Friday, October 18, 2013

Benki zapewa bilioni 16 kwa mikopo ya nyumba

KAMPUNI mahususi ya Kutafuta Fedha na Kutoa Mikopo ya Muda Mrefu ya Nyumba ya Tanzania Mortgage Refinance Company Limited (TMRC ), imeziwezesha benki nne wanachama wake, Sh bilioni 16.45 kwa ajili ya mikopo ya nyumba tangu ilipoanzishwa. Ofisa Mtendaji Mkuu wa TMRC, Oscar Mgaya alisema hadi kufikia sasa benki nne ambazo ni wanachama zimenufaika na mkopo huo.

Alizitaja benki hizo kuwa ni Azania Bank , Bank of Africa (BOA), Benki ya Exim na DCB Commercial Bank.

Kampuni hiyo imelenga kuhakikisha benki hizo ambazo pia ni wanahisa kwenye taasisi hiyo zinanufaika na mikopo rahisi kwa vile ina dhamira iliyolenga katika kuwakomboa wananchi kujenga na kumiliki nyumba nzuri kwa gharama nafuu.


Benki za biashara ambazo ni wanachama wa taasisi hiyo ya TMRC zinafikia takribani 11 ambazo ni pamoja na National Microfinance Bank (NMB ), Benki ya CRDB Plc, Benki ya Taifa ya Biashara ( NBC ), Exim Bank, Azania Benki, Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB ), DCB Commercial Bank Plc , NIC Bank, Banc ABC , Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) na Benki ya Afrika Tanzania (BOA).

Mgaya alisema bado kuna nafasi kwa benki nyingine kununua hisa kwenye kampuni hiyo ya TMRC.

“Hakuna vikwazo vyovyote kwa benki nyingine au taasisi nyingine kushiriki kwa usawa wa umiliki wa hisa kwenye kampuni ya TMRC. Ni kampuni iliyo na uwazi na hakuna vikwazo juu ya kuingia kwa wawekezaji makini,” alisema.

Kampuni ya TMRC iliundwa kama sehemu ya mpango wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia kuhuisha upatikanaji wa mikopo ya ujenzi wa nyumba kwa wananchi nchini.

Uanzishwaji wa kampuni ya TMRC ni miongoni mwa vipengele vitatu vya Mradi wa Nyumba Tanzania (HFP) ambao umelenga kuleta maendeleo kwenye sekta ya mikopo Tanzania.

TMRC kwa sasa inatumia mkopo wa Benki ya Dunia kuzikopesha benki wanachama nchini.

No comments:

Post a Comment