UKIZUNGUMZIA ukosefu wa maadili kwa wasanii, lazima utawagusa wasanii wa kike na kitu
utakachowatuhumu nacho ni mavazi yasiyoendana na maadili ya Mtanzania. Mavazi hayo huwaonyesha sehemu za maungo yao, kana kwamba wapo watupu maana wengi wao hupenda kuvaa mavazi yanayobana miili yao ili tu kuonyesha shepu na maungo yao ikiwemo ukubwa wa makalio yao, huku ikidaiwa kuwa uhalalisha biashara ya ngono kwa wateja wanaowahitaji.
Lakini ni kweli kuwa wasanii wa kike tu ndiyo wanaovaa mavazi yenye kuonyesha maungo yao? Je, wasanii wa kiume wanaovua nguo wakiwa jukwaani nao tuwahisi vipi? Je, hao nao wanajihusisha na biashara za ngono.
Usiniambie mzuka, mzuka ni nini? Mzuka ndiyo uvue nguo, mzuka ndiyo
ushushe suruali yako hadi chini ya makalio yako, mzuka ndiyo uonyeshe matiti yako, upuuzi huo!
Hivi karibuni katika ukumbi wa Sansiro, kulikuwa na onyesho la Miss vyuo vikuu, ambapo wasanii maarufu walialikwa kutumbuiza lakini cha kushangaza baadhi yao walipanda jukwaani wakiwa wameshusha suruali zao chini ya makalio, jambo ambalo linakiuka maadili ya Kitanzania na kwa nchi nyingine hutiliwa shaka watu hao.
Wasanii wengi wanasahau kuwa jukwaa ni sehemu kubwa ya kuwanyanyua ama kuwashusha wasanii, kwa kuwa ni sehemu inayowakutanisha wasanii na mashabiki wa aina tofauti, wapo wanaowapenda na wasiowapenda, hivyo kuvua nguo ni kujiongezea maadui kwa wasiopenda kazi zako.
Kwanini uongeze maadui kwa kufanya mambo ambayo hayatakuongezea maksi katika sanaa yako, kwanini usiwe mstaarabu ukapanda jukwaani na kuimba nyimbo zako kwa kutumia njia mbadala tofauti na kuvua nguo ili kushawishi mashabiki wakushangilie.
Mbona njia za kushawishi mashabiki zipo nyingi, kwanini msitumie hizo, fika mapema panda jukwaani kwa wakati hakuna shabiki atakayekupinga lakini ukifika umechelewa ukipanda umelewa hakuna shabiki atakayekupenda.
Mbona mwimbaji Joseph Haule ‘Profesa J’ havui nguo jukwani nabado anapendwa kupitiliza inakuwaje wewe, jiulize na ubadilike msanii wa Tanzania anatakiwa kufuata maadili yake na kuacha kuiga mambo ya kimagharibi.
Wapo wakina Farid Kubaga ’FD Q’, Ambwene Yessaya ‘A Y’ na wengine wengi wanafanya vizuri kila siku lakini hawavui nguo kuonyesha maungo yao wala vifua vyao, kwani hawa si wasanii wa hiphop sasa ubabe wako wa nini?
Nani aliyekwambia kuwa ukivaa nguo chini ya makalio ndiyo utapata mashabiki wengi, au ukionyesha kifua wazi ndiyo utapendwa na wasichana, nidhamu pekee ya msanii ndiyo itakufanya kuwa juu na kupendwa na kila rika.
Msanii mwenye nidhamu hashindwi kumshawishi mshangiliaji, mwenye nidhamu ashindwi kumshawishi mfuatiliaji muziki wake kwa kuwa anajua akitazama kazi yake haitokuwa na madhara, lakini kwa sasa kila kitu hovyo.
Mashabiki tuwakatae hawa wanaovua nguo jukwaani na kubaki watupu kama mnavyowakataa wacheza shoo wa bendi mbalimbali ambao huvaa mavazi yasiyoendana na maadili ya Mtanzania.
No comments:
Post a Comment