Wednesday, August 14, 2013

‘Kukashifu dini’ liondolewe kwenye rasimu ya katiba

Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni wamependekeza neno “kukashifu imani na dini nyingine” liondolewe kwenye Rasimu ya Katiba kwa madai kwamba limelenga
kuziua imani za dini za Kiislamu na Kikristo.

Wamesema sambamba na kuondolewa neno hilo, kifungu cha 31(5) kifutwe kwenye rasimu hiyo, kwani kinaondoa uhuru wa waumini wa dini za Kiislamu na Kikristo ambao imani zao zinatofautiana kwa baadhi kuamini kuwa Yesu ni Mungu na wengine kuamini kuwa Yesu siyo Mungu.



“Neno kukashifu dini nyingine asilia yake lilianza kutumika wakati Waislamu walipokuwa wakifanya mihadhara na kusema Yesu si Mungu, ikaonekana kama wanaingilia dini nyingine au wanakashifu, lakini ukweli ni kwamba kwa imani ya Kiislamu Yesu ambaye ni Issa Bin Mariam si Mungu.

Waumini wa madhehebu ya Kikristo wanaamini kuwa Yesu ni Mungu,” alisema Salim Omari Ali.

Salim ambaye ni Mjumbe wa Mabaraza ya Katiba kutoka Shehia ya Kinoe alisema ikiwa kifungu hiki kitaachwa kwenye katiba hata waumini wa dini ya kikristo watakaposema Yesu ni Mungu watakuwa wamekashifu imani ya dini ya Kiislamu kwa sababu imani yao inasema kuwa Yesu si Mungu na hivyo kuleta mifarakano ambayo itasababisha machafuko.

Alisema katika kundi lao ambalo lilipangiwa kujadili mambo ya maadili katika rasimu ya katiba wameona ili kuondoa mikanganyiko na mifarakano ambayo baadaye inaweza kuleta machafuko ya kidini ni vyema kifungu hicho cha 31 (5) kiondolewe kabisa ili kutoa uhuru kwa waumini wa pande zote.

Wajumbe waliochangia kifungu hicho walikubaliana na wenzao wa kundi hilo wakisema kuwa rasimu ya katiba imeweka maeneo ambayo yanaweza kuzusha machafuko badala ya kujenga na kwamba ni vyema masuala ya kiimani yaachwe kama yalivyo.

No comments:

Post a Comment