Tuesday, March 12, 2013

MAHAKAMA:DPP hana mamlaka ya "nani apewe dhamana na nani anyimwe."


JAJI wa Mahakama Kuu Zanzibar, Abraham Mwampashi, amesema Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) hana mamlaka ya kuiamuru mahakama nani apewe dhamana na nani anyimwe.

Alisema hayo alipokuwa akitoa hukumu juu ya kesi ya viongozi 10 wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu wanaomlalamikia kufungwa dhamana yao na Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar Ibrahim Mzee Ibrahim.

“Mkurugenzi wa mashitaka hana mamlaka ya kusema nani apewe dhamana na nani asipewe, ingawa anayo haki ya kumzuia ofisa yeyote wa polisi asitoe dhamana,” alisema Jaji Mwampashi.

Alisema kwamba katika misingi ya utawala wa sheria na utawala bora, mahakama ni muhimili unaojitegemea, suala la dhamana linaendelea kubaki kuwa la mahakama, si kwa Mkurugenzi wa Mashitaka.

Kutokana na uamuzi huo Jaji Mwampashi
aliwataka wadai kuwasilisha ombi jipya la dhamana, lisikilizwe na kutolewa uamuzi na Mahakama Kuu, si Mrajis wa mahakama kama ilivyokuwa hapo awali.

Pia, Jaji Mwampashi alisema DPP alipaswa kuweka wazi sababu za kukataa dhamana kutolewa kwa walalamikaji ili mahakama iweze kupima uzito wake na wahusika waweze kujitetea.

Kwa msingi huo alisema Mahakama Kuu imefuta maamuzi yote yaliyokuwa yametolewa na Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar, Geroge Kazi, yakiwemo ya kufunga dhamana ya watuhumiwa baada ya kuridhia hoja ya DPP ya kuzuia dhamana hiyo.

“Maamuzi ya Mrajis yote yanafutwa kwa sababu hakuwa na mamlaka kisheria kupokea ombi la dhamana pamoja na kulitolea maamuzi, wakati kesi imefunguliwa Mahakama Kuu,” alisema Jaji Mwampashi.

Katika mahakama hiyo ambapo kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi wenye silaha za moto, Jaji Mwampashi alihoji kuna haja gani kuwa na mahakama, kama mtu mmoja anakuwa na haki ya kunyang’anya uhuru wa mtu mwingine?

Tangu kuanza kwa kesi hiyo Oktoba 25, mwaka jana, mawakili wa utetezi wamekuwa wakipinga kitendo cha DPP kufunga dhamana.

Jaji Mwampashi alisema sheria iliyotumiwa na DPP kufunga dhamana ya watuhumiwa ambayo ni Ibara ya 19(1)(2) inampa uwezo wa kumuagiza ofisa wa polisi peke yake, si mahakama.

Alisema DPP alichotakiwa kueleza wakati wa kupinga dhamana ni sababu zipi za kuishawishi mahakama isitoe dhamana kwa watuhumiwa.

Hata hivyo alisema hawezi kufuta kibali cha DPP cha kufunga dhamana kwa sababu hakupewa nafasi ya kuja mahakamani kutetea hoja yake, lakini aliutaka upande wa walalamikaji kuwasilisha upya ombi la dhamana Mahakama Kuu.

Viongozi hao wakuu wa Uamsho wanakabiliwa na mashitaka manne yanayohusiana na kuharibu mali na kuhatarisha usalama wa taifa kinyume cha kifungu cha 3(d) cha Sheria ya Usalama wa Taifa, Sura ya 47, ya mwaka 2002.

Washitakiwa hao ni masheikh Farid Hadi Ahmed, Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Issa, Azzan Khalid Hamdan, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakari Suleiman, Gharib Ahmada Omar, Abdalla Said Ali na Fikirini Majaliwa Fikirini.

Tangu kesi yao ilipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 25, mwaka jana, wamekuwa wakirudishwa rumande kwa sababu DPP ametoa kibali cha kufunga dhamana kwa muda usiojulikana.

Watuhumiwa hao walifungua kesi Mahakama Kuu kutaka ifanye mapitio maamuzi ya Mrajis na kuyatengua, pia ifute maamuzi ya DPP kufunga dhamana yao.

Watuhumiwa hao wanatetewa na mawakili wanne wakiongozwa na Salum Toufiq, Abdalla Juma Mohamed, Rajab Abdalla Rajab pamoja na mwanasheria maarufu Suleiman Salim.

Kutokana na uamuzi wa Jaji Mwampashi, kesi ya msingi itasubiri kupangiwa jaji ili kujulikana siku ya kutajwa kwake.

No comments:

Post a Comment