Cardinal Keith O'Brien, Britain's most senior Catholic clergyman |
Kadinali O'Brien, ambaye ni mpinzani maarufu sana wa haki za mashoga, anayelaani ushoga na kuuita kuwa ni kitendo kinachokiuka maadili, ameshitakiwa Vatican na makasisi hao kutoka dayosisi ya St Andrews na Edinburgh, limeripoti gazeti la kila siku la The Guardian.
Wamepeleka malalamiko yao mbele ya Nuncio Antonio Mennini, balozi wa Vatican nchini Uingereza, kwamba walikuwa waathirika wa tabia mbaya ya O’Brien wakati huo, na kutaka ajiuzulu mara moja.
Madai yao yaliwasilishwa mbele ya ofisi ya Nuncio wiki moja kabla ya Papa Benedicto kutangaza kujiuzulu mnamo terehe11 Februari, na kuibua wasiwasi kuwa hatua hiyo ya ghafla iliyochukuliwa na Papa inaweza kuwa na uhusiano na kashfa na skendo nyingi zaidi ambazo zitaendelea kuibuka. Tuhuma za udhalilishaji kingono kwa viongozi wa kanisa zimeuandama uongozi wa Papa Benedicto wa 16, ambaye anatarajiwa kuachia madaraka mwishoni mwa mwezi huu.
Kasisi mmoja anadai kuwa alikuwa na “uhusiano usiofaa na kadinali, jambo lililopelekea kuhitajia ushauri nasaha wa kisaiklojia kwa muda mrefu.”
"Wana tabia ya kufunika na kuulinda mfumo kwa gharama zote,” alisema mlalamikaji. “Kanisa ni zuri, ila lina upande mweusi ambao unapaswa kuwajibishwa. Kama mfumo utabadilishwa, labda utahitaji kubomolewa kidogo.”
Tuhuma ya kwanza dhidi ya kadinali huyo inaanzia mwaka 1980. Mlalamikaji, ambaye kwa sasa ana mke, wakati huo alikuwa na umri wa miaka 18 akiwa mwanafunzi wa seminari katika chuo cha St Andrew College, Drygrange, ambapo O'Brien alikuwa “mwalimu wake wa kiroho.” Anadai kuwa O'Brien alimfanyia tabia mbaya baada ya maombi na sala za usiku.
mwanafunzi huyo anasema kuwa, hakuripoti tukio hilo kwa wakati huo kutokana na woga.
“Lakini baadaye shakhsia (personality) yangu ilibadilika sana kiasi ambacho waalimu waliniambia kuwa nilikuwa na mfadhaiko mkubwa. O’brien alipopandishwa cheo na kuwa askofu sikuwa na jinsi ila kujiuzulu. Nikajua kwamba daima atakuwa na madaraka juu yangu na kuninyanyasa. Watu walidhani kuwa niliachana na ukasisi ili nikaoe. Sikuondoka kwa sababu hiyo, bali niliondoka kwa sababu ya kulinda utu na ukamilifu wangu”, alisema.
katika taarifa ya pili, “Kasisi A” anaeleza kuwa aliishi kwa furaha ndani ya parokia na alipotembelewa na O’brien mahusiano yasiyofaa baina yao yalitokea.
Katika taarifa ya tatu, “Kasisi B” anadai kuwa alianza utumishi wake miaka ya 1980 ambapo alipewa mwaliko wa wiki moja “kwenda kufahamiana” na O’brien kwenye makazi ya askofu. Anadai kwamba ndipo alipojikuta ameingia katika kufanyiwa kile alichokiita kuwa tabia isiyofaa na kadinali huyo pindi wanapomaliza kupata vinywaji wakati wa usiku.
"Kasisi C" alikuwa kasisi kijana ambaye kadinali alikuwa akimpa ushauri nasaha kuhusu matatizo yake binafsi. Kasisi C anadai kuwa O'Brien alitumia muda wa maombi ya usiku kama sababu ya kumfanyia mambo yasiyofaa.
Wanaamini kuwa kadinali alitumia vibaya madaraka yake. “Unatakiwa kuelewa uhusiano uliopo kati ya askofu na kasisi. Unapowekwa wakfu unakula kiapo cha kumtii”, anasema kasisi huyo wa zamani.
"Anakuwa zaidi ya bosi wako, zaidi ya mkurogenzi wa kampuni yako. Ana mamlaka makubwa juu yako. Anaweza kukuhamisha, kukutoa, kukuingiza…anadhibiti na kutawala kila kipengele cha maisha yako. Huwezi kumkatalia na kumuasi hivi hivi.”
Kiongozi mkuu wa kanisa katoliki nchini Uingereza hivi karibuni alisema kwamba anaamini makasisi wanatakiwa kuruhusiwa kuoa kama wakitaka kufanya hivyo. Kadinali O'Brien anasema ni wazi kuwa makasisi wengi wanapata shida sana kuukabili useja, na wanatakiwa waruhusiwe kuoa na kuwa na watoto.
KWA HISANI YA: The Guardian.
No comments:
Post a Comment