Thursday, August 29, 2013

...KESI YA SHEKH PONDA, KAULI YA PONDA INA HOJA YA KUJADILIWA

UPANDE wa Jamhuri, umeiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro kuwa umekamilisha
upelelezi wa kesi inayomkabili Katibu wa Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda.
Wakili wa Serikali, Bernard Kongola, alidai upelelezi umekamilika na watawasilisha vielelezo mbalimbali, vikiwamo DVD, kibali cha mkutano na hukumu yenye Kumbukumbu namba 245/2012, iliyotolewa na Hakimu V. Nongwe wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mjini Dar es Salaam.


Alidai ushahidi mwingine ni mashahidi 15 ambao wako tayari kutoa ushahidi wao na kuiomba kutaja tarehe ya kusikilizwa shauri hilo.

Awali mahakama hiyo, iliahirisha kesi hadi Septemba 17, mwaka huu, ili kutoa uamuzi wa kupewa dhamana au kunyimwa.

Sheikh Ponda anakabiliwa na mashitaka matatu ambayo alisomewa jana mahakamani hapo, mbele ya Hakimu wa Hahakama hiyo, Richard Kabate, ambapo alikayana na kukubali baadhi ya vipengele.

Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Bernard Kongola, alidai shtaka la kwanza Agosti 10, mwaka huu,  eneo la Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, mshitakiwa aliwaambia Waislamu wasikubali uundaji wa kamati za ulinzi na usalama misikitini.

“Ndugu Waislamu, msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti, kwani kamati hizo zimeundwa na BAKWATA ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na kama watajitokeza kwenu watu hao na wakajitambulisha wao ni kamati za ulinzi  na usalama za misikiti, fungeni milango na madirisha ya msikiti yenu na muwapige sana”, kauli ambayo iliumiza imani za watu wengine.

Wakili huyo, alidai hatua hiyo ni kinyume cha agizo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mjini Dar es Salaam, iliyotolewa na Hakimu V. Nongwa Mei 9, mwaka huu, ambayo ilimtaka Sheikh Ponda ndani ya mwaka mzima kuhubiri amani, ambayo ni kinyume na kifungu cha sheria namba 124 cha mwaka 2002.

Katika shitaka la pili, wakili huyo alidai Agosti 10, mwaka huu, katika eneo la Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro na Mkoa wa Morogoro, mshitakiwa alitoa maneno yenye nia ya kuumiza imani nyingine za dini kwa kuwaambia Waislamu: "Serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi

wake ni Waislamu, lakini Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji, baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo".

Mwanasheri huyo, alidai maneno hayo yaliumiza imani za watu wengine  ambalo ni kinyume cha kifungu cha sheria 129 cha mwaka 2002.

Katika shitaka la tatu, ilidaiwa mahakamani hapo na wakili huyo kuwa  Agosti 10, mwaka huu, eneo la Kiwanja cha Ndege, mshitakiwa aliwashawishi Waislamu kujumuika kinyume cha sheria na kuwaambia kuwa "Serikali ilipeleka jeshi Mtwara

kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu, lakini serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipotaka Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji, baada ya kudai ni mali yao  kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo”,  na kudai kuwa  ni maneno ambayo yalikuwa yakiumiza imani za watu wengine na kwamba kufanya hivyo ni kinyume cha kifungu cha sheria namba  390 na kanuni ya adhabu namba 35 cha mwaka 2002.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo na kukana, Hakimu Kabate alimpa nafasi mshitakiwa, ambapo alisema anakubali tarehe ya mkutano ambayo ni Agosti 18, mwaka huu, tarehe ya kukamatwa akiwa jijini Dar es Salaam Agosti 11, mwaka huu na jina lake ambalo ni Ponda Issa Ponda.

Mshitakiwa, alipotakiwa kusaini maelezo hayo, wakili wake, Juma Nassor aliiambia mahakama kuwa hawezi kwa kuwa anatumia mkono wa kulia ambao alipigwa risasi, hivyo mahakama kukubali na kusaini kwa kutumia dole gumba la mkono wa kulia.

Hata hivyo, wakili wa utetezi, Juma Nassor, aliiomba mahakama impatie dhamana mteja wake katika mashitaka yote matatu aliyoshitakiwa, pamoja na maelezo ya mlalamikaji kwa ajili ya kuandaa utetezi.

Wakili wa Serikali, alisema ombi la dhamana halina msingi, kwa kuwa tayari  waliwapa upande wa washitakiwa nakala ya cheti kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka, DPP, inayopinga dhamana kwa mshitakiwa.

Alidai DPP anayo mamlaka ya kupinga dhamana kwa kutoa cheti na alikubali ombi la kumpa maelezo ya mlalamikaji.

No comments:

Post a Comment