zombi amesahau kuvaa viatu. |
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, ametangaza kikosi kazi kinachounda tume itakayochunguza chanzo cha kufeli kwa asilimia 60.5 ya watahahiniwa wa Mtihani wa Kidato cha IV mwaka jana nchini.
Tume hiyo inayoundwa na watu mbalimbali wakiwamo wabunge, wasomi, viongozi kutoka taasisi za kidini na wadau wa elimu, ilitangazwa jana jijini Dar es Salaam na itaongozwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini, Profesa Sifuni Mchome.
Waziri Mkuu Pinda aliwataja wajumbe wengine wa tume hiyo kuwa ni pamoja na James Mbatia Mbunge wa kuteuliwa, Bernadetha Mshashu Mbunge wa Viti Maalumu na Abdul Marombwa Mbunge wa Kibiti.Wengine ni Profesa Mwajabu Possi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Honorath Chitanga Makamu wa Rais Chama cha Walimu Tanzania(CWT), Daina Matemu Katibu, Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari
Tanzania (TAHOSSA).Wajumbe wengine ni Rakhesh Rajan, Katibu Mtendaji wa Shirika lisilokuwa na Kiserikali (NGO) Twaweza.Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi nchini (TAMONGSCO), Mahmoud Mringo na Mratibu wa Taasisi ya Kukuza Mitalaa, Kizito Lawa.Wengine ambao watatoka katika taasisi za dini ni Peter Maduke ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Kikristo la Huduma za Kijamii (CSSC), Nurdin Mohamed Mkuu wa Chuo cha Ualimu Alharamain iliyopo chini ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata).Wajumbe wa kutoka Zanzibar ni Suleiman Hemed Khamis mjumbe kutoka Baraza la Wawakilishi, Abdalla Hemed Moh’d wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA ) na Mabrouk Jabu Makame wa Baraza la Elimu Zanzibar.Akitangaza kuundwa kwa tume hiyo Pinda alisema matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012, yameonyesha kuwa kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa kiasi kikubwa, ikilinganishwa na mwaka 2011.Matokeo hayo yameonyesha kuwa kati ya wanafunzi 397,132 waliofanya mtihani huo, watahiniwa 126,851 ndiyo waliofaulu.“Katika idadi hii ya wanafunzi waliofaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu ni 23,520 na daraja la nne ni 103,327. Watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 65.5 wamepata daraja 0,” alisema Waziri Mkuu akiongeza: “Kutokana na matokeo haya mabaya, Serikali imeamua kuunda tume hii itakayochunguza tatizo hili kwa madhumuni ya kupata ufumbuzi wa kudumu.”
Alisema kuwa tume hiyo itakuwa na kazi nyingi ikiwa ni pamoja na kubainisha sababu za matokeo hayo kuwa mabaya, kutathmini nafasi za halmashauri katika kusimamia elimu ya sekondari na kuainisha sababu nyingine zinazoweza kuchangia hali ya matokeo hayo.
No comments:
Post a Comment