WAKILI anayemtetea Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania,Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake, Juma Nassoro jana amewasilisha ushahidi mzito na kudai kama mahakama ikiwaona wateja wake wana kesi ya kujibu, itakuwa haijatenda haki.
Nassoro alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar esa Salaam, mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa alipokuwa akiwasilisha majumuisho ya kesi inayowakabili Sheikh Ponda, baada ya upande wa mashitaka kufunga ushahidi.
Alidai katika maelezo yaliyotolewa mahakamani kuhusu uwanja wa Markaz Chang’ombe unaodaiwa kuvamiwa, hakuna ubishi kwamba kuna mgogoro wa umiliki wa uwanja huo.
“Haihitaji elimu kubwa sana ya sheria kujua kama hapa kuna mgogoro wa ardhi, kisheria mahakama hii haiwezi kutoa uamuzi wa kuingia kwa nguvu katika uwanja huo bila kuamua kwanza mgogoro wa ardhi.
“Hii si kesi ya kwanza kufikishwa mahakamani kimakosa, kwa kuwa mgogoro wa ardhi haujatatuliwa na Mahakama ya Ardhi, mheshimiwa hakimu, mahakama yako haipaswi kuwaona washitakiwa wana kesi ya kujibu.
“Mashahidi walishindwa kutoa nyaraka, ikiwemo hati miliki ya kuonyesha Kampuni ya Agritanza ina miliki kiwanja hikio kihalali na kuonyesha kwamba awali kilikuwa cha BAKWATA.
“Mheshimiwa uthibitisho wa kutuonyesha mmiliki halali ni yupi, kila mmoja anasubiri kutoa katika mahakama inayostahili na yenye maamuzi yanayostahili sio hapa,”alidai.
Alidai upande wa mashitaka, walishindwa kuonyesha kama washitakiwa walitumia nguvu Oktoba 12, mwaka jana kuingia katika uwanja wa Markaz na ili shtaka hilo lithibitike lazima viwepo vielelezo vya kuiridhisha mahakama.
“Washitakiwa wanadaiwa kuiba vifaa mbalimbali vyenye thamani zaidi ya Sh milioni 59, hakuna shahidi aliyekuja kuieleza mahakama kama kulikuwa na wizi, idadi ya matofali yanayodaiwa kuibwa yanatofautiana na idadi iliyokuwa katika hati ya mashtaka.
“Ushahidi unadai, yalikuwa matofali 2,000,lakini katika hati ya mashitaka inadaiwa yaliyoibwa ni matofali 1,500 na Suleiman wa Agritanza alidai mahakamani hakuna wizi uliofanyika.
“Mheshiwa katika kosa la kula njama haielezi washitakiwa walikula njama kufanya kosa gani, hata katika kosa linalomkabili Sheikh Ponda na Salehe Mukadam la uchochezi pia haielezi waliwachochea wafuasi wao kufanya kosa gani.
“Mpaka ushahidi wa upande wa mshitaka unafungwa kwa mashahidi 17, hakuna shahidi hata mmoja aliyewahi kueleza kwamba uchochezi ulifanyika kufanya kosa gani na walikula njama kutenda kosa gani,”alisema Nassoro.
Alisema mahakama, inatakiwa kuwaona washitakiwa wana kesi ya kujibu pale inapotokea upande wa mashitaka wamewasilisha ushahidi kwa kiwango bila kuacha shaka.
“Unasema waliingia kwa nguvu wakati mashahidi walikuja wakaeleza Sheikh Ponda aliingia wakasalimiana na mlinzi, akawaambia mafundi waache kujenga nao wakamjibu hadi bosi wao awaamuru, aliwaacha akaenda kupiga picha.
“Ponda akiwa anapiga picha, mlinzi alimpigia simu bosi wake kumjulisha,bosi akamwambia uwanja huo una mgogoro, akataka kuzungumza na Sheikh Ponda, mlinzi alimpa simu Ponda wakazunguza, nguvu iko wapi hapo,”alisema wakili huyo.
Alisema kwa upungufu huo, hakuna ushahidi wa kuifanya mahakama iwaone washitakiwa wana kesi ya kujibu na endapo itawaona wana kesi ya kujibu itakuwa haijawatendea haki.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka alidai hakuna ubishi washitakiwa walikutwa katika uwanja wa Markaz, hakuna ubishi walitumia vifaa vya ujenzi kujenga msikiti bila ridhaa ya mwenye mali.
Alisema kutumia kitu bila ridhaa ya mwenye mali, ni wizi na kwamba kuna vielelelezo vya kuonyesha Sheikh Ponda na Mukadam walihamasisha wafuasi wao kwenda katika uwanja huo kwa ajili ya kuukomboa.
“Mheshimiwa hakuna ubishi, waliingia kwa nguvu katika uwanja huo kwa sababu unamilikiwa na Agritanza si wao, tunaomba mahakama yako iwaone wana kesi ya kujibu na iwatake washitakiwa kupanda kizimbani kujitetea ,”alidai Kweka.
Baada ya pande zote mbili kumaliza kufanya majumuisho hayo, hakimu Nongwa aliahirisha kesi hadi Jumatatu ambapo atatoa uamuzi kama washitakiwa wana kesi ya kujibu au la.
No comments:
Post a Comment