KWA mara nyingine, wakulima wa zaidi ya 100 wa kata ya Hembeti, wilayani Mvomero, Morogoro wamefunga barabara ya Turiani-Morogoro - Dar es Salaam na Tanga, wakiitaka serikali iwarejeshee bonde lao la mpunga la Mgongola lenye mgogoro wa mapigano ili walilime.
Tukio hilo lilizua tafrani kubwa kwa Diwani wa Kata ya Hembeti, Juma Majala, akijeruhiwa vibaya na mkuu wa wilaya hivyo, Antony Mataka, akipopolewa mawe na wakulima hao huku wasafiri wakikwama kwa takriban saa sita na wengine kulazimika kurudi walikotoka.
Akizungumza na mwandishi toka mafichoni, mlinzi wa amani na mtendaji wa kata hiyo, Henry Kabuye, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo, ambapo magari zaidi ya 10 yakiwepo ya abiria na mizigo yalikwama kijijini hapo.
Kabuye alisema tayari alikuwa ametoa taarifa kwa vyombo husika akiwemo OCD wa Wilaya, Emanuel Gariamoshi, na mkuu wa wilaya hiyo, waje kwa ajili ya kumaliza tatizo hilo ambalo ni la muda mrefu sasa.
Wakizungumza na waandishi wa habari, wakulima hao walisema kuwa serikali imekuwa haiwatendei haki kwa kutotoa ufumbuzi wa kudumu dhidi ya mapigano baina yao na wafugaji, ambapo vibanda mashambani mwao vilichomwa.
Hii ni mara ya pili kwa siku za hivi karibuni wananchi wa vijiji vya Kisala na Kwamtonga Kata ya Sungaji wilayani humo, kufunga barabara hiyo baada ya wafugaji kuwalisha wanyama shamba la mahindi ekari tatu mali ya Alex Kazimheza, ambapo wakulima kwa hasira waliwakatakata kwa mapanga ng’ombe zaidi ya 15.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, aliwapa siku saba wafugaji kuhama kwa hiari na siku 14 kuhama kwa lazima pamoja na kuwatoza faini ya sh milioni saba, jambo ambalo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kata ya Sungaji, Musa Kombo alibeza akisema siku saba zimekuwa siku 70 za kuwasumbua wakulima.
Wananchi hao waliamua kupiga kambi kwenye kizuizi kilicho kwenye barabara hiyo ambayo sasa inajengwa kwa kiwango cha lami na kampuni ya kigeni kutoka China, tangu juzi jioni na kuendelea kukaa hapo hadi jana wakidai kutoka vijiji mbalimbali vya kata hiyo vya Dihombo, Hembeti, Kisalasala, Lukenge, Kambala na Mkindo.
No comments:
Post a Comment