SHAHIDI wa 13 upande wa utetezi katika kesi inayomkabili Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Ponda Issa Ponda na wenzake amedai aliamini walioingia ndani ya Msikiti wa Markaz Chang’ombe kuwakamata walikuwa wahuni na si polisi kwa sababu walilewa na walitukana matusi ya nguoni.
Hayo yalidaiwa jana na shahidi huyo, Rahma Hamza, ambaye ni mshitakiwa katika kesi hiyo wakati akijitetea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa.
“Nilikamatwa nikiwa nasali, nikasukumwa nikaamua kunyoosha mikono juu nikiashiria najisalimisha, nikashitukia nimepigwa rungu la mkono, nikaanza kutoa shahada kwa sababu niliona mauti yako mbele yangu.
“Nilihisi hakuna uzima, nikasikia naambiwa mwite huyo Allah wako akusaidie, polisi akanisukuma huku akitoa matusi makubwa ambayo siwezi kuyarudia hapa, sikuamini kama walikuwa polisi, kilichonifanya nihisi polisi ni sare walizokuwa wamevaa.
“Askari polisi aliyekuwa akinisemesha alikuwa anatoa harufu ya pombe katika kinywa chake, aliponifikisha nje nikakuta ndani ya gari la polisi kuna vijana wawili wamelala, akanilazimisha niwalalie, niliposita nikashitukia nimepigwa rungu, niliwalalalia vijana wale,” alidai Rahma.
Shahidi huyo, alidai analitambua Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kama taasisi inayoshughulikia masuala ya migogoro ya ndoa na kutangaza mwezi unapoandama.
No comments:
Post a Comment