SPIKA wa Bunge, Anna Makinda, amewataka wajumbe wa kamati za Bunge kuachana na tabia ya kupokea bahasha (rushwa) kwa kuwa itachangia kuiuza nchi.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya wajumbe wa kamati tatu za Bunge za Serikali za Mitaa (LAAC), Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Bajeti, Makinda alisema kuwa ni vyema wajumbe wa kamati hizo wakatumia nafasi waliyokabidhiwa kwa ajili ya kutoa huduma za msingi kwa wananchi.
Alisema kuwa iwapo wabunge watashindwa kuwa waadilifu na badala yake wakaendelea kupokea bahasha hizo kuna hatari ya kuiuza nchi na hivyo kutaka tabia hiyo ikome mara moja.
“Iwapo sisi wabunge katika kamati zetu hatuwi waadilifu, ndugu zangu tutakuwa tunaiuza nchi hii, naomba bahasha, tafadhali, zikome mara moja kwa upande wetu,” alisema.
Akitolea mfano, Makinda alisema kuwa Bunge la Uingereza liliwachukulia hatua kwa kuwafungulia kesi za jinai wabunge wake waliobainika kupokea mapato ya udanganyifu/ ziada.
Spika Makinda alisema kuwa ni vyema wabunge wakatunza maadili yao kwa kuwa masuala kama hayo yanaweza kutokea, kwamba wakionyesha mfano mzuri hata wanaotoa bahasha wataogopa na kuweka hesabu zao vizuri.
“Njia ya kukwepa kuwajibishwa kwa uchafu wa hesabu zao ni kuandika vizuri na si kutoa vibahasha,” alisema.
Hata hivyo, Makinda alisema kuwa wajumbe hao wanapaswa kupata ushauri kutoka katika ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili kubaini halmashauri zinazopaswa kuwa na mapato makubwa lakini zinashindwa kufanya hivyo na kuwataka wajumbe hao kuzifanyia kazi.
Alisema kwamba hatua ya kuwakemea au kutoa lugha kali kwa maofisa mahesabu wa taasisi za serikali hazisaidii bali hoja ni kuweka matatizo yanayowakabili kwa uwazi bila kuwepo kwa uonevu wala chuki.
“Fedha zetu kidogo tukizisimamia vizuri zitakuwa zinakua kila mwaka na wananchi wataona maendeleo kama inavyotarajiwa na watapata moyo wa kujituma kwa kufanya kazi ya kupambana na umaskini katika maeneo yao,” alisema.
Aliongeza kuwa ni muhimu kutumia mafunzo hayo na kufanya kazi kwa undani katika wizara nyeti na mashirika na wale watakaoangaliwa na kufuatiliwa watapata somo na kujua kuwa wanafuatiliwa.
Spika alisema kuwa hatua hiyo itajenga hofu kwa wengine kwa kuwa watabaini kuwa wanaweza kufikiwa.
“Mapendekezo ya kazi zetu mtakazozifanya naomba yawekwe bayana, Bunge litazingatia taarifa hiyo nzito mtakayoitoa kwa kuwa itakuwa imefanyiwa kazi kwa undani na litafanya maamuzi,” alisema.
Alisema kuwa kamati za kisekta zinaangalia matumizi ya kila siku ya mwaka lakini wajumbe wa kamati hizo wana uwezo wa kuangalia kwa undani, hivyo uwezekano wa kurudisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma uko kwao.
Tuhuma za baadhi ya wajumbe wa kamati kujihusisha na vitendo vya kuomba rushwa zimekuwa zikiwaandama baadhi ya wabunge ambapo Juni mwaka juzi, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, aliwatuhumu kwa kuwataja kwa majina wabunge wenzake watatu wa kamati ya LAAC kuwa waliomba rushwa kwenye moja ya halmashauri.
Pia mbunge wa Bahi, Omar Badwel (CCM), anakabiliwa na mashtaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam ya kudaiwa kuomba rushwa kwa mkurugenzi wa halmashauri moja mkoani Pwani.
Katika hatua nyingine, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, alisema kuwa anatambua tatizo sugu linalozikabili baadhi ya wizara, idara na taasisi za serikali la kushindwa kupelekewa kwa wakati fedha za bajeti zinazoainishwa.
Utouh alisema kuwa kutokana na tatizo hilo kuendelea, atafanya ukaguzi wa bajeti kuanzia kuandaliwa, kupitishwa na kutekelezwa na kuweza kuishauri serikali kupitia Kamati mpya ya Bajeti.
Alisema kuwa anaandaa mchakato wa mafunzo zaidi na kuwapeleka baadhi ya wajumbe wa kamati hizo katika nchi mbalimbali ili kuweza kupata uzoefu wa namna kamati hizo zinavyofanya kazi.
“Mwanzoni mwa Septemba mwaka huu ofisi yangu kwa kushirikiana na ofisi ya Bunge tutakuwa wenyeji wa mkutano wa Umoja wa Kamati za PAC katika Nchi za Kusini mwa Afrika (SADCOPAC) ambao unatimiza miaka kumi tangu kuanzishwa,” alisema.
Alisema kuwa mkutano huo utaenda sambamba na kuanzishwa kwa umoja wa kamati za PAC barani Afrika utakaojulikana kama ‘AFROPAC’.
No comments:
Post a Comment