Saturday, March 2, 2013

mapadri wapata taharuki. mmoja adai anataka kutekwa !

PADRI wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza, Alfonce Twimann’ye mwishoni mwa wiki alilazimika kujificha katika nyumba ya watu baada ya kukimbizwa na watu wasiojulikana eneo la Nyakato mkoani Mwanza
Padri Alfonce alisema akiwa katika kituo kimoja cha mafuta eneo la Nyakato wiki iliyopita, alishangaa kuona kwa mbali kikundi cha watu kikimtazama na baadhi yao wakioneshana vidole kumwelekea alipokuwa ameegesha gari.
Padri huyo aliongeza kuwa, wakati anaondoka baada ya kuweka mafuta katika gari, watu wawili waliokuwa katika pikipiki walimfuata, kwa mwendo wa kasi jambo lililompa wasiwasi.
“Nilipata hofu na kuongeza mwendo huku nikijitahidi kuzuia wasinipite, na kubadili mwelekeo na kuingia mtaa mwingine.
“Watu hao nao walikata kona na kunifuata, wakijaribu kunisogelea zaidi, lakini walishindwa kunipita kwa sababu njia ilikuwa na msongamano kidogo wa watu,” alisema.
Padri huyo alisema alibadili tena mwelekeo na kuingia mtaa mwingine, lakini bado alizidi kuandamwa na alipoona hakuna usalama, alilazimika kuegesha gari karibu na nyumba moja na kukimbilia ndani.
“Najua hata wenyeji wangu walinishangaa, na sikutaka kuwapa hofu, bali nilitulia na kuanzisha mazungumzo mengine, lakini akili na masikio yangu yakiwa nje,” alisema.

Aliongeza kuwa watu hao walisimama mbele kidogo na alipoegesha gari lake, na baada ya kusubiri kwa muda mrefu waliondoka, na alipohakikisha kuna usalama aliondoka kurejea nyumbani.
Alisema kabla ya tukio hilo, Jumatatu wiki iliyopita, majira ya saa moja usiku watu watatu wenye asili ya Kiarabu wakiwa na gari, walifika katika makazi ya mapadri hao huko Bugando na kutaka kuonana na mmoja wao.
“Walimlazimisha mlinzi awaoneshe kwanza padri ambaye hawakuweza kumtaja jina, lakini walipobanwa, wakasema wanamtaka yeyote aliyepo.
“Mlinzi alipowauliza shida yao na kwa nini waje usiku, watu hao walikuja juu wakitaka waruhusiwe kumwona padri, na kwamba sio kazi ya mlinzi kuwahoji,” alisema.
Akizungumzia hali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, alidai kutojua tukio hilo.
“Sijapata taarifa hiyo. Lakini nataka kusema wazi kuwa watu wasiogope kwa sababu kuna ulinzi wa kutosha, na kama mtu anahisi kuwepo kwa hatari atoe taarifa mara moja,” alisema.
Hata hivyo, alionya dhidi ya watu wanaojaribu kuleta hofu miongoni mwa wananchi, na kwamba jeshi hilo litamchukulia hatua yeyote anayesambaza vitisho dhidi ya viongozi na waumini wa dini.

No comments:

Post a Comment