Friday, March 8, 2013

BUGANDO yahofia kulipuliwa, ulinzi mzito waimarishwa zaidi

Hospitali ya Rufaa ya Bugando umeimarisha ulinzi kwa watu wanaoingia hospitalini hapo kwa shughuli mbalimbali na hasa kuona wagonjwa, tumeshuhudia.
hospitali ya rufaa bugando
Msingi wa uamuzi huo unadaiwa kuwa ni mwitikio wa taarifa za vitisho zinazotolewa na baadhi ya watu kuhusu hali ya utulivu jijini Mwanza na hasa katika taasisi kubwa za kidini bila kujali ni zenye manufaa zaidi kwa Watanzania wote.Hali hiyo ya kukagua wanaoingia hospitalini hapo ni tofauti na ilivyokuwa awali ambapo wagonjwa walikuwa wakiingia tu bila kufanyiwa ukaguzi wowote ukichilia mbali ukaguzi wa mabegi na mikoba wakati wa kutoka.
Kwa sasa utaratibu umekuwa ni kukaguliwa kwa mtambo maalumu wa kugundua vifaa vya chuma na kielectroniki ili kujihami na aina ya wageni wenye dhamira mbaya.

Vyanzo kadhaa vya habari  vimeeleza ya kwamba hatua hiyo imetokana na matukio kadhaa yasiyo ya kawaida, kwa mfano, kutumwa kwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi kuelezea tishio la kulipuliwa kwa hospitali hiyo.
Ujumbe huo unadaiwa kutumwa kwa baadhi ya viongozi wa Hospitali ya Rufaa Bugando, na hivyo viongozi hao kuzipa uzito taarifa hizo kwa njia ya kuimarisha ulinzi.
Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk.Charles Mjinge, amemweleza mmoja wa waandishi wetu ya kwamba, ingawa utawala wa hospitali haujabaini sababu hasa za kwa nini mtu aamue kulipua sehemu kama hospitali ambako wanalazwa na kutibiwa watu wa aina zote, wameamua kujihadhari kwa sababu suala la usalama si jambo la kupuuza.
“Tumekuwa tukipokea sms (ujumbe mfupi wa simu) kuhusu njama za watu kuja kulipua Hospitali kwa gesi, katika hali ya kawaida ilikuwa ni lazima kuchukua hatua kuimarsiha ulinzi kama hatua za kawaida tu, ingawa kwa kweli hatuoni sababu kwa nini mtu aje alipue hospitali,” alieleza Dk. Majinge
Pamoja na ujumbe huo mfupi kumekuwa na matukio kadhaa ya watu kutembelea hospitalini hapo katika hali inayotia shaka, ikiwamo taarifa ya watu wanaosadikiwa kuwa na asili ya kiarabu kwenda kwenye maeneo wanayoishi Mapdri wanaofanyakazi katika Chuo Kikuu cha Bugando na hospitalini hapo yaliyo karibu na hospitali hiyo. Wageni hao wanadaiwa kufika hapo na kuulizia nyumba wanayoishi (mapadri) bila kuwa na sababu za msingi za kutaka kujua na hata kutaja la padre wanayemtafuta.
Inaelezwa kuwa hali ilianza kuwa ya shaka katika hospitali hiyo baada ya majeruhi wa matukio ya vurugu zilizotokea kijijini Buseresere, mkoani Geita kupelekwa kulazwa katika hospitali hiyo ambapo baadhi ya wageni walioanza kujitokeza kutembelea wagomjwa walikuwa wakitiliwa shaka na wengine wakikutwa na vitu kama nondo hali ambayo iliashiria mahitaji ya kuimarisha ulinzi.
“Ni kweli baada ya majeruhi hao kuletwa hapa walinzi wetu walianza kuona wageni ambao walikuwa wanatiliwa shaka, kuna wengine walikamatwa na nondo, sasa suala kama hilo si la kawaida sana kwa mtu anayekuja hospitalini kutibiwa au kusalimia wagonjwa, tukadhani ni muhimu kwa usalama wa wagonjwa wetu tuimarishe ulinzi,” anasema.
kaa chonjo ilitaka kujua kutoka kwake kama hali hiyo maana yake ni kuwa Hospitali ya Bugando sasa iko hatarini na nini ushauri wake kwa wagonjwa, ndugu na jamaa za wagonjwa ambao ni lazima waende hospitalini hapo kwa huduma.
“Kwanza niwahakikishie wananchi kuwa sisi tunatibu raia wa aina zote, mwongozo wetu ni kumtibu mgonjwa bila kujali mambo mengine ya imani yake, kabila au chochote kile, kwetu mgonjwa ni mgonjwa. Kuhusu usalama wa hospitali hii, tuko salama hizi ni hatua za kawaida tu za kuimarisha ulinzi, wala watu wasiogope au kuhofia chochote hakuna hatari ya kiwango hicho, ni hatua za kuimarisha ulinzi tu, watu wasiwe na wasiwasi” alifafanua Mkurugenzi huyo.
Uhakika wa usalama katika hospitali hiyo unaungwa mkono na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, ambaye alisema kama ni suala la ulinzi kuimarishwa hospitalini hapo ni katika hatua za kawaida tu.
“Wanachukua hatua za kawaida tu kiulinzi na sisi tunawasiliana na kushirikiana nao kama kutakuwa na lolote litakalohitaji nguvu ya polisi, tuko imara si kwa Bugando tu lakini pia maeneo yote tumeimairsha ulinzi na hatuna wasiwasi na hilo,” alieleza Kamanda Mangu.
Taharuki kwa wananchi
Baadhi ya wananchi waliozungumza na waandishi wetu wameeleza jinsi walivyoshitushwa na hatua hiyo kwa kuwa kwa upande wao si ya kawaida.
“Ni kweli hili si jambo la kawaida tumezoea kwenda Bugando na kuingia tu, sasa yakianza masuala ya namna hii ni lazima mtu uogope, lakini pia kulikuwa na usumbufu mkubwa mwanzoni watu wengine wanakwenda kwa pamoja na vifaa vya kukagua ni vichache, tulipata usumbufu kweli, lakini sasa hivi naona usumbufu umepungua,” alisema Halima Jamal, Mkazi wa Igogo jijini Mwanza.
Hassan Fungamoyo alipozungumza na nasi alisema hatua hizi ni muhimu kuchukuliwa kwenye mazingira ya namna hii ambayo watu wanachukua hatua mkononi kutaka kuvuruga amani ya nchi, lakini hofu yake si usumbufu wa kuingia hospitalini hapo pekee.
“Mimi sina shida na hatua hii, hofu yangu kubwa ni kilichosababisha kuwapo hali hii, unaweza kuliona dogo lakini ni dalili za kuashiria Tanzania tunayoijua ya udugu na amani inaondoka, ukiona hatua hizi zinachukuliwa ujue ni ishara isiyo njema, wao ni lazima wachukue hatua hizi kwa usalama wetu tunaoingia humu lakini wale wakubwa wetu wa serikali wanatakiwa wajue hapa tulipofika siyo Tanzania, haya tuliyazoea huko nchi nyingine si yetu kabisa,” alisema.

No comments:

Post a Comment