Wednesday, March 13, 2013

MAASKOFU na jicho la chuki kwa Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete


Habari za ndani ya serikali na ndani ya makanisa zimethibitisha pasipo shaka kwamba karibu maaskofu wote wakubwa nchini walipata ujumbe wa dharura wa kuonana na uongozi wa juu wa nchi wiki iliyopita lakini hawakwenda isipokuwa mmoja tu.

Kwa mujibu wa habari hizo, aliyekwenda kuonana na viongozi wa serikali ni askofu mmoja ambaye naye baada ya kubanwa na wenzake alidai kupotoshwa katika taarifa za wito wake, pamoja na kuwa alikiri kuwa na mahusiano mazuri na viongozi hao.



“Askofu (anamtaja jina) alikwenda kuonana na viongozi wa serikali, lakini alipoitwa msaliti alisema yeye aliitwa na kuambiwa kwamba wenzake wote wako katika kikao isipokuwa yeye ambaye amechelewa, lakini alipofika alijikuta yuko peke yake,” anasema mtoa habari wetu.

Sintofahamu kati ya viongozi wa makanisa wakiwamo maaskofu ilitokea siku moja kabla ya kikao cha viongozi hao wa kiroho kilichoitishwa na Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) kujadili hali ya nchi na vurugu za kidini zilizoibuka nchini.

Katika kikao hicho kilichofanyika Ijumaa iliyopita katika Kituo cha Mikutano na Mafunzo cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Kurasini, jijini Dar es Salaam, kilijadili kwa kina hali ya kisiasa na kijamii nchini na kuunda jopo la wataalamu litakalotoa tamko zito.

Katika mkutano huo, baadhi ya viongozi walitoa matamko mazito na ambayo hayaashirii dalili njema kati ya viongozi wa makanisa na serikali, hali iliyochochewa na tukio la kujeruhiwa vibaya kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda.

Mbali ya kujadili kwa kina tukio la kujeruhiwa kwa Kibanda, viongozi hao wa makanisa walijadili matukio mengine yakiwamo mauaji ya viongozi wa dini ya Kikristo, akiwamo Mchungaji Kachira pamoja na Padri wa Kanisa Katoliki Visiwani Zanzibar, Evaristus Mushi. Pia walijadili kesi zipatazo 16 zinazowahusu viongozi wa Kikristo.

“Mmoja wao (askofu) alikiambia kikao hicho kwamba haridhishwi na jinsi serikali ilivyochukua hatua kuhusiana na matukio yanayohusu uhalifu dhidi ya Wakiristo kama vile uchomaji wa makanisa na kujeruhiwa na hata kuuawa kwa viongozi wa kiroho. Alikiambia kikao kwamba si busara kuwataka kukutanishwa bila kuona hatua zinazochukuliwa na serikali,” anasema.

Kiongozi mwingine mwandamizi katika uongozi wa Kanisa Katoliki nchini alikiambia kikao hicho kwamba kuna kila dalili kwamba serikali imekiuka katiba na inastahili kuchukuliwa hatua zinazostahili.

Mkutano huo ulioratibiwa na TCF kwa pamoja na makanisa yote makuu nchini, uliwahusisha maaskofu, wenyeviti na makatibu wakuu wa makanisa yote nchini yanayounda TCF.

Mkutano huo wa TCF uliitishwa ikiwa ni takriban miezi miwili tu kupita baada ya viongozi hao wakuu wa dini ya Kikristo kukutana na kutoa tamko kali kutokana na kile walichodai ni kutafakari kwa undani juu ya kuzorota kwa uhusiano baina ya dini mbili za Ukristo na Uislamu nchini, pamoja na kutathmini juu ya wajibu wa Kanisa na utume wake wa kinabii kwa taifa.

TCF, ambayo inajumuisha taasisi kuu za umoja wa makanisa nchini, ambazo ni Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (PCT) na Kanisa la Waadventisti Wasabato (SDA-Observers), katika tamko lao hilo la Desemba mwaka jana walisema:

“Katika nyakati zetu hizi, tunashuhudia fadhaa na migogoro mingi ya kijamii. Kuna hasira kubwa ya chini chini inayotokana na kasoro nyingi za kiutendaji katika mihimili mikuu ya uongozi na utando mkubwa wa ufukara wa kutupwa kwa wananchi wengi usio na matumaini ya kumalizika hivi karibuni.

“Hatari ya hali hii ni dhahiri kwamba makundi nyemelezi (kisiasa, kiuchumi na kidini), kwa kutumia vikundi halifu vilivyo katika hali ya ufukara na migogoro, yatavielekeza kimapambano na kiharakati kutetea kijeuri ajenda hasimu za wale walio madarakani au washindani wao kwa masilahi ya wanyemelezi.

“Hali tunayoelezea si ya kufikirika, kwani ndiyo inayotokea huko nchini Nigeria, Kenya na nchi za Afrika ya Kaskazini hivi sasa.

“Tanzania haina kinga ya kipekee kuiepusha kukumbwa na maovu ya namna hiyo bila utaratibu na vyombo thabiti kuhimili mienendo hasi kama hii.

“Kutokana na matukio na kauli zinazotolewa na watu mbalimbali hapa nchini, inawezekana tayari wanyemelezi wako kazini wakiongoza vikundi kusukuma ajenda za kutekeleza masilahi yao.”

Aidha, mkutano huo wa Desemba ulitaja mambo saba ambayo yanapaswa kufafanuliwa na kudhibitiwa na dola mapema ili yasiendelee kupotoshwa.

Mambo hayo ni pamoja na hali ya kuzorota kwa uhusiano pamoja na kashfa dhidi ya kanisa, hadhi ya Baba wa Taifa kuhifadhiwa, ‘Memorandum of Understanding’ (M.o.U) ya mwaka 1992, hujuma ya kuchomwa makanisa na mali za kanisa, dhana ya kwamba Tanzania inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo, matumizi hasi ya vyombo vya habari vya kidini na aina yoyote ya matukio yanayosababisha hasira na kutenda maovu.

“Tunaitaka serikali yetu na vyombo vyake vya usalama, sheria na amani kutendeka mara moja bila kuchelewa, katika nyakati ambazo vikundi halifu kisiasa au kidini vinapoanza uchochezi ili kupambanisha wanajamii.

“Tabia ya kuachia uchochezi wa kidini kuendelea pasipo hatua madhubuti kuchukuliwa na dola ni udhaifu mkubwa wa uongozi na uwajibikaji.

Ikithibitika kwamba uharibifu uliofanywa ulitokana na kikundi mahususi chini ya uongozi wa dini au chama cha kisiasa au asasi isiyo ya kiserikali, basi taasisi husika iwajibishwe na kulipa fidia kwa uharibifu uliofanywa,” TCF ilisisitiza katika moja ya maazimio hayo.

No comments:

Post a Comment