Sunday, February 24, 2013

kanisa laongezewa ulinzi !

Polycarp Kardinal Pengo,
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinal Pengo, Askofu wa Jimbo la Zanzibar Augustine Shayo (Katoliki) na Askofu wa Kanisa Anglikana Zanzibar, Michael Hafidh, wamewekewa ulinzi mkali kufuatia kuongezeka kwa vitisho vya mashambulizi dhidi ya viongozi hao wa dini,
Hofu hiyo imeongezeka kipindi hiki, hasa kutokana na taarifa zinazotumwa kwenye simu za mkononi kwa njia ya ujumbe mfupi, kwamba kuna kundi linajipanga kufanya tukio kubwa wakati wa Sikukuu ya Pasaka.

Maaskofu wengine ambao kwa sasa wameongezewa ulinzi ni pamoja na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dk. Alex Malasusa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Valentino Mokiwa.


Hivi karibuni, kundi la watu wasiojulikana lilisambaza vipeperushi visiwani Zanzibar vikiwa na majina ya viongozi wa dini wanaolengwa katika mashambulizi hayo, ambayo hadi sasa hayajulikani yanafanywa na kundi gani na kwa lengo gani.


Padre wa Kanisa Katoliki visiwani Zanzibar, Evaristus Mushi aliuawa wiki iliyopita katika shambulizi la risasi linalodaiwa kufanywa na watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki, huku wakiwa wamevalia (kininja) kwa kuficha sura zao.


Kabla ya tukio la kuuawa kwa Padre Mushi aliyezikwa juzi katika makaburi ya watawa yaliyoko eneo la Katope nje kidogo ya mji wa Zanzibar, kulifanyika shambulio jingine lililomjeruhi kwa risasi Padre Ambrose Mkemi.


Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, tangu taarifa za maaskofu hao kutishiwa kuuawa na kundi la kigaidi, wamekuwa wakichukua tahadhari kubwa katika shughuli zao na makanisa yao yameimarishwa ulinzi.


Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso hakukiri wala kukanusha kupewa ulinzi kwa viongozi hao, ila alisema ni wajibu na jukumu lao kumlinda kila Mtanzania.


“Viongozi wote wa dini wanayo haki ya kulindwa na wala isionekane ni hao tu wa Kikristo. Tunawajibu pia wa kumlinda kila raia,” alisema.

No comments:

Post a Comment