KADHI Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Habibu (49) amekana kumfahamu Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Shekhe Ponda Issa Ponda na wafuasi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.Mbele ya Hakimu Mkazi, Ritha Tarimo mara baada ya kutakiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka awatazame kina Ponda na aelezee iwapo kuna mmoja aliwahi kuingia kwenye Baraza la Maulamaa wa Bakwata.Habibu alidai kuwa hakuna hata mmoja anayefamfahamu katika utendaji wa kazi za Uislamu kama kiongozi kwenye baraza lakini akawatambua kimavazi kuwa ni waumini wa Kiislamu. "Ila kwa kuona, muungwana ishalaa inamuonyesha kuwa kuna baibui, kanzu na kofia (baraghashia) inaonekana kuna Waislamu na wasio Waislamu."Kadhi huyo aliiambia mahakama ; "Nathibitisha kuwa Kampuni ya Agritanza Ltd inamiliki lile eneo kwa Uhalali na kwamba haikupita uchochoroni ikaruka ukuta ikaingia ndani ya hilo eneo, ilifuata utaratibu na kupokea hati zote na haki yake," Alidai kuwa Baraza hilo la Maulamaa linaundwa na wajumbe 10 kutoka mikoa mbalimbali na kwamba mjumbe huteuliwa kutokana na kuwa na kiwango cha elimu kilichopevuka na uadilifu.
Kwa mujibu wa maelezo ya Katiba, vikao hufanyika mara mbili kwa mwaka chini ya Mwenyekiti wa Baraza la Maulamaa pamoja na vikao vya dharura. " Januari 3, 2011, tulifanya kikao cha kawaida ambacho kilikuwa na agenda tatu ikiwemo ya umuhimu wa kujenga chuo Kikuu cha Kiislamu ambapo wajumbe walipendekeza kijengwe katika maeneo ya Dodoma, Tanga ama Chang'ombe."Kutokana na mapendekezo hayo, tuliafikiana kijengwe Chang'ombe lakini ikaonekana kuwa Chuo Kikuu cha Kiislamu kinahitaji sehemu kubwa na pale kuna Ekari 4 hapatoshi," alisema shahidi huyo wa pili wa upande wa mashtaka.Hivyo walimtaka Katibu Mkuu wa Baraza la Maulamaa na timu yake wafanye mchakato wa kutafuta eneo maalumu kubwa ambalo wataweza kujenga chuo hicho Kikuu cha Kiislamu na kwamba baada ya siku nne au tano walipigiwa simu na kuwa wanahitajiwa Makao Makuu (Bakwata).Shahidi huyo alidai kuwa walipofika waliambiwa kuwa kuna kikao cha dharura na kupatiwa taarifa na Katibu Mkuu wao juu ya mchakato huo wa kutafuta eneo kuwa kampuni ya Agritanza Ltd ilijitokeza na kutaka tuwape zile ekari nne na wao watupe ekari 40 huko Kisarawe Pwani."Sisi tuliona ekari 40 kwa ekari 4 ni kama ardhi na mbingu na Mungu alisikia kilio chetu akawaleta hao na tukaona kabla ya mazungumzo twende tukaone, tulipofika Manshalaa eneo lilikuwa sehemu nzuri, linapendeza, linavutia na mimi nilikuwa wa kwanza kuwashawishi wenzangu tukubaliane na mabadilishano na mchakato ukafanyika," aliongeza shahidi huyo mahakamani hapo.
Baada ya kutolewa kwa ushahidi huo, mmoja wa Wakurugenzi wa Kampuni ya Agritanza Ltd, Seleman Mohamed (48) akitoa ushahidi wake aliiambia mahakama hiyo kuwa yeye ni mfanyabiashara na kwamba ni kweli wao waliingia mkataba na Bakwata wa kubadilishana ardhi ekari nne kwa ekari 40.Kesi itakuja kwa ajili ya kutajwa Desemba 18, mwaka huu na itaendelea kusikilizwa Desemba 31, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment