MKUU wa Gereza la Mahabusu Keko, Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP), Mbwana Senashida, anadaiwa kuchukua sh milioni 14 za Mfuko wa Maafa wa Wafanyakazi wa gereza hilo na kufanyia biashara zake.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya gereza hilo kiliieleza jijini Dar es Salaam jana kuwa mkuu huyo tangu afike hapo amekuwa akizitumia fedha hizo kinyume na malengo yaliyokusudiwa ya kumsaidia mfanyakazi pindi anapopata maafa.
Mkuu huyo anatuhumiwa kuzichukuwa fedha hizo kuendeshea biashara ya duka lake la kuuza vinywaji vikali, linalojulikana kwa jina la ‘Recreation Contena’.
Hali hiyo, imekuwa ikisababisha manung’uniko kutoka kwa wafanyakazi ambao wengi wao huutegemea mfuko huo wanapopata matatizo.
Chanzo hicho kilisema baada ya fedha hizo kuwa mikononi mwa watu, bila ya sababu za kueleweka, wanachama wa mfuko huo walikutana kwa ajili ya kusomewa mapato na matumizi ambapo baada ya kukamilika kikao hicho kiliazimia fedha hizo zigawanywe kwa kila mwanachama.
Hata hivyo, mgao huo haukufanyika baada ya wanachama kuambiwa kuwa mkuu wa gereza amekwenda mkoani Kilimanjaro huku akiwa na fedha hizo bila ya taarifa, kitendo kilichowakatisha tamaa ya kuzipata fedha zao.
Pia mkuu huyo wa gereza anadaiwa kuchukua misaada iliyotolewa na kikundi cha Waislamu cha DYCC, wakati wa Sikukuu ya Idd El Haj ya mwaka jana na mwaka huu na kwenda kuuza kwa manufaa yake, hivyo kufanya lengo la DYCC, kuwasaidia wafanyakazi hao kutokuwa na maana tena.
Chanzo hicho kilisema misaada aliyokuwa akifikisha ni ile ya wafungwa na mahabusu, huku ile ya wafanyakazi akiifanyia biashara tena kwa kuiuza kwenye duka la magerezani hapo.
Akijibu tuhuma hizo, mkuu huyo wa gereza alikana kufanya biashara na kusema yeye ni mtumishi wa Jeshi la Magereza.
Kuhusu fedha, alisema mgawo huo ulichelewa kutokana na mvutano uliojitokeza kwa wanachama wenyewe katika kukubaliana utumike utaratibu upi kutokana na baadhi yao kuwa na fedha nyingi na wengine kidogo.
Senashida alisema kutokana na mvutano huo ilibidi iundwe kamati ya watu wanne kutafuta utaratibu bora wa mgawo huo ambapo utakapotekelezwa utaondoa mashaka kwa kila mwanachama.
Aliwatoa wasiwasi kuwa fedha zao zipo, wasiwe na shaka kwani atakaporudi likizo Novemba 15 na kuipitia ripoti ya kamati hiyo na kuridhika nayo fedha hizo zitagawanywa.
Kuhusu msaada uliotolewa na DYCC, alisema si kama ameutumia kwa maslahi yake binasfi bali kilichotokea ni kuwa msaada ulioletwa ni kidogo ukilinganisha na wafanyakazi 300.
Alisema msaada huo hadi sasa umehifadhiwa stoo wakati wakitafakari jinsi ya kuugawa.
No comments:
Post a Comment