Tuesday, August 13, 2013

kupigwa risasi kwa shekh ponda:waislamu morogoro, dar wawatimua polisi,

Waumini wakisubiri zamu yaokwenda kumjulia hali
 Sheikh Ponda hospitali ya muhimbili....



SAKATA la kupigwa kwa Katibu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, limezidi kuitesa serikali, safari hii Tume ya Haki na Jinai ya Jeshi la Polisi chini ya Mwenyekiti Kamishina wa Jeshi hilo Isaya Mngulu iliyoundwa kuchunguza kujeruhiwa kwake ikikwaa kisiki.

Jana wajumbe wa tume hiyo, walitimuliwa jijini Dar es Salaam na huko Morogoro walipokwenda kufanya mahojiano na baadhi ya viongozi na wafuasi wa kiongozi huyo.

Jijini Dar es Salaam tume hiyo ilitimuliwa kufuatia maofisa wake kushindwa kujitambulisha wakati wakitaka kumhoji Sheikh Ponda katika Hospitali ya Muhimbili alikolazwa.



Taarifa ya kutimuliwa kwa maofisa wa tume hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Is-haq Rashid, msemaji wa familia ya Sheikh Ponda, wakati akiongea na waandishi wa habari.

Is-haq alisema juzi wakati maofisa hao wanaodaiwa kutoka tume ya haki jinai ya Jeshi la Polisi walifika katika chumba alicholazwa Sheikh Ponda pasipo kujitambulisha kama ni maofisa wa tume au askari wanaotaka kujua ukweli wa tukio la kujeruhiwa kwa kiongozi huyo.

“Walikuja na wakawa wanaongea na Sheikh pasipo kujitambulisha, kwa bahati nzuri tulimtambua yule Isaya Mngulu na hapo ndipo tukaanza kuhoji sababu ya ujio wao wa kimya kimya pasipo kututaarifu na hata walipopata nafasi ya kuongea na mgonjwa pia hawakuweza kujitambulisha nia yao,” alisema Is-haq.

Aliongeza kuwa kutokana na viashirio hivyo, hawana imani na utendaji wa tume hiyo na hivyo hawatatambua matokeo yoyote yatakayotolewa kwa kuwa hayana lengo la kuwashirikisha.
Waumini wa dini ya kiislamu Manispaa ya Morogoro wakiwa
 katika ibada ya
swala ya adhuri eneo la kituo kikuu cha polisi mkoa wa Morogoro 


Alisema mwanzoni walidhani polisi walikuwa na nia ya kusaidia kubaini ukweli wa tukio hilo na kwamba wamebaini dhamira ya jeshi hilo ni kutafuta njia ya kujisafisha.

Is-haq alisema wao kama familia kwa sasa wameshaanza kukusanya ushahidi na wakishaukamilisha watatoa taarifa kwa umma juu ya mtu aliyefanya unyama huo.

Wajumbe wa tume hiyo pia walikwaa kisiki mkoani Morogoro baada ya baadhi ya wafuasi wa Ponda kugoma kutoa maelezo.

Akizungumza na Waislamu waliokuwa wamefurika kituo kikubwa cha polisi mkoani Morogoro baadae kuhamishiwa msikiti mkuu, Mwenyekiti wa taasisi hiyo mkoani humo Ayubu Salum Mwinge alisema hawatatoa ushirikiano huo kwenye tume hiyo kwa kuwa wakosaji ni polisi na haikuwashirikisha wao kama waathirika wa suala hilo.

“Tume hiyo ni yao na haijatushirikisha kama waathirika wa jambo hili, baada ya kuvutana kwa muda tumewataka watushirikishe na sisi humo,” alifafanua Mwinge.

Aliongeza kufafanua kuwa mbali na tume hiyo kuwashirikisha viongozi kutoka kwa mwanasheria na mkurugenzi wa makosa ya jinai (DPP) hawana imani nayo kwa kuwa wote ni wajumbe wa serikali.

“Ikumbukwe kuwa hawa wanatekeleza agizo la kiongozi wa serikali la ‘wapigwe tu’. Ni hivi karibuni bungeni Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwangiza polisi kufanya hivi, sasa sisi tutakubaliana nao kivipi juu ya tume yao hiyo?

“Nikweli wapo wananchi walioshuhudia tukio zima, lakini hatuwezi kuwaita kutoa ushuhuda huo kwa kuwa kwanza ni tume ya upande mmoja yaani polisi, ni wapigaji risasi, na ni wao wachunguzaji,” alisema.

Hivi karibuni Sheikh Ponda akiwa mjini Morogoro kwenye sherehe za Idd alipigwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni risasi na watu wanaodaiwa kuwa polisi baada ya kumzuia barabarani akielekea kuswali swala ya jioni.

CHADEMA waijia juu polisi

Wakati huo huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimelishambulia Jeshi la Polisi kikisema kuwa haliwezi kukwepa dhamira ya kutaka kumuua Sheikh Ponda.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Profesa Abdallah Safari akiongea na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam, jana alisema imekuwa ni kawaida ya Jeshi la Polisi kuua watu hovyo na kisha kutafuta sehemu ya kujificha huku akikumbushia mauaji mbalimbali yanayodaiwa kufanywa na jeshi hilo kuanzia miaka ya 80.

Miongoni mwa mauaji aliyokumbusha ni pamoja na vifo vya wakata miwa 20 waliouawa mkoani Morogoro mwaka 1980, ambao walikuwa wakidai haki ambapo kamanda wa polisi wa wakati huo mkoani humo alifukuzwa kazi.

Alisema utendaji wa serikali kwa wakati huu ni tofauti na wakati wa Mwalimu Nyerere ambaye alimlazimisha IGP Hamza Azizi ajiuzulu nafasi yake kwa kisa cha kumgonga mtu na kumsababishia kifo.

“Leo wanaosababisha au kusimamia mauaji wanaongezwa vyeo. Mfano ni mauaji ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi, Kamuhanda ameongezwa cheo badala ya kuwajibishwa na huu ni mfumo mbovu wa kiutawala,”alisema Prof. Safari.

Kuhusu Tume ya Haki Jinai ya Jeshi la Polisi, Profesa Safari alisema CHADEMA haina imani na tume hiyo inayoongozwa na Mngulu kwa kuwa ni ofisa aliyefanya kazi mbalimbali ikiwemo tukio la bomu la Arusha pasipo kutoa majibu hadi leo.

Alisema ni wakati wa Watanzania wenye kuitakia mema nchi kuunganisha nguvu na kuilazimisha serikali kuchukua hatua juu ya maovu yanayofanywa na watendaji wake kwa raia.

Ponda atuma salamu kwa watetezi wa haki

Akizungumza na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA), John Heche aliyemtembelea hospitalini hapo jana, Sheikh Ponda alimuomba kiongozi huyo amfikishie salamu kwa watu wote wenye kutetea haki za wananchi.

“Nimefurahi… nimefurahi sana mmekuja kunijulia hali naomba nifikishie salamu zangu kwa wapenda haki wote,” alisema Sheikh Ponda.

No comments:

Post a Comment