Wafanyabishara wa matunda aina ya maparachichi katika Soko la Wakulima la Soweto Mkoa wa Mbeya,
wameiomba Serikali na wadau mbalimbali kutoa miche ya kisasa kwa wakulima ili waweze kuzalisha kwa wingi na kuboresha maisha yao.
Wamesema ubora wa maparachichi yanayozalishwa mkoani Mbeya sasa yameanza kuzidiwa na yale ya Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuwa wanatumia miche bora.
Mfanyabiashara Athanas Saimon akiwa kwenye soko hilo alisema maparachichi yanayopatikana wilayani Rungwe mkoani Mbeya yameshuka ubora kutokana na kutumia miti ya asili wakati mkoani Kilimanjaro wanatumia miche ya kisasa.
Alisema kwa kuzingatia ubora, gunia moja la maparachichi kutoka Kilimanjaro kwa sasa linauzwa Sh100,000 wakati ya kutoka Rungwe yakiuzwa kwa bei pungufu ya hiyo.
“Tunataka Serikali itusaidie kupata miche bora ili wakulima waipande na kuzalisha matunda mengi ya kuweza kusindika kwenye kiwanda kilichopo Rungwe’’ alisema.
Aidha baadhi ya wakulima waliomba kupatiwa mikopo isiyokuwa na riba ili kuwawezesha kubuni miradi endelevu licha ya kutegemea kilimo ambapo kwa sasa mazao mengi yameingia katika ushindani wa masoko na hivyo kupelekea baadhi ya wakulima kutonufaika na kilimo na badala yake wafanyabishara wamekuwa wakiingia mashambani kuwarubuni wakulima.
No comments:
Post a Comment