mchezo ulianzia hapa ! |
KAULI ya
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali
Pengo, kwamba serikali imezembea kutekeleza wajibu wake, uzembe ambao moja ya
matokeo yake ni kuuawa kwa risasi kwa Padri wa kanisa hilo, Evaristus Mushi,
imezua mgongano wa kimjadala miongoni mwa maofisa waandamizi serikalini, Kaa
chonjo, imeelezwa.
Kwa
mujibu wa vyanzo kadhaa vya habari, baadhi ya maofisa waandamizi
wamelazimika kujadili kauli hiyo, sambamba na kupima athari au faida zake
katika operesheni inayoendelea ya kuwasaka wahusika wa tukio hilo.
Hatua ya
maofisa hao imetokea saa kadhaa baada ya Pengo kuzungumza na vyombo vya habari
na Kaa chonjo ikielezwa ya kwamba, mabishano yamejitokeza miongoni mwa
maofisa hao.
“Imebainika
kuna baadhi ya taarifa ambazo hazikuwa zinafikishwa katika eneo husika, wakubwa
(maofisa waandamizi wa masuala ya usalama) wamelumbana. Wengine inadaiwa
walikuwa wakifikishiwa taarifa za dalili mbaya lakini hawakuwa wepesi kuchukua
hatua, ni kama vile wamelewa kuendelea kufanya kazi katika nchi iliyojaa amani
kila siku,” kilieleza chanzo chetu cha habari.
Katika
mazungumzo yake na waandishi wa habari kuhusu tukio la kuuawa kwa Padri
Evaristus Mushi wa Parokia ya Mtakatifu Joseph ya Mjini Magharibi, Unguja,
Zanzibar, Pengo alitoa maelezo yanayotilia shaka kwamba mauaji hayo yana mkono
wa baadhi ya watu wanaojitambulisha kwa jina la Kundi la Kidini la Uamsho.
Kwenye
mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Pengo alisema; “Tunahitaji
rehema (za Mwenyezi Mungu) ili tuendelee kuwapo. Tunahitaji utulivu na
kuelezana ukweli. Na endapo mmoja wetu atazembea, ni jukumu kuambiana kwamba
hapo umezembea na utalifikisha Taifa pabaya.”
Kwa
mujibu wa maelezo hayo ya Pengo, wauaji hao walipanga na kutekeleza unyama wao
huo kutokana na uzembe na udhaifu wa vyombo vya dola kwa kushindwa kusoma alama
za nyakati, kwa kuwa tayari wauaji hao walikwishasambaza vipeperushi
vilivyoashiria dhamira hiyo mapema.
“Watu
wanasema kikundi cha Uamsho kule Zanzibar ni kikundi cha kidini, lakini kinatoa
vipeperushi kama hiki (alikionyesha kwa waandishi) ambacho kimenifikia mkononi.
Kwa hiyo, ni wazi kuwa hadi kinifikie mimi, Watanzania wengi watakuwa
wamefikiwa na kipeperushi hicho…inathibitisha kwamba vipeperushi hivi ni vya
Uamsho, lakini si kazi yangu kuhakikisha (kuthibitisha) tamko la Uamsho ni la
Uislamu, siamini kwamba vyombo vya usalama vya taifa letu vinaweza kusema
havina habari,” alieleza Pengo.
Maziko ya
Padri Mushi
Padiri
Mushi aliyeuawa kwa kupigwa risasi Jumapili iliyopita asubuhi wakati akishuka
kutoka kwenye gari lake ili kwenda kuongoza ibada katika Kanisa la Betras,
lililopo Minara Miwili, Mji Mkongwe, Unguja, anazikwa Jumatano wiki hii
Visiwani humo.
Mazishi
hayo yanafanyika jioni ya Jumatano hii katika Kijiji cha Kitope, Kaskazini B,
Unguja yakiongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,
Eusebius Nzingilwa.
Lakini
kabla ya muda wa ibada hiyo ya mazishi, Kardinali Pengo ataongoza misa ya
kumwombea marehemu pamoja na kuliombea Taifa itakayofanyika katika Kanisa Kuu
Katoliki la Mtakatifu Joseph, jijini Dar es Salaam.
Masikitiko
ya Rais Kikwete
Tayari
Rais Jakaya Kikwete kupitia kwa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jijini Dar es
Salaam, ameeleza kusikitishwa na tukio hilo na kuahidi serikali yake kuwasaka
wote wanaohusika na kuwachukulia hatua za kisheria.
Hata
hivyo, kauli hiyo ya Kikwete kupitia kwa Kurugenzi hiyo inatajwa na duru za
baadhi ya viongozi wa dini nchini kuwa ni ya kawaida na imeanza kuzoeleka.
Viongozi hao wanarejea ahadi yake aliyoitoa wakati Padri Ambrose Mkenda
aliponusurika kuuawa huko Zanzibar, wakati wa Sikukuu ya Krismasi mwaka jana,
na kuishia kujeruhiwa.
Lakini si
padri huyo pekee aliyenusurika kuuawa bali vitendo vya kudhuru baadhi ya
viongozi wa dini nchini pia vimemfika Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, ambaye ni
Katibu wa Mufti Zanzibar, ambaye alimwagiwa tindikali.
Hata
hivyo, katika hatua nyingine tayari Serikali ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali
Mohammed Shein, nayo kama ilivyo kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, imeahidi
kuwasaka wahusika na kuwachukulia hatua.
Makanisa
zaidi yacharuka
Hali
imezidi kuwa tete ikiibua kauli na matamko mbalimbali ya viongozi wa dini
nchini.
Jukwaa la
Wakristo mkoani Mbeya ambalo linaundwa na mabaraza makuu matatu ya madhehebu ya
kikristo; Tanzania Episcopal Council (TEC), Christian Council of Tanzania (CCT)
na Pentecostal Council of Tanzania (PCT), limeitahadharisha serikali juu ya
kile walichokiita undumilakuwili na tabia yake kulichukulia suala la mauaji ya
viongozi wa dini ya Kikristo kama jambo la mazoea.
Jukwaa
hilo, limesema katika tamko lake la wiki hii kwamba ili Serikali ya Rais
Kikwete iweze kuaminika mbele ya macho ya waamini wa dini hiyo, lazima ionyeshe
usawa katika sakata la mauaji ya Mchungaji Mathayo Kachila wa Buseresere,
mkoani Geita na Padri Mushi wa Zanzibar.
“Miongoni
mwa harakati hatarishi zinazosambazwa kwa njia ya CD na DVD ni za Sheikh
(Hussein) Ilunga kuhusu kuuawa wachungaji, mapadri na maaskofu. CD na DVD
zimeanza kuwa na matokeo mabaya kwani Padri (Ambrose) kule Zanzibar alipigwa
risasi na watu walioitwa na Serikali wahuni, na sasa vifo vimetokea.
“Mchungaji
Mathayo Kachila kule Buseresere mkoani Geita ameuawa na kikundi kinachodhaniwa
ni wanaharakati wa kidini wenye jazba na ghadhabu kali inayotokana na mvutano
uliopo kuhusu nani mwenye haki ya kuchinja wanyama, na juzi Padri Mushi wa
Kanisa Katoliki kule Zanzibar,” alisema Askofu Damianus Kongoro wakati akisoma
tamko la Jukwaa hilo mbele ya wandishi wa habari jijini Mbeya.
Mauaji
kwingineko duniani
Mauaji ya
mapdri yamewahi kutokea katika maeneo tofauti duniani na kati ya nchi ambako
mauaji hayo yamepata kutokea ni Colombia.
Katika
Jiji la Bogotá, Colombia, Kardinali Ruben Salazar aliwahi kuja juu dhidi ya
mauaji ya Padri Luis Alfredo Suarez Salazar (50), akisema aliyeuawa hakuwa na
hatia yoyote na wajibu wake ulikuwa ni mwema kwa jamii iliyokuwa ikimzunguka..
Padri
huyo aliauwa kwa kupigwa risasi na watu wawili ambao baada ya tukio hilo
walitoroka kwa kutumia pikipiki. Aliuawa wakati akimsaidia dada yake kupakia
mizigo katika gari. Dereva wa padri huyo, Hernan Torres Ramos, naye alijeruhiwa
vibaya.
Kutokana
na tukio hilo, familia ya Padri Suarez ilieleza ya kwamba padri huyo hakuwa na
kisasi na mtu yeyote na walishangazwa na mauji hayo, hali ambayo pia inafanana
na maelezo ya wanafamilia wa Padri Mushi ambao kupitia kwa Aloyce Mushi
aliyezungumza na mwandishi wetu anaeleza padri huyo naye hakuwa na kisasi na
mtu au kundi lolote.
Mwanza
balaa tupu
Kutoka
mkoani Mwanza na Geita, Mwandishi Wetu anaripoti ya kwanza sakata la nani
mwenye haki ya kuchinja wanyama katika Kijiji cha Buseresere-Geita, ambako
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikwenda kutafuta suluhu, bado halijapata suluhisho.
Moja ya
mambo yaliyoshuhudiwa na Waziri Mkuu Pinda katika ziara yake hiyo ni kuibuka
kwa madai mapya ya kusambazwa biblia feki ambazo inadaiwa zinatumiwa na baadhi
ya kundi lililoko kwenye mvutano huo kuthibitisha madai ya nani hasa mwenye
mamlaka ya kuchinja kwa mujibu wa vitabu vyote vitakatifu vya Quraan na Biblia.
Katika
kikao cha usuluhishi na Waziri Mkuu jijini Mwanza, inadaiwa ya kwamba Sheikh
Issa Kalenga akiwa mmoja wa wajumbe wa mkutano huo alikuwa na biblia ambayo
kwenye tafsiri ya maneno magumu imelieleza eneo kibudu kuwa ni mnyama
aliyejifia mwenyewe au ambaye hakuchinjwa kwa mujibu wa taratibu za dini ya Kiislamu.
Taarifa
zinaeleza kuwa biblia hiyo iliibua mjadala mzito kwa wachungaji kutoitambua na
kumpelekea biblia nyingine tatu (Pinda) ili kuwaonyesha tafsiri hiyo lakini
zikawa zimetofautiana.
Baada ya
mkutano huo Shekh Kalenga waliowanyesha waandishi wa habari kipengele cha
ufafanuzi huo na kusisitiza kuwa mkristu haruhusiwi kula kibudu na hivyo ni
halali kula vilivyochinjwa na Waislamu.
Hata
hivyo hoja hiyo ilipingwa na Askofu Augustine Mpemba wa Kanisa la TFE kwa
Neema, ambaye alisema kuwa kuna watu wenye pesa ambao wamekuwa wakichapisha
biblia zisizoendana na mafundisho ya Kikristo ili kuchakachua imani yao.
Alieleza
kuwa katika ulimwengu wa leo kuna biblia nyingi sana wasizokubaliana nazo
Wakristo, akitoka mfano wa Biblia ya John Hagee ambaye ni mwanzilishi wa
Cornerstone Church, ambayo haikubaliki na Wakristu wengine kwa kuwa watu
wanachapisha biblia hizo kwa maslahi, na kuwatahadharisha waumini wao kutonunua
bila mitaani kwa kuwa ziko nyingi zilizochakachuliwa.
Lakini
akizungumzia hali ya vurugu za kidini, mmoja wa wanazuoni wa Kiislamu alisema
kwa jinsi matukio yalivyotokea (vurugu za uchinjaji na mauaji ya padri
Zanzibar) inaashiria kuwa kuna watu mahali fulani ambao dhamira yao ni kuona
Tanzania inaingia kwenye machafuko ili wao watimize malengo yao.
"
Hii haiwezi kuwa imetokea kwa nasibu tu, kwamba Waziri Mkuu ana ratiba ya
kukutana na viongozi wa dini zote halafu mtu anakwenda kumpiga risasi padri
hadharani akijua wako waumini wanamsubiri kuwasuluhisha, huyu alidhamiria
kutengeneza mshindo ambao utafanya mazungumzo yawe magumu," alieleza.
Alipoulizwa
anadhani kuwa watu hao wanaweza kuwa nani na wanafanya hayo kwa manufaa gani
alijibu; "Kwanza karibu asilimia kubwa ya biashara sasa zimeshikwa na
bidhaa kutoka China, na hii ni kwa dunia nzima, mataifa makubwa ya Magharibi
yamebakiza biashara ya maana ni silaha tu, wanaweza kuwa wanatafuta hilo soko
Tanzania ambako kila kona imejaa dhahabu, gesi au mafuta na hivi vyote ni
vivutio vya mataifa makubwa na China ndiyo wanaongeza ushawishi wao kwetu, mataifa
makubwa yangependa kuona tunafarakana ili wapate fursa ya kunufaika
kirahisi."
No comments:
Post a Comment