RAIS wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania, Dk. Malima Bundara, ameitaka Serikali kuwapa kipaumbele wahandisi wazawa pindi kazi za ujenzi zinapopatikana. Amesema kuwa, pamoja na kwamba Serikali haiwezi kufanya kazi na wahandisi wa kigeni, kuna haja wahandisi wazawa wakapewa kipaumbele kwa kuwa nao wanauwezo wa kufanya kazi katika viwango vinavyokubalika.
Dk. Bundara aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa wahandisi ulioandaliwa na taasisi hiyo kujadili umuhimu wa wahandisi katika utatuaji wa changamoto mbalimbali zinazokabili nchi katika sekta ya uhandisi.
“Changamoto za zinazoikabili sekta ya uhandisi nchini, zitapatiwa ufumbuzi endapo uhusishwaji wahandisi wa ndani utapewa kipaumbele tofauti na ilivyo sasa.
“Sekta ya uhandisi inakabiliwa na changamoto nyingi lakini changamoto hizo zitaweza kupatiwa ufumbuzi endapo wahandisi wa wazalendo watahusishwa katika kutatua matatizo hayo kwa sababu wana uwezo mkubw atofauti na inavyofikiriwa.
“Tusijidanganye kuwa wahandisi wa kigeni watatoa ufumbuzi wa muda mrefu wa matatizo tuliyonayo kama nchi kwani wao wamekuja kutafuta pesa na kurudi nazo kwao. Kitu tunachotakiwa kufanya ni kuwajengea uwezo wahandisi wetu wa ndani ambao watatoa majibu ya changamoto zinazoikabili miundombinu yetu ambayo inaathari ya moja kwa moja katika uchumi wa nchi,” alisema Dk. Bundara.
Aliitahadharisha Serikali akitaka wahandisi wazalendo watafute ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazorudisha nyuma maendeleo ya nchi na pia aliwataka wahandisi wa ndani waache kulalamika badala yake wachukue hatua ili kusaidia kukuza uchumi wa taifa.
“Nguzo ya ukuaji kwa uchumi katika kila nchi ni upatikanaji wa miundombinu imara na inayoeleweka na maendeleo ya miundombinu na kukua kwa sekta ya viwanda ipo mikononi mwa wahandisi. Kama Serikali na taasisi zake itawatumia vizuri wahandisi wazalendo, mapinduzi ya haraka katika uchumi wa nchi yatapatikana,” alisema.
Naye, Rais wa Zamani wa taasisi hiyo, Mhandisi Ladislaus Salema, alishangaa ni kwa nini Tanzania bado inakabiliwa na tatizo la ajira kwa wananchi wake.
Kutokana na hali hiyo, aliitaka Serikali ifanye kazi kwa karibu na wahandisi, ili kulikwamua taifa katika janga la ukosefu wa ajira.
Kwa upande wake, Mhandisi Shabbir Khataw, aliwaonya wahandisi wenzake na kuwataka wafanye kazi kwa bidii kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kulikwamua taifa kutoka katika shida zilizopo
No comments:
Post a Comment