MBUNGE wa Viti Maalumu, Suzana Lyimo (CHADEMA), amesema usimamizi na uendeshaji mbovu wa shule katika ngazi zote ni chanzo cha matokeo yasiyoridhisha ya elimu nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Lyimo katika mahafali ya tano ya darasa la saba katika shule ya msingi Ndalala, Mwenyekiti wa M4C Jimbo la Ukonga, Nixon Tugara, alisema ili kuhakikisha taifa linakuwa lenye ustawi ni lazima usimamizi na uendeshaji wa taasisi za elimu katika ngazi zote unafanyika kwa ufanisi.
Alisema elimu kwa Watanzania ni muhimu hasa katika mbio za kupambana na maadui ujinga, maradhi na umaskini.
“Silaha pekee ya kuwashinda maadui hawa ni elimu bora, maana elimu kama inavyobainishwa na sera ya elimu na mafunzo ni mchakato ambao mtu hupata maarifa na ujuzi wa kujitambua na kujiweka sawa katika kupambana na mazingira na mabadiliko ya mara kwa mara ya kijamii, kisiasa na kiuchumi,” alisema.
Tugara aliwaasa wahitimu hao 53 wajipange kukabiliana na mipango ya kuhujumiwa kwa Katiba mpya na kudai kuwa hapo ndipo penye nia ya kupata haki za kielimu zilizokosekana kwa miaka 52 ya uhuru wa Tanganyika.
Mwalimu wa shule hiyo, Mariam Omary, akisoma risala ya shule, alisema shule hiyo inakabiliwa na ukosefu wa maji, uzio na kompyuta kwa ajili ya somo la Tehama.
No comments:
Post a Comment