#WAIOMBA SERIKALI KUTIA MIGUU MISIKITINI,
#WANA SUKUMWA NA NANI KUFANYA HAYA.
#WAISLAMU WASEMA HAYO AYASEMEE NDANI YA MISIKITI SIYO MAGAZETINI.
SOMA HABARI HII KAMA ALIVYONUKULIWA NA GAZETI MOJA.
MWENYEKITI wa Taasisi ya Kiislamu ya Imamu Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis, amedai kuwa baadhi ya misikiti imegeuzwa ya kujifunzia kareti na kuhamasisha vurugu nchini na kusisitiza kuwa Uislamu usigeuzwe dini ya wahuni.
waislamu walivyojaribukwenda ikulu kutaka haki ya kusikilizwa. |
Pia amewataka Waislamu kutojihusisha na kundi la Kiislamu ambalo kwa linadaiwa kuongozwa na kiongozi mmoja wa dini hiyo (jina linahifadhiwa), kwani linatumia misikiti kuwa vituo vya kufanya mikutano na hotuba za kuwahamasisha kufanya vurugu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Sheikh Khamis, alisema Taasisi yake inalaani vikali vitendo vya kikundi kinachoeneza vipeperushi vya kuchochea chuki baina ya Waislamu na Wakristo au Serikali na Waislamu.
Sheikh Khamis alidai kuwa kundi hilo linahamasisha wafuasi wake ambao ni wachache kufanya ghasia kila Ijumaa au siku ambayo kesi ya Katibu wa Taasisi na Jumuia za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda inaposikilizwa.
”Tunawataka Waislamu wafahamu kuwa hakuna mahali Uislamu unafundisha kujichukulia sheria mikononi, kupuuza na kutoheshimu mamlaka ya dola na vyombo vya sheria.
“Kujitumbukiza katika maandamano ya kuishinikiza Serikali, Mahakama au Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kumwachia kwa dhamana Sheikh Ponda… hicho ni kitendo cha kijinga kwani ni kinyume cha taratibu za kisheria zilizowekwa katika kumpatia mtuhumiwa dhamana,” alidai Sheikh Khamis.
Sheikh Khamis aliwatahadharisha Waislamu wanaoishi Dar es Salaam kujiweka mbali na kikundi hicho ambacho kinawatumia vijana wasiojua kitu kwa ajili maslaha yake binafsi na kwamba kinawachafua na kuwatia aibu.
Pia alidai kundi hilo linaonesha kuwa Uislamu ni dini ya wahuni, watu wa fujo, wasiofuata na kuheshimu taratibu wala sheria za nchi na kusisitiza kuwa, Serikali inatakiwa kuchukua hatua za haraka ili kukabiliana na hali hiyo.
“Wanataka kuwafanya Waislamu waonekane watu ambao hawajali uhuru wa watu wengine, watu ambao wanasababisha nchi yao kukosa amani na utulivu, wakati zote hizo hakuna hata sifa moja anayostahili kuwa nayo Mwislamu,” alisema Sheikh Khamis.
Pamoja na mambo mengine, Sheikh Khamis aliishauri Serikali na vyombo vyake kuacha kufumbia macho matendo maovu na ya kuvunja sheria za nchi yanayofanywa na baadhi ya watu kwa kisingizio cha dini.
“Serikali inatambua kwa muda mrefu kuwepo kwa kikundi hiki ambacho kimekuwa kikiendesha operesheni za kuteka misikiti ambayo inaendeshwa na bodi za wadhamini waliosajiliwa kihalali kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Wamekuwa na jeuri ya kupinga hata amri zilizotolewa na Mahakama huku vyombo vya dola vikishuhudia, hatua ambayo imekifanya kidhani kipo juu ya sheria. Tunaiomba Serikali itumie uwezo na dhamira yake ya kudumisha amani iliyopo nchini,” alisema.
Wakati huo huo, Sheikh Khamis alisema taasisi hiyo imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kuuawa kwa viongozi wa dini mkoani Mwanza na kuuawa kwa Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki aliyepigwa risasi na watu wasiofahamika Februari 17, visiwani Zanzibar.
“Wakati umefika sasa wa kutafakari na kuangalia hatua za kuchukua kwa haraka kunusuru taifa kuingia katika dimbwi la umwagaji damu wenye misingi ya chuki za kidini. Vitendo vyote hivyo vinaashiria kuwepo kwa kikundi cha watu wachache ambao wamechoka kuishi kwa amani,” alisema.
Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete amekemea vikali mapigano ya kidini yaliyotokea mkoani Geita na kusababisha kifo cha Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God, Mathayo Kachila (45), huku watu kadhaa wakijeruhiwa na kusema vita ya kidini haina mshindi.
Alisema katika masuala ya udini watu wanapaswa kuvumliana ili nchi iendelee kuwa ya amani na utulivu uliopo kwa miaka 50 sasa. “Tuvumiliane kwani ni jambo la fedheha sana kwa mapigano yaliyotokea dhidi ya Waislamu na Wakristo, haijawahi kutokea tangu Uhuru,” alisema Rais.
Rais Kikwete aliwataka viongozi wa dini kushughulikia masuala ya kiimani kwa kuwaagiza waumini wao kutenda mema.
“Viongozi we dini ni watu muhimu sana, tena mnaaminiwa sana na waumini wenu, chochote mtakachozungumza ndicho watakachofanya msizungumze masuala ya uchochezi na Serikali kazi yake ni kulinda amani na kutafuta wachochezi wanaoharibu amani iliyopo nchini,” alisema.
Alisema mapigano hayo hayana tija kwa pande zote, hivyo kwa dini zote hakuna sababu ya kuendeleza vita ambayo haina mshindi.
“Muhimu yasitokee tena kwani hayana tija kwa mtu yeyote, lakini vita vya kidini haina mshindi, isipokuwa kila mmoja atataka kumfanyia mwenzake jambo baya.
“Tuishi kama tulivyokuwa tukiheshimiana kidini, dhehebu baina ya dhehebu, dini baina ya dini na wale wasiofungamana , tumeishi kwa miaka 50, tusiharibikiwe sasa,” alisema na kuwataka Watanzania kukataa ushawishi wa mambo yanayosabaisha kuhatarisha amani.
Wakati huo huo, Sikitiko Phillip anaripoti kutoka Kagera kuwa, viongozi wa dini wana jukumu kubwa la kulinda, kusimamia amani na kuzuia waumini wao kuepukana na chokochoko zinazoanza kuondoa amani na utulivu nchini.
Rai hiyo ilitolewa jana na Shehe wa Wilaya ya Bukoba, Alhaji Haruna Kichwabuta wakati akizungumza na waandisi wa habari katika ofisi za Bakwata mjini hapa kuhusiana na matukio na mauaji yanayotokea nchini kutokana na imani za kidini.
”Pamoja na jukumu la viongozi kuonesha nia ya kudumisha amani na uvumulivu nchini, lakini viashiria vinaonesha kuwa watu wanachezea amani na kushindwa kuvumiliana,” alisema.
Alisema matukio kadhaa yanaashiria kuvunjika kwa amani na uvumilivu. Viashiria hivyo vinaonekana kuanzia katika ngazi za kiasiasa kwa baadhi ya wafuasi wa vyama fulani vya siasa kuona wengine hawafai.
Viashiaria vingine alivitaja kuwa ni mauaji wa albino na vikongwe, kuchinja watu na kuondoka na vichwa vyao huku viwiliwili vikitelekezwa. Hali kadhalika mapigano ya wakulima na wafugaji yanasababisha uharibifu wa miundombinu na vifo ni ishara ya kushindwa kuvumiliana.
Alisema kutokana na mfululizo mwa matukio hayo, kwa sasa yameibukia katika dini, ambapo wana dini nao uzalendo umewashinda na kuanza mapigano hadi kufikia mauaji na kujeruhiana na kuharibu mali.
Sheikh huyo alisema kundi hilo ndilo moyo wa Watanzania na kwamba likiharibika kila kitu kinaharibika. Alisema Watanzania hawatakiwi kuikufuru neema waliojaliwa ya kuwa kisiwa cha amani na kwa sasa kiwe kisiwa cha hofu na njaa. Alisema Watanzania wanatakiwa kutakafari kama kweli wamechoka kuitwa wananchi na waitwe wakimbizi, na hivyo kutoa mwito kuacha kuhojiana kuhusu nani afanye hivi au vile.
”Tumekuwa na utamaduni wa kuvumiliana kwa muda mrefu kabla na baada ya Uhuru, tumekuwa na tabia ya kuheshimu mila na desturi na imani ya kila mtu, hebu angalieni tunavyoheshimu sikukuu za kidini, kama ni siku za Kikristu, Waislamu wanapumzika bila kuhoji vivyo hivyo kwa Wakristu bila kujali ni hasara gani za kiuchumi, mtu au taifa itazipoteza kutokana na ofisi kutofanya kazi …hivi ndivyo tulivyozoea,” alisema.
No comments:
Post a Comment