Monday, November 19, 2012
UFUJAJI WA MALI ZA WAISLAMU.MSIMAMIZI ANAPOSHIRIKI HUJUMA !! YA CHANG'OMBE KUING'OA RASMI BAKWATA .
MARKAZ CHANG’OMBE DAR ES SLAAM
PLOT NO. 311 BLOCK “T” CHANG’OMBE
Hivi karibuni kumetokea wimbi kubwa la wafanyabiashara kuvamia eneo la kiwanja cha waislamu kilichoko Markaz Chang’ombe kwa mgongo wa kuuziwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA). Eneo hili limesajiliwa kama PLOT NO. 311 BLOCK “T” CHANG’OMBE lenye ukubwa wa HEKARI 27.7 lililokuwa limekusudiwa kwa ajili ya matumizi ya shughuli za dini ya kiislamu hususan kujenga Chuo Kikuu cha kwanza cha Kiislamu Tanzania.
Eneo hili linahistoria kubwa katika historia ya uislamu hapa Tanzania, kwani mwaka 1964 waislamu wa Tanzania wakiongozwa na Marehemu TEWA SAID TEWA akiwa ni Waziri wa ARDHI walishuhudia likiwekwa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu cha kiislamu. Hata hivyo kwa fitna za wakati huo zilizotoka nje ya waislamu chuo hicho hakikujengwa.
Kwa miaka yote kiwanja hiki hakikuwahi kumilikiwa na BAKWATA hadi mwaka 1984 kiliposajiliwa rasmi na Wizara ya Ardhi kuwa chini ya usimamizi wa BAKWATA ikiwa ni mali ya WAKF.
Kwa mujibu wa sheria za Kiislamu ambazo ni sehemu ya sheria halali za nchi hii mali ya WAKF haipaswi kuuzwa na kutumiwa kinyume na malengo ya WAKF. Vile vil
e hata kwa mujibu wa sheria ya mirathi ya kiserikali sura ya 352 yaani The Probate and Administration of Estates Act Cap 352 kifungu no. 150 hairuhusiwi kuuzwa au kutumika mali ya wakf kinyume na makusudio ya wakf husika. Lakini kutokana na ufisadi, hila na hujuma kiwanja hiki cha WAKF kimekuwa kikimegwa na kuuzwa kwa usimamizi wa BAKWATA kwa wafanyabiashara kwa mikataba tata na ya kifisadi.
Mamlaka za Ardhi yaani Wizara ya Ardhi na Manispaa ya Temeke zimekuwa mara kwa mara zikigawa kiwanja hiki kutokana na maombi ya BAKWATA kama inavyo onekana hapa chini.
Kwa mfano mwaka 2000 BAKWATA kwa barua kumb. Namba MK.U.50/3/19 ya tarehe 6.11.2000 na barua MK/M.20/4/3 ya tarehe 15.5.2001 zilizosainiwa na Alhaj M.R. Kundya (aliyekuwa Katibu Mkuu BAKWATA wakati huo) iliomba eneo hilo PLOT NO. 311 BLOCK “T” CHANG’OMBE ligawanywe lifanyiwe “subdivision” kutoa vipande vitatu na kuwa:
. Plot No. 331/1 hekari 12.2 isajiliwe kwa jina la THE REGISTERED TRUSTEES OF MILLENIUM MUSLIM UNIVERSITY COLLEGE.
. Plot No. 311/2 hekari 3.5 isajiliwe THE REGISTERED TRUSTEES OF DAR ES SALAAM YEMEN COMMUNITY FOR CULTURE AND CHARITY (DYCC)
. na kipande kilichosalia Plot No. 311/3 hekari 12 kibaki kuwa chini ya BAKWATA.
Kwa hivyo basi mwaka 1984 ukubwa wa kiwanja hiki ukiwa ni hekari 27.7 BAKWATA ilipoingia ikakigawa gawa na kubakia nazo hekari 12 tu bila ya yenyewe BAKWATA kufanya maendeleo yoyote toka kilipoangukia mikononi mwao!
Ili kutekeleza makusudio ya kugawanya kiwanja hicho Wadhamini wa BAKWATA Marehemu ABUBAKAR KOMBO na Alhaj SEFU MOMBA walirejesha offer ya kiwanja Wizarani ili Wizara igawanye kiwanja hicho kama BAKWATA ilivyoomba hapo juu. Muslim University College ikamilikishwa kiwanja kilichomegwa na kuwa PLOT NO. 311/1 BLOCK “T” CHANG’OMBE kwa offer No. LD/195976/LO ya tarehe 11.6.2001 kwa matumizi ya ujenzi wa chuo cha Kiislamu. Mpaka leo chuo hicho hakijajengwa na wala hakuna dalili yoyote ya mipango ya kutekelezwa jambo kama hilo.
Alhaj Sefu Momba ambaye alifanya kazi hii kuomba kugawanya eneo kwa kurejesha “surrender” offer kama mdhamini wa BAKWATA ndiyo huyo huyo mdhamini wa MUSLIM UNIVERSITY COLLEGE taasisi iliyoombewa kumegewa kiwanja hiki MUHIMU CHA WAISLAMU!!! Ni wazi hapo utaona kuna mgongano wa kimaslahi, uliotumika kufisidi mali ya waislamu. Vile vile hapa tunapenda ummah na serikali ifahamu kwamba kwa barua ya terehe 29.3.2006 Kumb. Na. ADG/T1/4/5 iliyoandikwa na Kabidhi Wasii Mkuu aliyekuwepo wakati huo C.O.Kaisi kwenda kwa Kamishna wa Ardhi ilionyesha kuwa taasisi ya MUSLIM UNIVERSITY COLLEGE si halali kwani viongozi wake walighushi saini za wajumbe wanaodaiwa kuunda taasisi hiyo, hivyo hati yao ya usajili ilifutwa na Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali!
Hata hivyo pamoja na upungufu huo mkubwa wa kisheria na wa kiuadilifu taasisi hiyo iliendelea kumilikishwa ardhi ya Waislamu. Na mara tu baada ya kumilikishwa Plot No. 311/1 MUSLIM UNIVERSITY COLLEGE kwa barua yao MUCE/E.16.19/40 ya tarehe 24.11.2003 waliomba plot waliyomilikishwa igawanywe tena kwa ajili ya kujenga ofisi na hospitali. Katika maombi yao waliomba pia kwamba baada ya mgawanyo sehemu ya ofisi imilikishwe kampuni ya QUALITY GROUP (1999) LTD inayomilikiwa na mfanyabiashara YUSUF MANJI kwa hoja kuwa QUALITY GROUP watafadhili ujenzi wa hospitali katika eneo lililobaki na pia kuwajengea shule katika kiwanja kingine. Inasikitisha kusema kuwa hakuna lililofanyika. Si shule wala hospitali ilioyojengwa. Hoja ya ujenzi wa hospitali na shule ilikuwa ni hoja ya kubuniwa ili kuhalalisha nia ovu iliyokuwepo kujipatia ardhi ya Waislamu kifisadi.
Hata hivyo bado maombi ya mgawanyo yalifanikiwa na QUALITY GROUP (1999) LTD ilimilikishwa PLOT NO. 311/1 kwa HATI MILIKI NO. 55274 iliyotolewa tarehe 8.12.2003. Baada ya QUALITY GROUP kumilikishwa eneo hilo lililomegwa; BAKWATA iliomba kipande kilichobaki PLOT NO.311/3 kigawanywe tena! Kilipogawanywa vikatoka vipande viwili PLOT NO. 311/3/1 na PLOT NO. 311/3/2. Wabadhirifu walio ndani ya BAKWATA hawakuishia hapo kwani kwa barua ya tarehe 24.8.2009 Kumb. Na. MK/N.20/4/75 toka BAKWATA kwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, BAKWATA iliomba ipatiwe offer ya sehemu nyingine ya kiwanja hicho kwa ajili ya “kukiendeleza”. Tarehe 9.9.2009 Manispaa ya Temeke ilitoa offer yenye Kumb. Na. LD/TM/CH/16083/5/TJM kumilikishwa BAKWATA kiwanja kilichomegwa na kuwa PLOT NO. 311/4 BLOCK “T” CHANG’OMBE. Hata hivyo tofauti na malengo yaliyoombewa offer yaani kuendeleza eneo hilo, BAKWATA mara tu baada ya kupewa offer waliuza eneo hilo ndani ya muda mfupi kwa Kampuni ya AGRITANZA!!
BAKWATA haikuishia hapo iliomba tena Manispaa kufanya subdivision nyingine ya kiwanja kilichobaki kupitia barua ya tarehe 2.2.2011 Kumb Na. MK/AR/010/49 kwa madhumuni ya “kujenga kituo cha watoto yatima”. Hapo ilifanyika subdivision nyingine na kutolewa kiwanja PLOT NO. 311/3/4. Bila ajizi wala aibu kiwanja hiki nacho kiliuzwa chapchap kwa Kampuni ya AGRITANZA mara tu baada ya subdivision kufanyika!!!
Inatia uchungu mkubwa kusema kuwa ukubwa wa eneo hili kabla ya kumegwa megwa na kuuzwa na BAKWATA ilikuwa ni hekari 27.7 Lakini baada ya kumegwa na kuuzwauzwa eneo lililobaki hekari chache sana. Umma wa kiislamu umejawa na mshangao kwa kitendo cha BAKWATA kuuza kifisadi eneo hili la waislamu kinyume na sheria za kiislamu kuhusu wakf, kinyume na malengo ya wakf na pia kinyume na sheria ya mirathi ya serikali sura ya 352.
Mnamo mwezi Machi 2006 Sheikh Mkuu na Mufti wa BAKWATA Sheikh Shaabani Simba aliunda TUME iliyoitwa TUME YA KUDUMU YA UCHUNGUZI WA MALI ZA BAKWATA iliyoongozwa na Sheikh Sharif Idrissa Omar (Mwenyekiti), Dr. Ahmed L.A. Twaha (Katibu) na wajumbe walikuwa Alhaji Zulu Lyama, Sheikh Khamis Mataka na Sheikh Hassan Idd Kiburwa. Tume ilichunguza Mgogoro wa Kiwanja Plot No. 311 Block “T” Chang’ombe. Ilihoji watu 38 na ilitoa mapendekezo na hatua za kuchukuliwa. Hapa tutataja mapendekezo machache kama ifuatavyo:-
1. Baadhi ya watendaji wa BAKWATA wawajibishwe.
2. Wote waliotenda makosa ya kijinai wafikishwe mahakamani
3. Kiwanja namba 311/1 kilitolewa kwa QUALITY GROUP kinyume cha maslahi ya UMMA wa kiislamu na kwamba mikataba yote ilikuwa ya rushwa na ufisadi. Tume ikapendekeza HALMASHAURI YA BAKWATA iombe serikali irejeshe umiliki wake wa awali kama ilivyokuwa mwaka 1984.
4. Tume ilijiridhisha kuwa kulikuwepo kwa vitendo vya kughushi nyaraka na sahihi za miongoni mwa viongozi wa BAKWATA kwa lengo la kujinufaisha kifedha, Tume ikapendekeza BAKWATA iteue wakaguzi wakague mahesabu ya BAKWATA makao makuu na wahakiki mali zote za BAKWATA nchi nzima
HATA HIVYO PAMOJA NA KAZI NZURI YA TUME NA MAPENDEKEZO YAKE YENYE TIJA KWA UISLAMU NA MALI ZAKE BAKWATA hakuithubutu kuchukua hatua muhimu zilizopendekezwa na BADALA YAKE kiwanja kikamemegwa tena na KUUZIWA KAMPUNI YA AGRITANZA.
Baada ya kuona vitendo vya kiubadhirifu, kifisadi na hujuma kwa mali za waislamu katika hii PLOT NO. 311 vinazidi na eneo linaelekea kumalizika hapakuwa na jinsi waislamu waliamua kuondoa MUNKAR na kusitisha dhulma na ufisadi ili vyombo vya dola viweze kuchukua hatua kusimamia sheria na kuzuia mara moja ufisadi na kurudisha katika mikono ya waislamu mali yao iliyoporwa.
Serikali badala ya kushughulikia tatizo na kuhakikisha kuwa haki ya waislamu inarudi mikononi mwao, yenyewe imeamua kuwashughulikia walalamikaji!!!!!!.
Sheria ya mirathi ya kiserikali sura ya 352 kifungu no. 145 kimempa mamlaka Rais wa Tanzania kuunda Kamisheni ya Wakf yenye wajumbe wasiozidi wanane (8). Kwasababu zisizoeleweka toka kutungwa kwa sheria hii tarehe 1.3.1963 zaidi ya miaka 40 sasa Rais hajaunda Kamisheni ya Wakf kama sheria inavyomtaka.
Matokeo ya kutokuundwa kwa kamisheni ya wakf ni mali za waislamu kuangukia isivyo halali mikononi mwa BAKWATA. Na matokeo yake mali za waislamu zimekuwa shamba lisilokuwa na mwenyewe kila mwenye nafasi ndani ya BAKWATA anajitwalia apendavyo. Inatia uchungu.
Tunafahamu kuwa kifungu hicho cha sheria ya mirathi ya kiserikali sura ya 352 kinawalakini, lakini ukweli lazima tuseme kuwa lau kama Kamisheni ya Wakf ingeundwa, kama ilivyo Zanzibar Mali za Wakf zisingeuzwa hovyo kama ambavyo BAKWATA imekuwa ikifanya kwa miaka yote ya uhai wake. Nchi nzima mali za waislamu zinazosimamiwa na BAKWATA hazina usalama tena. BAKWATA badala ya kuwa mdhamini “trustee” wa mali za waislamu imegeuka kuwa “dalali” wa mali za waislamu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment