendelee kuwatukana mawaziri kuwa kauli zao ni za hovyo hovyo na kubishana na kiti chako.

Kama unabisha, jaribu kumsimamisha uone Watanzania watakavyokutolea macho. Nina hakika ukijaribu kwa namna yoyote kwenda kinyume na ushauri ninaokupa, utakisababishia chama chako kushindwa katika uchaguzi mdogo unaokuja na utachafua sana jina lako. Nadhani umesikia.

Ndugu Spika, naomba kuungana na ndugu Juma Kilimbah kukutaka usitumie kiti chako kuwadhalilisha wenzako. Fahamu kwamba ulichokifanya kwa ndugu John Cheyo, kumtimua bungeni hata kama alikiuka kidogo kanuni za Bunge kwa kubishana na kiti chako, si uungwana. Kumbuka ndugu Spika, uungwana ni vitendo.

Ukiwa mtu makini, mwenye mbwembwe za kila aina, spidi na viwango vya hali ya juu katika utendaji wa shughuli zako bungeni, hukupaswa kukasirika kiasi cha kumtimua mzee wa watu huku ukimwita dikteta, ukiushangaa usomi wake kwa kuhoji kile anachokiamini katika somo la kemia na kutumia lugha ya kimombo kumtaka akae chini.

Ndugu Spika, najua kuwa ulikuwa unasimamia kanuni, lakini kama wapo waliowaita wenzao mbwa, nyoka wa mdimu, wengine wakamuomba Mungu awalaani kwa sababu ya kulilia kupelekwa maendeleo katika majimbo yao ili wasikose ulaji, wewe ukawa mpole kwa kile ulichoeleza kuwa walikuwa wakitoa hisia za ndani ya mioyo yao, vipi kwa ndugu Cheyo ambaye alikuwa akitoa hisia za ndani ya moyo wake kuhusu uhai wa watu?

Ndugu Spika, wewe ni rafiki yangu na sipendi jambo lolote baya likutokee pasipo mimi kukutahadharisha. Namuomba Mungu akulaani kwa hiki ulichomfanyia ndugu Cheyo wakati akijaribu kuelezea hisia zake kuhusu madhara makubwa ya kemikali zinazotoka migodini kwa watu wetu.

Ndugu Spika, baada ya kukuombea laana hiyo, sasa ninaomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment