SHEKH PONDA ISSA PONDA AKIWA MAHAKAMANI, |
WANAWAKE WAO HAWAKUWA NYUMA. |
ULINZI MKALI NAO ULISHUHUDIWA KUULIDA MSAFARA WA SHEKH PONDA |
Hadi jana upande wa jamhuri ulikuwa umeleta mashahidi 17 na vielelezo 13 ambavyo vilipokelewa mahakamani. Baada ya wakili Kweka kutoa maelezo hayo wakili wa Ponda, Juma Nassor, aliomba mahakama iwapatie muda
hadi Machi 4 ili wakajiandae kuwasilisha maombi ya wateja wao 49 kuwa hawana kesi ya kujibu.
Hata hivyo Hakimu Nongwa alisema jukumu la kupanga tarehe ya kufanya majumuisho ni vyema ikaachiwa mahakama na hakimu huyo akatoa amri kuwa majumuisho hayo yatafanyika kesho, Februali 27 na akautaka upande wa utetezi uwe wa kwanza kuwasilisha majumuisho yao kwa njia ya mdomo. Kabla ya jamhuri kufunga maelezo yake mahakama ilisikiliza mashahidi watatu ambao ni shahidi wa 15, F3929 D/C , Constebo Eliaeli (35), shahidi wa 16 Sajenti Amos wa kituo cha polisi Kati na shahidi wa 17 askari mpelelezi Na. F8586 D/C Ismail.
Shahidi wa 17, D/C Ismail aliieleza mahakama kuwa Oktoba 17, mwaka jana, alipewa kazi na mkuu wake wa kazi na kati ya saa 2-9 alasiri alikuwa kituo cha polisi Kijinyoma akiwahoji washtakiwa ambao walikamatwa katika kiwanja cha Chang’ombe Marskas wakikabiliwa na makosa ya kuingia kwa jinai katika kiwanja hicho.
Ismail alidai kumhoji mshtakiwa Fiswaa ambaye alimweleza kuwa kati ya tarehe, mwezi na saa isiyofahamika akiwa nyumbani kwake Mlandazi, mkoani Pwani, akiwa anasikiliza Redio Iman, alisikia tangazo lililokuwa likiwataka waumini wa dini ya Kiislamu kwenda kuongeza nguvu ya kujenga msikiti katika kiwanja kilichovamiwa cha Chang’ombe Markas ambacho ni mali ya Waislamu na si BAKWATA.
Shahidi huyo alidai kuwa mshtakiwa huyo alimweleza kuwa aliitikia wito huo na kufunga safari toka Mlandizi kuja kuungana na wenzake ambapo kiongozi wao walipokuwa kwenye kiwanja hicho ni mshtakiwa wa kwanza ambaye ni Ponda.
“Sululu, mapanga vilitumika kama vifaa vya kujengea msikiti wa muda katika kiwanja hicho na ndipo usiku wa kuamkia Oktoba 17, mwaka jana, tukiwa tumekaa kwenye kiwanja hicho nikasikia sauti ikisema, tupande kwenye gari na sikuwa na kumbukumbuku yoyote,” alidai Ismail.
Maelezo ya mshtakiwa huyo yalipokelewa kama kilelezo cha 13 na hakikupingwa na mawakili wa utetezi. Shahidi wa 16, Station Sajenti Amos, alidai kuwa Oktoba 17 mwaka jana alipewa jukumu la kumhoji mshtakiwa Hussein Ally ambaye alimweleza kuwa alipokea maelekezo kutoka kwa masheikh wake wa msikiti wa Kinyerezi yakimtaka afike katika kiwanja cha Markas na alienda na kukutana na wenzake ambapo walianza kufanya kazi wakiongozwa na Ponda katika kiwanja ambacho tayari mashahidi wengine toka BAKWATA walisema ni mali ya kampuni ya Agritanza Ltd siyo BAKWATA tena.
Aidha shahidi wa 15 D/C Konstebo Elieli alidai kuwa Oktoba 17, mwaka jana, alipewa jukumu na mkubwa wake wa kazi la kuandika maelezo ya mshtakiwa Mohamed Ramadhan ambaye alimweleza kuwa siku hiyo yeye alikwenda kusali katika eneo la kiwanja hicho akitoka Oysterbay Dar es Salaam.
Elieli alieleza kuwa mshtakiwa huyo alimweleza kuwa alikwenda kusali swala ya alfajiri hapo Chang’ombe Markas kwa sababu alikuwa anauguliwa na ndugu yake anayeishi Keko ambapo hakwenda kusali misikiti ya Keko kwa vile hali ya usalama ilikuwa mbaya.
“Mshtakiwa akanieleza eti baada ya kusali hapo alfajiri ya Oktoba 17, mwaka jana, ndiyo ghafla alishtukia anakamatwa na polisi. Nilipomhoji kama analifahamu vuguvugu la Waislamu kudai haki zao, mshtakiwa alikubali na kwamba pale alikuwa katika kutetea na kudai haki yao ya kurejeshewa kiwanja kile ambacho ni mali ya Waislamu na si BAKWATA,” alidai Elieli. Hata hivyo mahakama ilikataa kupokea maelezo hayo kama kielelezo kwa sababu ya dosari nyingi za kisheria.
No comments:
Post a Comment