SAUDI Arabia iko tayari kutoa fursa maalumu kwa walimu wa Zanzibar kupata taaluma zaidi ya elimu ya dini ya Kiislamu na lugha ya Kiarabu nchini humo kwa lengo la kuwajengea uwezo wa ufundishaji.
Balozi Hani Mominah ambaye alikwenda kwa Balozi Seif kumuaga rasmi baada ya kumaliza utumishi wake nchini alisema fursa hizo zitahusisha mafunzo kati ya vipindi vya miezi minne hadi mwaka mmoja.
Alisema cha msingi na kuzingatiwa zaidi ni suala la mawasiliano kati ya pande hizo mbili ili kuandaliwa utaratibu wa mfumo wa kuitumia vyema fursa hiyo muhimu.
“Sioni kama kuna vikwazo vyovyote katika suala hili kwani hivi sasa tayari wapo wanafunzi wapatao 40 wa Tanzania wanaopata mafunzo ya dini na lugha ya Kiarabu Nchini Saudi Arabia katika vyuo vikuu tofauti,” alifafanua Balozi Hani Mominah.
Akizungumzia ibada kubwa ya Hijja inayofanyika Macca nchini humo, Balozi Hani alisema serikali ya nchi hiyo inajitahidi kuimarisha miundombinu ya kisasa katika kuwahakikishia waumini wa dini ya Kiislamu ulimwenguni wanakwenda kutekeleza ibada yao ya hija kwa utaratibu muafaka.
Akitoa shukrani zake, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, aliipongeza Saudi Arabia kwa hatua yake ya kusaidia maendeleo ya Zanzibar katika sekta ya elimu na dini.
Alisema Saudi Arabia imekuwa ikiiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kupitia mfuko wake wa misaada ya kimataifa, Saud Fund, ambao umewezesha kunyanyua kiwango cha elimu ya dini ya Kiislamu nchini.
No comments:
Post a Comment