Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), amewasilisha hati ya kumuondolea mashtaka mshitakiwa wa 35, Rashid Omary, akieleza kwamba hana nia ya kuendelea na mashitaka dhidi yake.
UKUMBI WAFURIKA
Ukumbi namba moja wa mahakama hiyo ulifurika watu wakiwamo wanaodaiwa kuwa ndugu wa washitakiwa na makachero wa Jeshi la Magereza na la Polisi waliovaa kiraia na sare za majeshi hayo.
"Baraza hilo (Bakwata) linamiliki mali mbalimbali ikiwamo viwanja na majengo, miongoni mwa hivyo viwanja ni pamoja na kilichopo Chang'ombe Markas," alieleza Wakili Kweka.
Alieleza kuwa, Juni 18, mwaka 2011, Bakwata chini ya Bodi ya Wadhamini wake walikubaliana na Agritanza Ltd kuuziana kiwanja hicho.
"Mauziano yalifanyika na fedha zililipwa na kiwanja cha Chang'ombe Markas kikawa na umiliki halali wa Agritanza Ltd na kiwanja kilipewa namba za usajili 93073," aliieleza Mahakama kuongeza:
"Oktoba 12, mwaka huu Agritanza walianza kuendeleza kiwanja hicho, l na Mukadam."
Aliendelea kudai kuwa, washitakiwa walikaa katika eneo hilo tangu Oktoba 12 hadi 16, mwaka huu walipokamatwa, lakini kabla ya kukamatwa waliharibu msingi wa jengo lililokuwa linajengwa na waliiba baadhi ya vifaa vya ujenzi vilivyokuwa kwenye kiwanja hicho.
Aliendelea kueleza kuwa, washitakiwa walikamatwa Oktoba 16 na walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka yanayowakabili Oktoba 18, mwaka huu.
Washitakiwa kupitia wakili wao, Nassoro Juma, walikana maelezo yote yaliyosomwa dhidi yao, lakini walikubali kukifahamu chombo cha Bakwata.
Pamoja na kuitambua Bakwata, walidai kuwa Baraza hilo ni taasisi iliyosajiliwa kwa ajili ya baadhi ya Waislamu na sio Waislamu wote nchini.
Wakili Juma aliomba mahakama haki za Sheikh Ponda zizingatiwe ikiwamo kutofungwa pingu anapoingia mahakamani kusikiliza kesi yake.
Aliomba wapatiwe maelezo ya mlalamikaji na orodha ya mashahidi pamoja na vielelezo.
Upande wa Jamhuri ulijibu hoja za utetezi kwamba kutoa orodha ya mashahidi na vielelezo hakuna ulazima wa kuvitaja mahakamani na kwamba upande wa utetezi wawe na subira.
Hakimu Nongwa aliamuru kuwa Sheikh Ponda anapopandishwa kizimbani kusikiliza kesi yake asifungwe pingu, upande wa Jamhuri utafute utaratibu mwingine wa ulinzi dhidi yake.
"Kesi hii itaanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa Jamhuri Novemba 29, mwaka huu, washitakiwa wengine dhamana zao zinaendelea isipokuwa Sheikh Ponda na Mukadam ambao wana pingamizi la dhamana kutoka kwa DPP," alisema Hakimu Nongwa wakati akiahirisha kesi hiyo.
Mbali na Sheikh Ponda washitakiwa wengine ni, Kuluthumu Mohamed, Zaldah Yusuph, Juma Mpanga, Farida Lukoko, Adamu Makilika, Athum Salim, Seleman Wajumbe, Salum Juma, Salum Mkwasu na Ramha Hamza.
Wengine ni Halima Abas, Maua Mdumila, Fatihiya Habibu, Hussein Ally, Shaban Ramadhani, Hamis Mohamed, Rashid Ramadhani, Yusuph Penza, Alawi Alawi, Ramadhani Mlali, Omary Ismaili, Salma Abduratifu, Khalidi Abdallah, Said Rashid, Feswali Bakari, Issa Wahabu, Ally Mohamed, Mohamed Ramadhani, Abdallah Senza, Juma Hassani na Mwanaomary Makuka.
Wamo pia Omary Bakari, Hamza Ramadhani, Ayubu Juma, Maulid Namdeka, Farahan Jamal, Smalehes Mdulidi, Jumanne Mussa, Salum Mohamed, Hamis Halidi, Dite Bilali, Amiri Said, Juma Yassin, Athuman Rashid, Rukia Yusuph, Abubakari Juma na Ally Salehe.
Katika hati ya mashitaka, upande wa mashitaka ulidai kuwa, katika shitaka la kwanza, Oktoba 12, mwaka huu huko Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote 50 walikula njama ya kutenda makosa.
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza katika eneo la Chang'ombe Markas, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote 50 kwa jinai walivamia kwa nia ya kutaka kujimilikisha kiwanja ambacho ni mali ya Agritanza Ltd.
Ilidaiwa kuwa, katika shitaka la tatu kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu huko Chang'ombe Markas pasipo uhalali na uvunjifu wa amani, washitakiwa wote kwa pamoja walijimilikisha ardhi ambayo ni mali ya Agritanza Ltd.
Katika shitaka la nne, ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu huko Chang'ombe Markas, washitakiwa wote kwa pamoja waliiba vifaa mbalimbali vya ujenzi yakiwamo matofali 1,500, tani 36 za kokoto na nondo vyote vikiwa na thamani ya Sh. 59,650,000, mali ya Agritanza Ltd.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa katika shitaka la tano linalomkabili Sheikh Ponda peke yake, kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu huko Chang'ombe Markas, akiwa Katibu wa Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, aliwashawishi wafuasi wake kutenda makosa ya jinai.
Washitakiwa wote walikana mashtaka yao kwa nyakati tofauti.
Oktoba 18, mwaka huu washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka yao, lakini Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), aliwasilisha hati ya kiapo cha kupinga dhamana ya Sheik Ponda na Mukadam kwa usalama wake na maslahi ya taifa.
No comments:
Post a Comment