Kiongozi wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila
amenusurika kifo na mtu mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la
Mikidadi, ambaye yupo mahututi katika Hospitali ya Temeke, baada ya
kushambuliwa na watu wanaodaiwa kuwa na mzozo wa ardhi eneo la Kurasini,
jijini Dar es Salaam.
Mchungaji Mtikila alikumbwa na mkasa huo Ijumaa wiki iliyopita baada ya
kufika katika eneo hilo kwa nia ya kutaka kuwaondoa watu hao wa familia
tatu tofauti ambao wanaishi katika eneo hilo.
Kipigo hicho ambacho kimemsababishia majeraha ya kisogoni na hata
kushonwa nyuzi tatu kichwani, kuvimba usoni na maumivu makali mwilini
yalitokana na kipigo kutoka kwa familia mbili tofauti zinazoishi katika
eneo hilo ambao wanapinga kuhama.
Pia katika sakata hilo, Mtikila anadai kupoteza simu mbili, pesa taslimu
Sh400,000 na Dola za Marekani 2,000 na siku ya tukio na alifika hapo
akiwa ameongozana na watendaji wa Dawati la Msaada wa Kisheria katika
taasisi yake ya Liberty Fund International.
Kamanda wa Polisi Temeke, Engbert Kiondo alikiri kutokea kwa tukio hilo
na kusema kuwa wanalifanyia uchunguzi na taarifa kamili itatolewa kesho
Jumanne.
“Ni kweli suala hilo limeripotiwa hapa na tunalifanyia uchunguzi na
kesho Jumanne nitatoa taarifa rasmi kwa waandishi wa habari,” alisema
Kiondo.
Mtikila alisema, mara baada ya kufika eneo hilo, alikwenda katika nyumba
ya kwanza na kuwakuta walinzi ambao walikubali na kuondoka katika eneo
hilo kwani tayari notisi walikuwa nayo na walikuwa wanatambua kuwa
wanatakiwa kuondoka.Alisema baadaye walikwenda katika nyumba ya pili
ambayo anaishi mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la Rubein Sanga ambaye hata
hivyo vitu vyake vingi akuwa amekwisha vihamisha.
Alisema wakiwa mbele ya nyumba hiyo gari la polisi lilifika na wakiwa
hawana hili wala lile vijana ambao anawataja kuwa ni wa Sanga walianza
kuwashambulia kwa kutumia nondo na kila aina ya silaha za jadi.
“Walinipiga sana hadi nikapoteza fahamu na wakawa wanasema huyo Mtikila
bebeni na mumchome moto, walitaka kuniua kwani walinikwida tai hadi
ikakatika,” alisema.
Na kuitaja pia familia ya Evelyne Mboya kuwa ilishiriki kuwashambulia.
Alisema wakati vurugu zinaendelea, ndipo akatokea mmoja wa jirani
wanaoishi katika eneo hilo aliyemtaja kwa jina la Mikidaki: “Yule bwana
alipojaribu kunitetea kuwa nisiendelee kupigwa alipigwa nondo kichwani
na akaanguka na alishambuliwa hadi kuzirai na hajapata fahamu hadi leo,”
alisema.
Mchungaji Mtikila alisema alikuwa ameambatana pia na walinzi wawili
(mabaunsa), wafanyakazi wa dawati lake la msaada wa kisheria lililopo
chini ya taasisi yake ya Liberty Fund International na mmiliki halali wa
eneo hilo, Omar Salum Muhsin ambaye pia alijeruhiwa mkononi kwa nondo.
Mtikila aliwataja wafanyakazi wake waliojeruhiwa kuwa ni Hemed Wendo na
Gray Mhando na akiwa amezirai alibebwa na kupandishwa katika gari hadi
Kituo cha Polisi Chang’ombe ambako yeye na wenzake walifunguliwa jalada
kwa shtaka la kuingia isivyo halali katika eneo la watu wengine.
No comments:
Post a Comment