Tuesday, October 22, 2013

kesi ya #SIMCARD_TAX yawekwa kiporo tena!

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilishindwa kusikiliza maombi ya zuio la muda la kodi ya simu, yaliyowasilishwa mahakamani hapo na Chama cha Kutetea Walaji Tanzania (TCAS).

TCAS kiliwasilisha maombi hayo mahakamani hapo kikiomba mahakama itoe amri ya kuzuia kwa muda utekelezaji wa kodi ya simu, kusubiri usikilizwaji na hukumu ya kesi yao ya msingi ya kikatiba waliyoifungua mahakamani.

Maombi hayo ya zuio la muda yalitarajiwa kusikilizwa jana na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, linaloongozwa na Jaji Aloyisius Mujuluzi akisaidiana na Jaji Lawrence Kaduri na Jaji Salvatory Bongole.


Hata hivyo, usikilizwaji wa maombi hayo ulishindikana jana kutokana na Jaji Mujuluzi kutokuwepo, badala yake iliahirishwa na Jaji Kaduri hadi Oktoba 31, mwaka huu.

Katika kesi hiyo ya msingi, TCAS kinapinga Sheria ya Fedha Namba 4 ya Mwaka 2013 marekebisho yaliyoingiza tozo ya kodi ya Sh1,000, kwa kila mtumiaji wa simu za mkononi kila mwezi.

TCAS katika kesi hiyo ya msingi iliyofunguliwa chini ya hati ya dharura, ikiiomba Mahakama Kuu itamke kuwa sheria hiyo ya tozo ya kodi ya simu ni kandamizi .

Wanadai kuwa watumiaji hao si tu kwamba hawana uwezo wa kulipa tozo hiyo, bali pia hawana uwezo wa simu zao kuwa na muda wa maongezi.

Mbali na TCAS, wadai wengine katika kesi hiyo ni kampuni tano za huduma za simu za mkononi za Tigo, TTCL, Airtel, Vodacom na Zantel, ambayo yaliomba na kuruhusiwa na mahakama kuunganishwa katika kesi hiyo, siku chache baada ya kufunguliwa na TCAS.

No comments:

Post a Comment